Hamis Wendo Mwinyipembe, mkazi wa Kijiji cha Gombero, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga ni miongoni mwa wananchi wengi walioonja suluba ya kunyanyaswa na vyombo vya dola pengine kwa kukosa uelewa wa sheria ama kufanyiwa vitendo hivyo kwa makusudi na wahusika.

Kwa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba wananyanyaswa na polisi kwa vipigo na kubambikwa kesi zisizowahusu, huku baadhi yao wakitumikia vifungo ama wamemaliza kutumikia vifungo hivyo katika magereza mbalimbali nchini.

Wendo ni miongoni mwa wananchi waliokumbwa na mikasa hiyo inayomwandama kwa miaka 24 sasa, tangu ndugu yake alipofariki kwa kinachoelezwa kuwa kipigo cha polisi.

Anasema mwaka 1992 shemeji yake aliyefahamika kwa jina la Rembo Juma, aliuawa kutokana na kupigwa na polisi bila kuhusika na kosa lolote.

Marehemu Juma alikamatwa na polisi Jumanne, Machi 10, 1992 saa 1:00 usiku akiwa nyumbani kwake Barabara ya 17 katika msako wa nyumba kwa nyumba ambako waliwapiga raia wakiwamo wapita njia.

Madai ya polisi hao ilikuwa ni kuwasaka watu waliodaiwa kuwa wahalifu waliowapiga askari waliokuwa katika majukumu yao. Waliendesha msako bila kuongozana na mjumbe wa nyumba kumi na kuwatoa ndani ya nyumba wanawake na wanaume huku wakiwapiga.

Askari hao walipoingia katika nyumba namba 7, kitalu namba 130, eneo la Ngamiani ambayo ni nyumba ya marehemu Juma na kumkuta akiwa amepumzika na familia yake, na bila kumweleza walifika hapo kwa suala gani, walianza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili.

Kwa ukatili uliovuka mipaka, waliendelea kumpiga kwa muda mrefu mbele ya familia yake akiwamo mkewe na watoto wake na kumburuza hadi nje ya nyumba walikokuwa wamesimamisha gari lao kisha kumtupa ndani ya gari hilo.

Akiendelea kuelezea kisa hicho, Mwinyipembe anasema miongoni mwa askari wanne waliokuwa wameingia ndani ya nyumba hiyo na kumshambulia kwa kipigo Juma, wawili walifahamika kwa jina moja moja akiwamo Elirindia na Olomi. Waliondoka na watu waliokuwa wamewakamata baada ya kuwashambulia kwa kipigo hadi kituo cha Polisi cha Chumbageni mkoani Tanga.

Siku iliyofuata Machi 11, 1992 walifanya mchujo wa kuwabaini waliohusika na wasiohusika na kitendo cha kuwashambulia askari waliokuwa katika majukumu yao; walimwachia Juma (marehemu) na wenzake walipojiridhisha kwamba hawakuhusika.

Akiwa analalamikia maumivu makali aliyoyapata sehemu za kichwani, kifuani na tumboni na wenzake waliokuwa wanalalamikia majereha waliyoyapata kutokana na kipigo cha polisi na kuumwa na mbwa wa jeshi hilo, waliomba wapatiwe fomu ya PF3 wakapatiwe matibabu, lakini walikataliwa. 

Kutokana na hali yake kuwa mbaya na kunyimwa PF3 ilimpasa kurudi nyumbani bila matibabu, hivyo kutwa nzima alikuwa akilalamika kuwa na maumivu makali kichwani, kifuani, tumboni na uvimbe mgongoni.

“Hali yake ilizidi kubadilika huku akiendelea kuwa na maumivu makali mno, ndipo Machi 12, 1992 tukamrudisha tena Kituo Cha Polisi cha Chumbageni ili kuomba tupatiwe fomu hiyo akatibiwe, lakini tulikataliwa tena.

“Tuliamua kumpeleka katika Hospitali binafsi ya Jafari iliyoko Barabara ya 16, lakini madaktari tuliowakuta nao walikataa kumtibu bila kuwa na PF3,” anasema.

Baada ya kukosa matibabu katika hospitali hiyo, anasema waliamua kumpeleka katika Hospitali ya Serikali ya Ngamiani. Hata hivyo, daktari alikataa kumhudumia bila kuwa na fomu hiyo na hivyo wakaamua kumrudisha nyumbani na kununua dawa ya kupunguza maumivu dukani (Panadol) ili kumpunguzia maumivu aliyokuwa nayo.

Machi 13 hadi 26, 1992 hali ya mgonjwa ilizidi kuwa mbaya kila siku, hivyo Machi 27, mwaka huo huo waliamua kumpeleka mgonjwa Hospitali ya Serikali ya Makorora. Dk. Jane alimpokea na kukubali kumpatia huduma ya kwanza baada ya kuona hali ya mgonjwa ni mbaya.

Anasema baada ya huduma hiyo ya kwanza, Dk. Jane aliandika barua apelekwe katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo. Hapo walipokewa na Dk. Mgonja ambaye alikataa kutoa matibabu kwa mgonjwa huyo bila kuwa na PF3.

Walimweleza kwamba polisi walikataa kutoa fomu hiyo tangu alipoiomba baada ya kuachiwa huru Machi 11, 1992; lakini aliwaagiza ndugu warudi tena katika kituo cha Polisi Chumbageni kuomba tena fomu hiyo na ikiwezekana askari hao wawasiliane naye kwa simu.

Lakini walipofika tena katika kituo hicho cha polisi walikutana na askari aliyefahamika kwa jina la Yassin akiwa kaunta, naye alikataa kuwapa fomu hiyo ya PF3 kwa maelezo kwamba wanaoruhusiwa kupewa ni wagonjwa waliofikishwa kituoni hapo. Hata alipoombwa azungumze na daktari kwa simu alikataa.

Iliwalazimu ndugu kurudisha majibu hayo ya polisi kwa daktari siku hiyo hiyo ya Machi 27 saa nne usiku na hivyo kukubali kumhudumia bila kuwa na fomu hiyo.

“Mgonjwa aliwekewa dripu na kufanyiwa vipimo vya X-ray ya kichwa na kifua, na Dk. Mgonja aliwaeleza kwamba picha hizo zinathibitisha kuumia sehemu za kichwa na kifua kwa kuwa damu ilikuwa inavuja ndani kwa ndani,” anasema. 

Madaktari waliendelea kumpatia matibabu, lakini ilipofika saa 5:45 usiku alifariki dunia. Machi 28, 1992 asubuhi ndugu walielekea katika kituo cha Polisi cha Chumbageni kutoa taarifa na kuandikisha maelezo kuhusu kifo hicho cha ndugu yao.

Anasema baada ya ndugu yao kufariki, madaktari waliwaeleza kwamba hawawezi kuwakabidhi mwili wa marehemu bila kibali cha polisi kutokana na mazingira ya kifo hicho. Kutokana na sharti hilo iliwalazimu kurejea tena kituoni hapo, ndipo wakapewa askari watatu walioambatana nao hadi hospitalini, lakini hawakumpata Dk. Mgonja.

Siku iliyofuata Machi 29, 1992 ndugu walirudi tena katika kituo hicho cha Polisi na kupewa tena askari watatu chini ya uongozi wa askari Stephen D/Stg C3427 na kufanikiwa kumpata Dk. Mgonja aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kutoa ripoti ya kifo hicho.

Anasema Dk. Mgonja alifanya uchunguzi na kubaini kwamba chanzo cha kifo cha ndugu yao ni kupasuka kwa baadhi ya viungo ndani ya kichwa na kifuani, vilivyosababisha damu kuvuja kwa wingi ndani ya mwili.

Kuvuja kwa damu ndani ya mwili wa Juma kulitokana na kipigo kutoka kwa polisi waliokuwa wamevamia nyumba yake siku ile na hivyo iliwalazimu kufungua jalada la uchunguzi lenye namba TAN/IR/1106/92.

Anasema wamefuatilia suala hilo hadi kwa Waziri Wa Mambo ya Ndani bila mafanikio yoyote kwani hakuna anayejali miongoni mwao – si RPC, DCI, IGP, DPP wala kiongozi yeyote na hivyo kusababisha mlolongo mwingine wa matukio dhidi yake ikiwamo kubambikwa kesi nyingi na polisi huku maisha yake yakiendelea kuwa hatarini kwa vitisho vya kila aina.

Novemba 16, 1992 walimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani wakilalamikia kitendo cha kuuawa kwa ndugu yao kutokana na kipigo kutoka kwa askari polisi bila kuwa na kosa lolote, lakini hawakupata jibu lolote.

Matukio mengine

Akiwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Magaoni, Kata ya Mabawa, Halmashauri ya Jiji la Tanga anasema kulitokea tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha mtaani kwake Septemba 23, 1993 ambalo liliwahusu askari wa kituo cha Polisi cha Mabawa.

Anasema alipofuatilia tukio hilo la wizi lililofanyika nyumbani kwa Mwalimu Saidi Omary usiku wa kuamkia Septemba 24 kwa kuwa alikuwa kiongozi wa mtaa huo, yaliyomkuta yanasikitisha.

Katika kufuatilia tukio hilo la uhalifu kwa vijana waliokuwa wakifanya ulinzi wa sungusungu, ambao walimweleza kwamba walipishana na askari polisi waliokuwa doria jirani na nyumbani kwa Omary na kuelezwa kwamba polisi wa Kituo cha Mabawa ndiyo waliohusika na wizi huo, polisi walimgeuka.

Kutokana na matukio hayo Desemba 2, 1993 alikwenda katika kituo hicho cha polisi kufuatilia matukio hayo likiwamo la kifo cha ndugu yake na hatua zilizochukuliwa, lakini alichoambulia ni kukamatwa, kupigwa na kuumizwa na polisi.

“Nilijeruhiwa sana na polisi, hivyo nikaomba fomu ya PF3 nilinyimwa kama ilivyotokea kwa marehemu Juma,” anasema Mwinyipembe akisimulia mikasa iliyompata katika kudai haki zake.

Anasema alikwenda kwa RPC, IGP na kwa Waziri wa Mambo ya Ndani (wakati huo alikuwa Augustine Lyatonga Mrema), kwa bahati mbaya hakuweza kumpata ofisini kwake baada ya kuelezwa kwamba alikuwa mjini Dodoma kwenye kikao cha Bunge.

Hivyo, aliamua kumfuata Dodoma bila mafanikio yoyote na kuelezwa kwamba yuko mkoani Kigoma kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika mwaka 1994.

Licha ya kukwama kwa jitihada zake za kumtafuta kiongozi huyo afikishe kilio chake kutokana na kunyanyaswa na askari polisi, hakuwa na namna nyingine ya kufikisha kilio chake isipokuwa kumwona Waziri Mkuu.

Alimwona katibu wa Waziri Mkuu na kueleza mlolongo wa matukio hayo likiwamo la kufariki kwa ndugu yake kwa kipigo cha polisi, na yeye kupigwa alipokuwa akifuatilia katika kituo cha polisi Mabawa na kubambikwa kesi kwa madai kwamba analisumbua jeshi hilo.

Katibu huyo aliyefahamika kwa jina la P. Tilwe, baada ya kusikiliza malalamiko hayo, aliandika barua kwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga ambaye alitoa maagizo kwa Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) kufuatilia malalamiko ya mwananchi huyo.

Anasema Machi 1994, alipokuwa amerejea mkoani Tanga baada ya jitihada zake za kumtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutozaa matunda, akiwa kituo kikuu cha mabasi alikamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu kwa mwezi mzima.

Wakati anakamatwa, polisi walimpokonya barua zake zote alizokuwa nazo na kuzichana. Hata hivyo, aliachiwa kwa dhamana.

Ndipo alipoamua kumwona Mkuu wa Wilaya ambaye aliwasiliana na OCD na kumwomba amsaidie aweze kupata haki zake, lakini ikatengenezwa kesi ambayo haikusikilizwa ila akahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Baada ya kutumikia kifungo hicho, yaliendelea kujitokeza matukio mengine yakiwamo kutishiwa kuuawa ambako mwaka 2003 alivamiwa na watu wawili anaowafahamu kwa majina na sura zao wakazi wa Kijiji cha Gombero, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga na kupigwa na kuporwa mali zake.

Anasema waliohusika kumshambulia na kumpora lori moja la maembe aliyokuwa ameangua kutoka katika shamba lake ni wanandugu wawili (majina yanahifadhiwa).

Kutokana na majeraha aliyokuwa ameyapata ilimlazimu kwenda kutibiwa katika Hospitali Teule ya Muheza, lakini daktari aliyeonana naye hakuweza kumtibu kwani alikuwa ni ndugu wa waliomjeruhi.

Dk. Twaha Zinga, anayedaiwa kukataa kumtibu, alitaka apatiwe barua kutoka kwa mtendaji wa kata na alipoipata alipatiwa huduma ya kwanza na hivyo kwenda kuripoti tukio la kushambuliwa katika kituo cha polisi na kupewa PF3, Januari 10, 2003.

Anasema pamoja na kuripoti tukio hilo huku afya yake ikiwa mbaya, alipofika nyumbani kwake alikutana na barua ya wito akiwa ameshitakiwa Baraza la Ardhi la Kata iliyoandikwa Januari 9, 2003.

Alipopata nafuu alikwenda kufungua kesi katika kituo cha Polisi cha Maramba Januari 15, 2003 na kupewa namba MAR/IR/22/2003.

Shauri hilo lilifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo na kupewa namba CC 19/2003. Kesi hiyo haikusikilizwa hadi leo hii na vielelezo vyote vimepotea.

Mwinyipembe amefuatilia mlolongo wa mashauri yake ambayo majalada yamepotea katika vituo vya polisi tangu mwaka 1992 ikiwa ni pamoja na Makao Makuu ya Polisi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Sheria na Katiba na Ofisi ya Waziri Mkuu bila mafanikio.

Anasema kutokana na mikasa mizito inayomkumba kila wakati huku ndugu zake wakiuawa na mwenyewe kutishiwa kuuawa, amefikia hatua ya kuziomba mamlaka husika kumpa kibali cha kwenda kuishi uhamishoni kama mkimbizi wa kwanza kutoka Tanzania kwani anaona nchini mwake hakufai tena kuishi.

Juni 25, 2015, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mkoa wa Tanga, aliijibu barua yake aliyomwandikia Juni 15, 2015 iliyohusu kupotea kwa jalada CC 19/2003 akimtaka kufika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Muheza ili aweze kukagua na kujiridhisha juu ya uwepo wa vielelezo hivyo na mazingira ya kufunguliwa kwa jalada mbadala na shauri liweze kuendelea.

Anasema hakuna kilichoendelea, hata pale IGP alipoitisha majalada yake yote hajayapata hadi sasa, hivyo polisi na Mahakama waliendelea kutoa taarifa za uongo kuanzia mwaka 1992 hadi 2016.

Pamoja na malalamiko aliyoyawasilisha kwa viongozi wa jeshi hilo mara kwa mara kuhusu kutotendewa haki na vyombo vya dola kwa miaka hiyo 24, aliandika tena barua nyingine Mei 20, 2015 kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na kujibiwa kwa barua yenye kumbukumbu namba CID/HQ/C.13/ 800/ VOL. V/ 28 ya Desemba 7, 2015 ikieleza kwamba majalada ya malalamiko yake yalipelekwa kwa Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali Mkoa wa Tanga.

“Kwa matukio mengine ya ukiukaji wa haki utakayofanyiwa unashauriwa uyatolee taarifa kwenye kituo cha polisi kilicho karibu ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na SACP Y.K. Ilembo kwa niaba ya DCI.

Pamoja na kuomba kupatiwa ufumbuzi wa madai yake kwa nyakati tofauti katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka, Waziri wa Sheria na Katiba, Jaji Mkuu wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani na Ofisi ya Waziri Mkuu hakuna msaada alioupata huku maisha yake yakizidi kuwa hatarini.

Anasema Aprili 5, 2016 yalitokea mauaji ya ndugu yake aliyefahamika kwa jina la Kibwana Salim, huko Kurasini Shimo la Udongo jijini Dar es Salaam yanayodaiwa kufanywa na askari polisi, pia.

Anasema polisi walimchukua Salim nyumbani kwake na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Kurasini na baadaye kuripoti kwamba aliuawa na wananchi wenye hasira.

“Haiwezekani, polisi wanamshikilia mtu halafu anakufa akiwa katika mikono yao wenyewe na kutoa taarifa za uongo kwamba ameuawa na wananchi.

“Polisi wameninyanyasa mno, ndugu zangu wameuawa bila hatia pamoja na kuripoti mapema taarifa za vitisho hivyo na huyu anauawa akiwa mikononi mwao, wanawasingizia wananchi. Nimefuatilia suala hili kwa viongozi wa polisi makao makuu bila mafanikio na sasa nimekuwa na mashaka makubwa na jeshi hili,” anasema.

Katika barua yake kwa DCI ya Juni 30, mwaka huu, kuhusu mauaji ya Salim, akimwomba aliitishe jalada namba DSM/PE/115/2016 alilolifungua dhidi ya RCO wa Temeke na wenzake, anaodai ndiyo waliohusika na kifo hicho.

Anasema amefikia uamuzi wa kumwomba DCI aingilie kati suala hilo, kwani tangu alipoelekezwa kufuatilia Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam hakuna jibu lolote alilolipata kwa zaidi ya miezi mitatu sasa tangu mauaji hayo yalipotokea.  

Mwinyipembe anasema maisha yake yamezidi kuwa hatarini na kuiona Tanzania si mahali salama pa kuishi, na badala yake Serikali imtafutie mahali pengine pa kuishi kama mkimbizi aliyeikimbia nchi iliyojaa manyanyaso, vitisho na mateso ya kila namna kwa raia wake wasiokuwa na hatia.

Hata hivyo, amesema anayo imani kubwa na Rais John Pombe Magufuli, hivyo kama karata ya mwisho anamwomba aingilie kati kumsaidia kupata haki yake iliyokandamizwa na polisi na Mahakama kwa miaka 24 sasa. 

Mwinyipembe anapatikana kwa simu: 0712  243 856. Anaomba msaada kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

By Jamhuri