Ripoti ya CAG, nafasi ya uwajibikaji kwa Serikali

Wiki iliyopita Rais Dk. John Magufuli akiwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma, alipokea Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2019 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama kawaida ripoti hiyo iliyoandaliwa na wataalamu wa ukaguzi wa hesabu ndani ya Ofisi ya CAG imesheheni taarifa muhimu na nyeti, huku pia ikiwa na mapendekezo ya nini kinapaswa kufanyika ili kudhibiti matumizi ya fedha za umma ndani ya ofisa za serikali, ikifichua pia makosa yaliyofanywa ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi.

Rais Dk. Magufuli alimuahidi CAG kuwa taarifa hiyo kama alivyoipokea, atawakabidhi wasaidizi wake akiwamo Waziri Mkuu waifanyie kazi katika maeneo yanayowahusu na kwamba pia atamkabidhi ripoti hiyo Spika wa Bunge ‘kama ilivyo’! Akimaanisha kuwa haitaongezwa wala kupunguzwa hata nukta moja, ili wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi waijadili na kutoa mapendekezo yao.

Aghalabu, kwa miaka mingi mapendekezo ya wabunge katika ripoti ya CAG huwa ni kukazia yale mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu wa Ofisi ya CAG, lakini wabunge hupendekeza kuchukuliwa kwa hatua kali zaidi kwa wlaiokutwa na makosa na kutaka serikali ionyeshe wazi uwajibikaji mbele ya umma.

Tunafahamu umakini uliomo ndani ya serikali ya sasa dhidi ya wabadhirifu na wote wanaochezea fedha za umma hasa katika kipindi hiki ambapo taifa linahitaji kila shilingi moja inayopatikana itumike ipasavyo na kusaidia kujenga uchumi utakaoliwezesha kuingia miongoni  mwa mataifa yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kasi ya maendeleo ya taifa iliyokuwapo kwa miaka minne iliyopita ambayo kwa sasa ipo katika kipindi kigumu kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaojulikana kama corona, haipaswi kuchezewa na kusimamishwa na wazembe wachache waliomo ndani ya ofisi za umma wakisababisha kupotea kwa fedha za umma kwa makusudi kwa faida yao.

Ndiyo maana tunaamini kuwa serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Ofisi ya CAG ndani ya taarifa hiyo pamoja na yale yatakayotolewa na Bunge siku chache zijazo kwa kuwawajibisha wote waliohusika bila kuwaonea haya, hivyo kuweka mazingira ya matumizi bora ya fedha za umma kwa miaka ijayo.