Ugonjwa wa COVID-19 ulioanzia nchini China mapema mwaka jana na kusambaa duniani kote, unaendelea kugharimu maisha ya walimwengu wengi.

Tanzania, kama yalivyo mataifa mengine ya Afrika na dunia, imeshaonja machungu ya uwepo wa maradhi haya hatari. 

Mwaka jana shule na vyuo vilifungwa, lakini hata baadhi ya sehemu za uzalishaji wafanyakazi walipunguzwa, ukiwa ni mkakati wa kukabiliana na maradhi haya kiafya na kiuchumi.

Tunapongeza juhudi zilizochukuliwa na serikali kwa wakati huo, pamoja na wadau wengine, hasa vyombo vya habari kwa namna walivyosimama imara kuwaelimisha wananchi namna ya kujinga na ugonjwa huo.

Idadi kubwa ya wananchi hasa maeneo ya mijini iliheshimu maelekezo ya serikali na ya wataalamu wa afya. Wananchi walianza kunawa mikono kwa sababu, walitumia vitakasa mikono, walivaa barakoa, na wakaacha utamaduni wa kusogeleana na hata kupeana mikono. Hizi zilikuwa hatua nzuri za kuikabili COVID-19.

Lakini baadaye haya yote yaliachwa pengine kutokana na kuaminishwa kuwa ugonjwa ulishatoweka. Bado viongozi wakuu waliendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia kanuni za usafi ili kukwepa maambukizi mapya.

Kwa bahati mbaya hapa katikati ni kama tulijisahau, matokeo yake japo vyombo husika havijatangaza, ukweli ni kuwa vifo vingi vinavyotokea sasa vinatushawishi tuhisi kuwa huenda ugonjwa huu umerejea.

Tunawashukuru viongozi wa madhehebu mbalimbali waliojitokeza hadharani kuwataka waamini na wananchi kuchukua hadhari dhidi ya maradhi haya. 

Tunawapongeza viongozi wa serikali walioamua kuuvaa ujasiri na kukiri kuwa hali ya mambo si nzuri, na kwa maana hiyo hadhari sharti ichukuliwe.

Kwa mara nyingine tunawaomba viongozi wenye mamlaka wautangazie umma ili taratibu za kujikinga ugonjwa huu zichukuliwe. Mathalani, vyombo vya usafiri kama daladala ni vizuri abiria wakavaa barakoa na wakaketi kwenye viti.

Kila mahali, kuanzia magengeni hadi ngazi ya kaya kuwe na maji ya kunawa na sabuni. Suala la kunawa lisiwe la hiari maana licha ya kusaidia kutokomeza COVID-19, imebainika kuwa unawaji umepunguza maradhi mengi ya kuhara.

Tuyafanye haya wakati huo huo tukiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na hili janga. 

Tuombe pia serikali itenge fedha za kutosha ili watafiti wetu wafanye kazi zao. Hatuna sababu ya kusubiri tuletewa dawa au chanjo kutoka ughaibuni. 

Maana mojawapo ya uhuru ni kujitegemea kwa mambo kama haya ya chanjo na dawa. Tuchukue hadhari. COVID-19 bado ipo.

By Jamhuri