Askari Polisi wa Wilaya ya Kinondoni amefanya uporaji kwenye ofisi za kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam.

Oktoba 3, mwaka huu saa tatu usiku, askari aliyefahamika kwa jina moja tu la Shuka, akiwa na wenzake wawili walifika kituo cha mabasi Ubungo na kuwakamata wafanyakazi wa kampuni tatu za mabasi kisha kuwaweka chini ya ulinzi katika kituo kidogo cha polisi kilichopo ndani ya stendi.

Wakielezea mkasa huo, wafanyakazi hao wameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa Hamidu Mahmoud mwenye umri wa miaka 44, karani wa mabasi ya Modern Coast alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu ambaye aliomba kusaidiwa kukatiwa tiketi akiwa na mzigo wake.

Baada ya kuzungumza naye alimtaka kufika kwenye ofisi za mabasi hayo lakini mtu huyo alimwambia kuwa ameleta mzigo hivyo anaomba msaada wake, baada ya kwenda kama alivyoombwa na mteja huyo, aliwekwa chini ya ulinzi na watu watatu waliojitambulisha kuwa ni askari maalumu.

“Waliniambia kuwa ni askari wa kikosi maalumu wametoka makao makuu, wakaninyang’anya simu na kuniingiza kwenye gari walilokuwa wamekuja nalo ambalo ni aina ya Passo la rangi ya bluu. Niliwaambia wanipeleke Polisi post wakagoma, ndipo nikaanza kupiga kelele kuwa ninatekwa, wakaamua kunipeleka polisi, kwani watu walikuwa wameanza kujaa,” amesema Hamidu.

Hamidu ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa baada ya kuzingirwa na watu alipelekwa kituo kidogo cha polisi na kuingizwa sero, anamkumbuka askari wa zamu katika kituo kidogo cha Polisi kilichopo Ubungo stendi kwa jina moja la Chuki.

 “Watu hao waliondoka na kuniacha bila kusema jambo lolote, lakini baada ya muda mfupi niliona analetwa Hassan na kisha Mbisso hapo ndipo tukaambiwa kuwa tuna kesi ya wizi wa mtandaoni,” amesema Hamidu.

Hassan Msigiti, ambaye ni meneja wa mabasi ya Ratco, amesema alikuwa ofisini kwake anafunga hesabu wakaingia watu watatu huku mmoja wao akiwa amebeba begi mgongoni na kuondoka na wafanyakazi wawili wa kampuni yake ambao ni Musa na Kidubule.

Msigiti ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa baada ya dakika tano aliambiwa kuwa naye anahitajika kituo cha polisi, hivyo aliondoka nao bila kujua tatizo ni nini.

Anasema alipofika kituoni alipokewa na afande Chuki ambaye alimuuliza kuna nini mpaka analetwa hapo, Chuki akamjibu kuwa hao ni askari kutoka makao makuu wamefika Ubungo kwa kazi maalumu inayohusiana na wizi wa mtandaoni (cyber crime) hivyo wanakamata watuhumiwa.

“Afande Chuki aliwaambia askari wenzake waite gari ili lituchukue…niliwaomba nikafunge ofisi, maana iko wazi, wakati tunakwenda kufunga ofisi rafiki yangu Mbisso akaniita na kuniuliza: ‘Vipi’…nikamjibu: ‘Poa’. Askari mmoja akaniuliza: ‘Huyo ni nani?’ Nikamwambia, akasema twende tumfuate, tulipomfikia tu, akasema naye anahitajika polisi, wakatufunga pingu,” amesema Msigiti.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu tukio hilo, Mbisso Chibura, ambaye ni meneja wa mabasi ya City Boy, amesema alikuwa ofisini kwake akamuona rafiki yake anapita ameongozana na watu akamsalimia, ghafla akajikuta mikononi mwa polisi.

“Nilikuwa ofisini nimemaliza kufunga hesabu, wakaja watu kunikamata bila kuelezwa kosa langu, nikaonekana kuwa ni mkorofi, nikafungwa pingu, wakaniambia wao ni watu wasiojulikana.  Mmoja alinitolea bastora na pingu, niliogopa sana ikabidi nitii, kwani sijazoea mambo hayo. Nikachukuliwa na kupelekwa kituoni nikaunganishwa na wenzangu.

“Nilipofika huko nikauliza kosa langu, Chuki akaniambia kuwa ninatuhumiwa kwa wizi wa mtandaoni. Nilishangaa kwani sijui unafanywaje. Hapo nilinyang’anywa simu zangu kisha tukaondolewa pale na kuambiwa kuwa tunapelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.  Tulitoka hapo kwa kutumia magari mawili; Passo na gari la kukodi,” amesema Mbisso.

Amesema walipotoka Ubungo walipitia kituo cha mafuta kilichopo Shekilango kujaza mafuta, polisi walimwambia Msigiti atoe Sh 20,000 kwa ajili ya kulipia mafuta. Kisha waliondoka mpaka Magomeni Mwembechai ambako magari hayo yalisimama na kuanza kuwahoji upya huku wakiwabadilishia kesi na kuwaeleza kuwa ni majambazi.

“Kwenye gari walianza kuniambia kuwa mimi ni jambazi, niliwahi kupigwa risasi Tarime natakiwa kuwaeleza bunduki iko wapi, niliwashangaa kwani sijawahi kushika wala kugusa bunduki katika maisha yangu. Nikawaambia kuwa huo ni uongo na wala sijawahi kupigwa risasi,” amesema Mbisso.

Mbisso ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa wakiwa Magomeni Mwembechai, Msigiti alishushwa kwenye gari na kutakiwa kutoa pesa Sh 350,000 ili Musa na Kidubule waweze kuachiwa. Aliwapatia Sh 100,000 huku Musa na Kidubule wakitoa Sh 150,000.

Waliendelea kubaki eneo hilo kwa muda wa zaidi ya saa moja kwa madai ya kuwasubiri wenzao wanaoleta nyaraka za watuhumiwa. Walifika watu ambao walikwenda kuzungumza nao upande wa pili wa barabara kisha wakaondoka.

Wakiwa njiani kuelekea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, askari waliwataka watuhumiwa hao kutoa kiasi cha Sh milioni 3 ili waachiwe, lakini hawakutoa, ghafla wakabadilishiwa uelekeo na kuambiwa wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central).

“Tulipelekwa kituo cha mabasi ya stesheni badala ya Central, tulipofika hapo stesheni Hamidu alishushwa kwenye gari na kupigwa pingu kisha kupelekwa kituoni ambako walikataa kumpokea,” amesema.

Hamidu anasema alipofikishwa mapokezi, askari waliokuwa zamu waliuliza iwapo mtuhumiwa ana jalada, askari aliyempeleka akasema hana, akaulizwa iwapo ana RB, akasema hana, ila mtuhumiwa amepelekwa kituoni hapo kwa amri ya wakubwa, jambo ambalo hawakukubaliana nalo.

“Waligoma kumpokea maana hawana taarifa zinazojitosheleza, wakafukuzwa na kumtaka polisi aliyempeleka ampeleke kituo chake cha kazi si kumtelekeza hapo. Aliwapigia wenzake simu wakaja kutukuta Posta Mpya kwenye banda la chips,” amesema Mbisso.

Saa sita usiku askari hao waliwachukua tena na kuwaingiza kwenye jengo lililozungushiwa mabati (Embassy Hotel) na kuwanyang’anya pesa zote walizokuwa nazo kisha waliwarudisha kwenye gari kwa madai ya kuwapeleka Kituo cha Polisi cha Salender Bridge.

Mbisso anasema alinyang’anywa Sh 1,495,000, Hassan Sh 970,000 na Hamidu Sh 560,000.

“Tuliondoka Posta Mpya kuelekea Salender lakini hatukusimama, wakasema wanatupeleka Oysterbay Polisi lakini tukapitishwa, wakasema wanatupeleka Mabatini, napo tukapitishwa. Tulipofika Kwa Chesko Mzee wa Matunda, gari likasimama, ghafla likatokea gari aina ya Toyota Noah lililokuwa na askari aliyevaa sare akauliza: “Kulikoni?” Askari mmoja akashuka kutoka kwenye gari letu akaenda kuzungumza naye.

“Tukiwa tumebaki kwenye gari, Msigiti akasema tuondoke, maana tumezungushwa sana, akashuka akaanza kuondoka, nami ndipo nikashuka, tukamuacha Hamidu ambaye alishuka akiwa wa mwisho. Tuliondoka bila kuulizwa, tukaamua kwenda Kituo cha Polisi cha Urafiki kuripoti suala letu, wakatuambia turudi asubuhi kwani wasingeweza kufungua faili wakati Ubungo kuna inspekta,” amesema Mbisso.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba Oktoba 4, mwaka huu waliwasiliana na mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ubungo ambaye aliwataka wasubiri ashughulikie suala lao.

Baadaye vijana hao wanadai kupelekwa na inspekta huyo moja kwa moja kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Murilo Jumanne Murilo,  ambaye alimuagiza kamanda wa upelelezi wa wilaya kufuatilia suala hilo.

Baada ya kufanyiwa mahojiano walikabidhiwa kwa askari wa upelelezi na kupewa RB namba DSM/KIN/CID/PE/248/2018 huku mpelelezi wa kesi hiyo akitajwa kwa jina moja la Paroko.

Gazeti la JAMHURI limefika Kituo cha Polisi Oysterbay ili kupata ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo na kufanikiwa kuzungumza na mmoja wa wapelelezi ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake, na kubainisha kwamba upelelezi wa jambo hilo umekamilika na suala hilo liko kwa ‘wakubwa’.

“Hili suala ni kweli lipo na lilitokea, huyu askari anayetuhumiwa yupo na inasikitisha kuona askari anakuwa mhalifu kwa kushirikiana na wahalifu wengine…upelelezi umekamilika, kilichobaki ni hatua za kisheria kuchukuliwa, ukikutana na wakubwa watakupa ufafanuzi wa kina,” amesema askari huyo.

Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo, kuzungumzia suala hili hazikufanikiwa.

By Jamhuri