Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetangaza kumsaka aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kukuza Maendeleo Vijijini (PRIDE Tanzania), Rashid Malima.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, John Mbungo, amesema Malima (65), anakabiliwa na tuhuma za kuchota Sh bilioni 1.8 ambazo ni mali ya PRIDE.

Habari za kufilisika kwa PRIDE zilianza kuandikwa kwa undani zaidi na JAMHURI kuanzia toleo Na. 337 na 338

chini ya kichwa cha habari ‘PRIDE inachungulia kaburi’. JAMHURI liliandika kuwa hali hiyo imesababishwa na kile kinachoelezwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha na ufisadi baada ya taasisi hiyo kuonekana kama haina mwenyewe.

TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilianza kuwachunguza viongozi wa PRIDE wanaohusishwa kwenye ufisadi huo.

Uchunguzi huo unafanywa ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kutolewa kwa taarifa ya Mkaguzi wa Ndani iliyosheheni maelezo ya namna viongozi wakuu wa PRIDE Tanzania walivyochota fedha. Ukaguzi huo ni wa Januari hadi Novemba, 2017 na taarifa yake iliwasilishwa kwenye kikao cha Bodi ya PRIDE cha Februari, mwaka huu (2018). Ulifanywa na Apolinary Mwijage (CPA).

Gazeti la JAMHURI lilipata nakala ya Ripori ya Mkaguzi wa Ndani inayoonyesha kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2017 pekee, fedha zilizotumika na ambazo hazina maelezo ya kuridhisha ni Sh bilioni 1.481.

PRIDE tayari ina wanachama zaidi ya 100,000 katika matawi 72 nchini kote.

Ilibainika kuwa kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa kikitolewa benki na kupelekwa kwenye ofisi ya malipo ambako baadaye kiliwafikia walengwa kwa kutumia nyaraka zilizoghushiwa na ambazo hazikuwa na viambatanisho kwa mujibu wa taratibu za fedha.

Malipo mengine yalifanywa kwa ‘mtu wa tatu’ kwa fedha taslimu badala ya hundi kama miongozo ya fedha za PRIDE inavyoagiza. Pia ilibainika kuwa malipo ya mamilioni ya fedha yalifanywa kwa kisingizio cha kuwalipa watoa huduma mbalimbali wa PRIDE, lakini mwishowe fedha hizo zikaingia kwenye akaunti za vigogo wa PRIDE.

Ilibainika kuwa Malima, kwa nyakati tofauti alichota Sh milioni 334.84; na baadaye alitoa kwenye akauti kiasi cha Sh milioni 275.582 kwa kutumia kadi ya AMEX (mwaka 2017 pekee).

Fedha nyingine, Sh milioni 213.048 zilitolewa na Meneja wa Fedha, Alfred Kasonka; Sh milioni 23.4 zilitolewa na Maltin Ndibaika; Sh milioni 338.204 zilitolewa kama malipo ya awali ya mishahara, lakini hakuna nyaraka za kuthibitisha hilo; Sh milioni 126.227 zililipwa kama marejesho ya mikopo lakini hakuna nyaraka; na kiasi kingine cha Sh milioni 170 hazijulikani zililipwa kwa shughuli gani.

Kwenye ukaguzi huo wa ndani ilielezwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kilidaiwa kutumika kuwalipa watoa huduma wa PRIDE, lakini kikawa kinawekwa kwenye akaunti binafsi za Mkurugenzi Mkuu Malima. Baadhi ya waliodaiwa kutoa huduma na wakaandaliwa malipo yaliyoishia kwenye akaunti ya Malima ni Arusha Art kwa ajili ya matengenezo ya magari ya PRIDE. Pia baadhi ya fedha anadaiwa kuzichukua kama malipo ya awali ya mishahara (salary advance), lakini baadaye kwenye mshahara wake akawa hakatwi. Kiasi kinachodaiwa kupotea kwa mtindo huo ni Sh milioni 338.204 ambacho ni cha kuanzia Januari hadi Novemba, 2017.

Mchanganuo wa baadhi ya fedha zilizochukuliwa na Malima ni kama ifuatavyo: Januari 26, 2017 zilichukuliwa Sh milioni 15 kupitia vocha Na. 166 kwa ajili ya malipo ya matengenezo ya gari kwa Arusha Art, lakini vocha ikasainiwa na Malima.

Februari 1, 2017 Malima alichukua Sh milioni 27 zikiwa ni malipo ya awali ya mshahara kupitia hundi Na. 364571. Vocha ya malipo haikusainiwa, lakini malipo hayo yaliingia kwenye akaunti iliyoko Benki ya BOA.

Februari 17, 2017 Malima alichukua Sh milioni 10 kwa vocha ya malipo Na. 341 kwenda kwa Arusha Art kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa matengenezo ya gari la ofisi. Fedha hizo zikawekwa kwenye akaunti yenye jina lake katika Benki ya BOA.

Machi 10, 2017 zilitolewa fedha taslimu Sh milioni 20 kwenda kwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari la ofisi. Hati ya malipo iliidhinishwa na Malima, na fedha taslimu zikaingizwa kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Benki ya Stanbic.

Machi 16, 2017 ilitolewa hundi yenye Na. 364659 kwa ajili ya usafiri. Imebainika kuwa malipo hayo hayakuidhinishwa na Meneja wa Fedha.

Tarehe hiyo hiyo zilitolewa fedha taslimu Sh milioni 15 kwenda kwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari la ofisi kwa hati ya malipo Na. 542. Hakuna invoisi wala stakabadhi iliyotolewa na mtoa huduma kuhalalisha malipo hayo.

Machi 17, 2017 inaonyesha kuwa zilitolewa fedha taslimu Sh milioni 15 kwa Antelope Safaris Ltd kugharimia safari za viongozi wa PRIDE. Muidhinishaji wa malipo alikuwa Malima, lakini hakuna invoisi wala risiti kutoka kwa mtoa huduma huyo.

Machi 27, kiasi kingine cha Sh milioni 17 kiliidhinishwa na Malima kwa kampuni hiyo hiyo ya Antelope kwa ajili ya safari ya viongozi wa menejimenti, lakini pia hakuna stakabadhi kutoka kwa mtoa huduma.

Machi 24, 2017 Sh milioni 5 ziliidhinishwa na Malima kwa ajili ya safari huku kumbukumbu zikionyesha kuwa Meneja wa Fedha hakuidhinisha malipo hayo.

Machi 24 vocha Na. 596 ilitumika kutoa Sh milioni 15 kwa ajili ya malipo ya matengenezo ya gari la ofisi kwa Arusha Art huku kukiwa hakuna risiti ya malipo hayo kutoka kwa mtoa huduma.

Aprili 12, 2017 Sh milioni 16 zinadaiwa kulipwa kwa Antelope Safaris Ltd kwa ajili ya safari za viongozi wa PRIDE, lakini hakuna risiti ya malipo kutoka kwa mtoa huduma. Badala yake, fedha hizo zikaingia kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Benki ya BOA.

Aprili 24, 2017 Sh milioni 26.5 zilitolewa kupitia hundi Na. 157621 kwenda kwa Essence International Ltd kugharimia mafunzo. Vocha ya malipo haikusainiwa na mtoa huduma, na badala yake fedha hizo zikawekwa kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima iliyoko Benki ya BOA.

Aprili 28, 2017 zilitolewa Sh milioni 2 kwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari la ofisi. Malipo yaliidhinishwa na Malima na hakuna risiti kutoka kwa mtoa huduma huyo. Mei 21, 2017 Sh milioni 5 zinadaiwa kupelekwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari, lakini kama ilivyokuwa nyuma hakuna risiti ya mtoa huduma.

Juni 5, 2017 Malima alilipwa Sh milioni 10 kupitia hundi Na. 157736 kama ‘salary advance’, lakini kiasi hicho hakikukatwa kwenye mshahara wake wa mwezi huo kama sera ya PRIDE inavyoagiza. Hati ya malipo ilisainiwa naye mwenyewe.

Juni 9, 2017 akachukua tena ‘salary advance’ ya Sh milioni 6 na hazikukatwa kwenye mshahara wake. Julai 18, 2017 zilichukuliwa Sh milioni 5 kwa ajili ya kuwalipa Essence International Ltd kwa kile kilichodaiwa kuwa ni gharama za mafunzo. Mkaguzi wa Ndani hakuonyeshwa risiti wala hati ya malipo kutoka kwa mtoa huduma.

Agosti 17, 2017 Malima alichukua dola 6,500 (Sh milioni 15) kwa hundi Na. 158148. Siku iliyofuata, alichukua dola 3,500 (Sh milioni 8.05) kama ‘advance salary’ yake lakini hakuna nyaraka za kuhalalisha malipo hayo.

Agosti 23, 2017 alichukua Sh milioni 8 kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa kutumia hundi Na. 158185 lakini baadaye ikabainika kuwa Sh milioni 3.005 aliziweka kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Bank M; na Sh milioni 1.985 akaziweka kwenye akaunti yenye jina la Abdallah Malima iliyoko katika benki hiyo hiyo.

Agosti 31, 2017 alijiidhinishia malipo ya Sh milioni 52 kupitia hundi yenye Na. 158193 na kwenda kuziweka zote kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima iliyoko katika Benki ya Stanbic.

Septemba 7, 2017 alichukua Sh milioni 10 ambazo ziliwekwa kwenye akaunti yake ya M-Pesa iliyosomeka kwa jina la Rashid Malima. Septemba 19, 2017 alichukua dola 2,000 ambazo hazina maelezo. Novemba 14, 2017 kiasi kingine cha Sh milioni 3.5 kiliingizwa kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Benki ya Stanbic.

Kwenye ukaguzi huo inadaiwa kuwa Malima alitumia kadi ya AMEX (American Express) inayomwezesha kuingia kwenye akaunti ya PRIDE moja kwa moja. Malipo ya kuwa na kadi hiyo kwa mwaka ni dola 2,500 (shilingi zaidi ya milioni 10). Kwa kuitumia AMEX aliweza kuondoa Sh milioni 275.582 kwa mchanganuo ufuatao:

Februari 3, 2017 alichukua Sh milioni 80.521 kutoka Bank M; Aprili 3, 2017 alichukua Sh milioni 52.744; Mei 3, 2017 alichukua Sh milioni 35.549 kutoka Tawi la Magomeni; Juni 2, 2017 alichukua Sh milioni 37.42; Julai 13 alichukua Sh milioni 22.5; Julai 14, 2017 alichukua Sh milioni 14.7; na Septemba 4, 2017 Sh milioni 32.146 zilitolewa kwa utaratibu huo.

Pia kiasi kingine cha Sh milioni 126 kinaonekana kutumika kulipa deni la mkopo binafsi wa Malima kati ya Januari -Novemba, mwaka jana lakini nyaraka za kuthibitisha malipo hayo hazikuweza kuonekana wakati wa ukaguzi wa ndani.

 

JAMHURI Toleo Na. 338

Kwenye Toleo Na. 338 la JAMHURI chini ya kichwa cha habari, ‘Pride inafilisika – *Mkurugenzi wake Mkuu akimbia -*Polisi watoa RB asakwe, akamatwe – *Vigogo wake 6 wasimamishwa kazi’, tuliripoti kuwa

Malima ameikimbia ofisi na polisi wametoa hati ya kukamatwa kwake ili ahojiwe TAKUKURU.

Malima aliripotiwa katika Kituo Kikuu jijini Arusha na kuanzia hapo akawa hapatikani kwenye simu yake ya mkononi.

 

JAMHURI Toleo Na. 340

Kwenye toleo hilo tuliripoti kuwa ‘Malima afukuzwa PRIDE’, nafasi yake imejazwa na Ruth Urassa.

Taarifa zisizotiliwa shaka zilionyesha kuwa Malima alikuwa amekimbia nje ya nchi akikwepa kujibu tuhuma za kuifilisi PRIDE.

Hatua hiyo ilichukuliwa na Bodi ya Wakurugenzi inayoongozwa na Profesa William Lyakurwa; ambaye naye uchunguzi umebaini kwamba muda mrefu anakuwa nje ya nchi kwa shughuli binafsi.

Ilibainika kuwa Malima alitorokea Marekani kwa kupitia mpakani Sirari mkoani Mara hadi Nairoibi, Kenya.

3156 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!