Wagawa viwanja barabarani

Ugawaji wa nyumba za Shirika la Nyumba (NCH)

 

663. Kwa muda mrefu kumekuwepo na malalamiko miongoni mwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa utaratibu unaotumika katika kugawa nyumba za Shirika. Baadhi ya waombaji wa nyumba hizo wamejaza fomu za maombi miaka mingi iliyopia na kila wakifuatilia maombi hayo wanajibiwa kwama hakuna nyumba zilizo tupu. Hata hivyo, kuna baadhi ya watu ambao wameomba nyumba na kupata katika muda mfupi tu. Kukosekana kwa uwazi katika utaratibu huu kunasababisha mambo yafuatayo:

 

(i)                Nyumba za Shirika la Nyumba zimekuwa zinagawiwa wapangaji kwa upendeleo. Watu wanaotafuta nyumba hizo wamekuwa wanatoa fedha kwa watumishi wa Shirika ili waweze kupata upendeleo wakati wa kugawa nyumba hizo.

 

(ii)              Baadhi ya viongozi wamekuwa wanavuruga utaratibu wa kugawa nyumba za Shirika la Nyumba. Viongozi hao wamekuwa wanaandika vikaratasi (memo) kwa Mkuu wa Shirika la Nyumba kumshinikiza atoe nyumba kwa ndugu na marafiki zao au kwa yeyote yule baada ya kupokea chochote.

 

664. MAPENDEKEZO

 

(i)                Maamuzi yote yaliyofanywa kuhusiana na kurudisha nyumba kinyume cha sheria na yabatilishwe.

 

(ii)             Uuzaji wa nyumba za Shirika ufuate kanuni na taratibu zilizowekwa. Wapangaji halali wa nyumba zinazotakiwa kuuzwa wapewe kipaumbele kununua.

(iii)           Kwa wale wote waliopewa nyumba ambazo hazikuwa zao, nyumba hizo ziuzwe kwa ridhaa ya NHC kwa kufuata taratibu zilizopo.

 

KIAMBATISHO NA. 1

 

Kamati za kugawa viwanja zina wajumbe wafuatao:

 

(a)  Wilaya

 

1.     Afisa Tawala (W) – Mwenyekiti

2.     Afisa Ardhi – Katibu

3.     Afisa Mpima

4.     Mhandisi wa Maji

5.     Mhandisi wa Ujenzi

6.     Afisa Afya

7.     Mkurugenzi Mtendaji

8.     Madiwani 5

 

(b) Mkoa

 

1.     Mkuu wa Mkoa – Mwenyekiti

2.     Afisa Maendeleo Ardhi – Katibu

3.     Afisa Mipango Miji

4.     Afisa Mpima (M)

5.     Mhandisi Mji (M)

6.     Mhandisi wa Maji (M)

7.     Mhandisi wa Ujenzi (M)

8.     Madiwani 5

9.     Afisa Kilimo (M)

10.                        Afisa Mipango Miji

 

(c ) Wizarani

 

1.     Kamishna wa Ardhi – Mwenyekiti

2.     Kamishna wa Serikali za Mitaa – Katibu

3.     Mkurugenzi Mipango Miji

4.     Mkurugenzi Upimaji na Ramani

5.     Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira

6.     Kamishna wa Kilimo

7.     Mkurugenzi wa Utalii

8.     Mkurugenzi wa “Heavy Industries”

9.     Mkurugenzi Mkuu wa Jiji

10.                        Madiwani 6 wa Halmashauri ya Jiji.

 

Majukumu ya Kamati za kugawa viwanja

 

(a)  Wilaya

(i)                Kugawa viwanja kwa ajili ya makazi (high density) na huduma;

(ii)             Kugawa viwanja kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo;

(iii)           Maeneo ya mashamba yasiyozidi ekari mia moja (100) isipokuwa kwa Kamati za Dar es Salaam ambazo zina uwezo wa kutoa mashamba yasiyozidi ekari tatu (3);

 

(b)  Mkoa

(i)                Viwanja kwa ajili ya viwanda vya ukubwa wa kati;

(ii)             Maeneo ya biashara na makazi mijini;

(iii)           Viwanja kwa ajili ya mashirika na jumuia za kidini;

(iv)           Viwanja vya maeneo ya ufukwe wa pwani;

(v)             Viwanja vya serikali

(vi)           Maeneo ya mashamba kuanzia ekari 100 na yasiyozidi ekari 500.

 

(c ) Wizarani

Kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa isipokuwa Dodoma.

(i)                Kugawa viwanja maeneo ya katikati ya Jiji;

(ii)             Maeneo ya huduma na makazi;

(iii)           Maeneo ya ukubwa wa kati (medium density) na maeneo makubwa (low density);

(iv)           Kugawa maeneo ya ufuko wa bahari;

(v)             Viwanja vya matumizi ya serikali jijini;

(vi)           Viwanja vya matumizi ya mashirika ya umma jijini;

(vii)        Maeneo ya viwanda vikubwa;

(viii)      Viwanja kwa ajili ya hoteli za kitalii;

(ix)           Viwanja kwa ajili ya ofisi za Ubalozi au mashirika ya kimataifa;

(x)             Mashamba kuanzia ekari 500 na kuendelea;

(xi)           Maeneo ya vijiji.

 

KIAMBATISHO 2

VIWANJA AMBAVYO VIMETOLEWA MARA MBILI MANISPAA YA TABORA NA AFISA ARDHI WA MKOA NDUGU MWAIBALE BINAFSI

 

PLOT

NAMBA YA TOLEO

726 55MD Ipuli

1.     TB/L/55291 – 28/3/94 – J.J. Nyanda

2.     TB/L/6351 – 18/7/94 – Grace For a Yongolo

56  S MLD Ipuli

2.TB/L/6845 – 5/4/95 – Harson Mgombele

1.TB/L5571/1 – 28/2/94 – William M. Chimaguli

137 E Isevya

2.TB/L/6768/1 – 12/5/95 – Marco

 James

1.TB/L6442 – 25/8/94 – Mwanahamisi Hassan

557 RR HD Chemchem

2.TB/L6727/1 – 16/2/95 – Saad D. Idd

1.TB/L6645/2 – 14/11/95 – Fikirini Masudi

210 PP Ng’ambo

1.TB/L5251/1 – 1/11/93 – Kassim Yohaya Masud

2.TB/L4522/3 -19/9/94 – Selemani Abam Lusunga

565 RR Ng’ambo

2.TB/L6719/1 – 16/2/95 – Kudra Malingumu

1.TB/L3200/1 – 31/3/92 – Enock Lumala

64 PP Ng’ambo

2.TB/L3321/3 – 20/9/94 – Amisa Haji Kazili

1.TB/L2901/1 – 20/11/90 – Ismail Mohamed

425 PP Ng’ambo

2.TB/L6819/16/3/95 – Mwange Seleman

1.TB/L2820 – 2/2/94 – Habib Salum Mkalanga

631 RR Ng’ambo

1.TB/L6193 – 3/6/94 – Verick John Malika

2.TB/L6288/1 – 9/6/94 – Richard Saimon Nyangisa

 

Kiwanja – Plot 7 Kitalu ‘F’ – tangu – 29/1/86 – Ref. No.LD/TTC/56139 Afisa Ardhi Manispaa.

 

Plot No. 486, 487 PP Ng’ambo Plot No. 484, PP Ng’ambo

Ndugu Mwaibale Afisa Ardhi (M) na Ndugu Ketto Ardhi Manispaa wamevigawa mara tatu.

 

KIAMBATISHO NA. 3

Viwanja Na. 4 na 6 Oysterbay Shopping Centre vinamilikiwa na Msasani  Peninsular Hotels Ltd. S.L.P. 20200 Dar es Salaam kwa muda wa miaka 99 kuanzia mwaka 1978 kwa hati Na. 186037/125. Katika viwanja hivi ndipo ilipojengwa Hoteli ya Karibu. Viwanja Na. 14 na 15 Oysterbay Shopping Centre vinamilikiwa na Msasani Flats Ltd. S.L.P 20200 Dar es Salaam kwa muda wa miaka 33 kuanzia mwaka 1991.

Kiwanja Na. 1821, Oysterbay Shopping Centre kinamilikiwa na M/s Msasani Flats Ltd S.L.P. 20200 Dar es Salaam kwa hati Na. 35341 kwa miaka 99 kuanzia mwaka 1989. Msasani Shopping Centre Ltd na Msasani Flats Ltd, ni kampuni zinazomilikiwa na Bw. L. W. Ladwa.

Chini ya Mpango kabambe wa Jiji la Dar es Salaam, eneo ambalo sasa lina viwanja Na. 14 na 15 lilitengwa kama eneo la wazi kwa manufaa ya Umma (Open space) mnamo mwaka 1978 eneo hili lilipimwa viwanja Na. 14 na 15 kwa makosa na kumilikishwa kwa Bw. Lionel Frank Mlang’a Marealle wa S.L.P. 2042 Dar es Salaam. Mnamo tarehe 1/7/1978  Ofisi ya Ardhi Wilaya ya Kinondoni [na] Bw. Marealle alipewa hati Na. 186037 ya kumiliki viwanja hivyo mwaka 1980. Vile vile katika miaka ya 80, kilibuniwa kiwanja Na. 1821 mbele ya viwanja Na. 14 na 15.

Ubunifu wa viwanja Na. 14 na 15 ulifanyika kinyume  na taratibu bila idhini ya Mkurugenzi wa Mipango Miji. Tarehe  26/11/1981 Mkurugenzi wa Mipango Miji alimwandikia barua Mkurugenzi wa Jiji kumtaka asimamishe ujenzi uliokuwa unafanywa na Bw. Marealle katika viwanja hivyo kwa sababu ni eneo la wazi.

Mkurugenzi wa Mipango Miji alibadilisha matumizi ya eneo hilo kutoka eneo la wazi na kuagiza liendelezwe kama bustani, bwawa la kuogelea na egesho la magari kwa ajili ya wageni wa hoteli na maduka yaliyo karibu. Mkurugenzi wa Mipango Miji aliwasilisha michoro mipya ya eneo hilo Halmashauri ya Jiji na kushauri eneo hilo liendelezwe na Msasani Peninsular Hotels kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji.

Msasani Flats Ltd, walikwishapewa viwanja hivi kwa makosa mwaka 1989. Utoaji huu ulikuwa batili ingawa ulifuata maelekezo ya mwaka 1987 yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Mipango Miji. Halmashauri ya Jiji ilimpa Msasani Flats eneo hilo kwa masharti kwamba angetunza bwawa la kuogelea ambalo litatumika kwa manufaa ya Umma na sehemu ya egesho la magari kubakia chini ya Halmashauri na kuwekewa mita kwa ajili ya kuongeza pato la Jiji.

Tarehe 22/2/1991 milki ya Bw. Marealle ilifutwa kwa manufaa ya umma. Ilipofika tarehe 15/8/1991 milki mpya ilitolewa kwa Msasani Flats na ipo hai hadi leo. Bw. Marealle kuona kwamba amenyang’anywa viwanja hivyo na kupewa mtu mwingine kwa matumizi ambayo sio ya manufaa ya umma, alifungua kesi Na. 22/1994 Mahakama Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msasani Flats Ltd, kudai fidia ya mamilioni ya fedha alizokuwa amewekeza katika viwanja hivyo kabla ya milki yake kufutwa. Kesi hiyo bado haijamalizika.

Uamuzi wa Wizara ya ardhi kugawa tena eneo hili kwa mteja mwingine hasa baada ya kubaini kwamba yalikwishafanyika makosa hapo awali  ni kinyume kabisa na taratibu za Ugawaji wa Ardhi. Kitendo kama hiki kinatia wasiwasi kuhusu uaminifu wa watumishi wa Wizara ya Ardhi na hasa ikizingatiwa kwamba aliyepewa kiwanja hiki ni yule yule anayehusika na kiwanja cha Indian Ocean.

 

KIAMBATISHO NA. 4

Bw. Ameir Mohamed Hassan alikuwa na nyumba huko Michenzani Zanzibar ambayo ilivunjwa ili kutoa nafasi ya ujenzi wa Majumba ya ghorofa. Bwana Mohamed alipewa flat moja katika moja ya ghorofa hizo lakini kutokana na ugonjwa alikuwa hawezi kupanda ngazi za ghorofa hiyo. Bwana huyu aliomba apewe flat ya chini bila ya mafanikio, na mwishowe serikali ilimpatia nyumba iliyokuwa inatumika kama Afisa ya Majenzi katika eneo la Mlandege. Nyumba hiyo ilikuwa imezungukwa na kiwanja kikubwa kuelekea barabara kuu iendayo Hoteli ya Bwawani. Baada ya muda mrefu kipita, Kamisheni ya Ardhi na Mazingira iliandaa ramani mpya ya matumizi ya eneo hilo na kupima viwanja 12. Kulingana na ramani mpya nyumba ya Bw. Ameir iko ndani ya kiwanja na. 28.

Bw. Abdulsatar aliomba apewe viwanja vitatu yaani Na. 28, 29 na 34. Kamisheni ya Ardhi ilimpa kiwanja Na. 34 ambacho kilikuwa tupu na kumshauri afanye mazungumzo na wenye nyumba katika viwanja Na. 28 na 29 na ikiwa watakubali anunue nyumba zao basi atapewa viwanja hivyo. Bw. Abdulsatar aliweza kununua nyumba katika kiwanja Na. 29 lakini Bw. Ameir alikataa kumuuzia nyumba yake ndani ya kiwanja Na. 28. Baada ya Bw. Abdulsatar kumfanyia vitisho na jeuri nyingi Bw. Ameir ili amuuzie nyumba yake kushindwa, alikwenda Kamisheni ya Ardhi ambapo aliandaliwa mchoro mahsusi kukidhi matakwa yake. Mfanyabiashara huyu tajiri alimwambia Bw. Ameir kwamba kwa sababu amekataa kumuuzia nyumba yake basi atakuja ‘kuhamishwa na mbwa wenzake’ akimaanisha polisi weusi kama yeye. Bw. Ameir alikwenda kumwona aliyekuwa Waziri wa Ardhi na kumweleza jinsi mfanyabiashara huyo anavyonyanyaswa na akaahidiwa kwamba tatizo lake litapatiwa ufumbuzi.

Wakati wa sherehe za 31 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika huko Pemba ambapo viongozi wengi walikwenda kwenye sherehe hiyo, Bw. Abdulsatar alileta malori ya kokoto na kuanza kazi ya kuweka msingi. Bw. Abdulsatar alianza kuvunja banda la mbao lililokuwa mbele ya nyumba ya Bw. Ameir na alipotaka kuzuia uvunjaji huo alikuja kukamatwa na polisi ambao walikuwa wameletwa na mfanyabiashara huyo. Polisi walimtaka Bw. Ameir apande kwenye gari la Bw. Abdulsatar kuelekea Kituo cha Polisi lakini alikataa. Baadaye alikwenda kituoni mwenyewe na kuwekwa rumande kwa muda wa siku tatu. Alipoachiwa alikuta msingi wa nyumba ya Bw. Abdulsatar umekamilika.

Mafundi wanaojenga nyumba hiyo wamekuwa wanaangusha kila aina ya uchafu na matofali kwa makusudi juu ya nyumba ya Bw. Ameir ili mradi tu aondoke sehemu hiyo. Juhudi za Bw. Ameir za kutafuta haki yake zimekuwa zinapigwa tarehe na tayari jumba la ghorofa tatu limekamilika katika sehemu hiyo na kuibana kabisa nyumba ya Bw. Ameir. Bw. Ameir ni mwanajeshi mstaafu na kitendo cha viongozi kumkumbatia mfanyabiashara hiyo na kutochukua hatua za kumsaidia kimemfanya asiwe na imani na uongozi, jambo ambalo anaungwa mkono na wanyonge wenzake.

KIAMBATISHO 5

Bwana A. Kasuga aliyekuwa mfanyakazi wa Benki ya Taifa  ya Biashara alikuwa na shamba huko Kunduchi Mtongani. Shamba hilo lilipimwa na kutoa viwanja viwili Na. 91 na Na. 93. Mdogo wake alipewa kiwanja Na. 91 kwa sababu tayari alikuwa amejenga nyumba ya kisasa na fidia ingelikuwa kubwa sana. Bw. Kasuga aliahidiwa kupewa kiwanja Na. 93 lakini badala yake kilitolewa kwa Bw. F. Rutaihwa, Bw. Kasuga alikwenda Ofisi ya Jiji kulalamika kuhusu ukiukwaji wa utaratibu na akaahidiwa kwamba suala hilo lingefanyiwa uchunguzi wa kina.

Kwa muda wa mwaka mmoja Bw.  Kasuga alifuatilia suala hilo ofisi za Jiji bila ya mafanikio. Alikwenda Wizara ya Ardhi kumwona Waziri Mhe. A. Ntagazwa ambaye pia alishindwa kumtatulia tatizo lake hadi alipoondolewa katika wadhifa huo. Mwishoni mwa mwaka 1991 Bw. Rutaihwa akishirikiana na wazee fulani wa Jiji aliuza kiwanja hicho kwa Mhindi aitwaye Himat Babla mwenye kampuni ya Asher Automobiles.

Wazee  hao wa jiji waliweza kumjazia hati ya kurejesha (surrender) kiwanja na kumjazia Offer ya kiwanja hicho kwa jina la Kampuni ya Asher Automobiles katika siku moja ya tarehe 20 Februari, 1991. Bw. Kasuga alikwenda kumwona Waziri wa Ardhi, Mhe.M. Komanya na kumweleza mkasa wote na aliahidi kushughulikia tatizo hilo lakini akamtaka subira.

Baada ya kumwona Waziri kila wiki kwa muda wa miezi zaidi ya minne, subira yake ilifikia kikomo pale alipoelezwa na waziri kwamba suala lake ni nyeti na linahusika na wakubwa. Bw. Kasuga aliamua kufungua kesi Mahakama ya Kisutu ili aweze kupata haki yake. (Kesi Na. 171/92).

Kitika kiwanja Na. 93, Bw. Kasuga alikuwa amepanda migomba, mazao mengine pamoja na nyumba ndogo na hivyo kumfanya Bw. Babla kushindwa kuendeleza kiwanja hicho. Tarehe 14 Mei, 1993, Bw. Kasuga akiwa kwenye kiwanja Na. 93 alikamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka ya kuvamia kiwanja cha mtu na kulima migomba na mazao pamoja na kujenga nyumba.

Alipelekwa Central Police siku hiyo ya Ijumaa akaandika taarifa yake na mwishowe kuwekwa rumande hadi siku ya Jumatatu kwa amri ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa wakati huo Bw. Mahenge ambaye alitumiwa na Babla. Bw. Kasuga aliamriwa na polisi kubomoa nyumba iliyokuwa katika kiwanja hicho kabla kesi hiyo haijapelekwa mahakamani tarehe 22 Mei, 1993.

Baada ya kutoka rumande, Bw. Kasuga alikwenda kumwona Kamishna wa Polisi na kumweleza mkasa wote na jinsi kesi yake Na. 171/92 ilivyokuwa inaahirishwa na Mwendesha Mashtaka katika Mahakama ya Kisutu. Alipewa ‘memo’ ambayo alipeleka kwa RPC Bw. Tryphon Maji na baada ya kusoma statement aliyokuwa ameandika aliamuru kesi ya Babla dhidi yake isubiri uamuzi wa kesi Na. 171/92.

Tarehe 28 Juni, 1993 Bw. Kasuga alikwenda Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesiyake na ghafla alikamatwa na polisi na kupelekwa kituo cha polisi cha Wazo Hill ambapo alifunguliwa mashtaka ya wizi wa matofali 500 ambayo ilidaiwa kwamba Babla aliyaweka katika kiwanja Na.93 kwa ajili ya kujenga kibanda cha mlinzi.

Baada ya kuandika statement na kueleza jinsi aliyvopata matofali hayo alitakiwa kufika kituoni hapo kila wiki ili kujua hatma ya tuhuma iliyokuwa inamkabili. Wakati huo huo kesi Na. 171/92 ilikuwa inatajwa tu bila ya kusikilizwa ilifutwa tarehe15/10/1993 kwa kisingizio kwamba mshtaki na mtuhumiwa walikuwa hawafiki mahakamani.

Ukweli ni kwamba hizi ni njama zilizotumika ili kumwezesha Babla aweze kuendeleza kesi aliyofungua dhidi ya Bw. Kasuga ya ‘Criminal Treaspassing.’ Bw. Kasuga alipokwenda kituo cha Polisi Wazo aliwekwa rumande na kesho  yake alipelekwa mahakamani Kisutu na kufunguliwa kesi Na. 1356/93 ya wizi wa matofali 500. Kesi hiyo iliendeshwa kwa muda wa miezi 11 na Bw. Kasuga akashinda.

Bw. Kasuga aliandika barua kwa Rais kueleza jinsi chombo cha polisi na mahakama vinavyotumiwa na Babla kumnyima haki yake na mbinu zinazotumika ili kumkatisha tamaa ya kutafuta haki hiyo. Ikulu iliandika Barua Kumbu. Na. SHC/L.50/1 kwa Waziri wa Ardhi Mhe. E. Lowassa kumwagiza kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mgogoro wa kiwanja hicho.

Baada ya uchunguzi ilibainika kwamba Babla alipata kiwanja hicho kwa hila na miliki ya Asher Automobiles ilifutwa kwa barua Kumb. Na. LD/149378/29/DW ya tarehe 1 Agosti, 1994.

Himat Babla kwa kumrubuni Mthamini wa Serikali na wafanyakazi wa NBC aliweza kuidanganya NBC kwamba alikuwa amejenga nyumba ya ghorofa mbili ya thamani ya Shs 35,000,000 katika kiwanja Na.93 na hivyo kujipatia mkopo baada ya kuweka hati miliki ya kiwanja hicho kama dhamana.

Kwa hiyo Bw. Babla anatakiwa kurejesha hati hiyo Wizara ya Ardhi, lakini anashindwa kwa sababu hati hiyo imeshikiliwa na Benki kwa jengo ambalo halipo. Bwana Kasuga amekuwa anatafuta haki yake kwa kipindi cha miaka 6 na hajafanikiwa mpaka sasa! 

 KIAMBATISHO 6

Barabara kati ya Msasani Old Mosque na Army Camp katika eneo la Msasani ina eneo la kuegesha magari na sehemu ya upanuzi siku za baadaye. Katika sehemu zote mbili za barabara viwanja vilitolewa zamani na vimeendelezwa. Hivi karibuni sehemu ya barabara hiyo kuingia baharini imegawiwa mtu kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya kuishi na umma hauna tena njia ya kuingia baharini.

Jiji liliamua kupima viwanja katika barabara hiyo bila ya kuzingatia kanuni na taratibu za kubadilisha matumizi ya maeneo ndani ya master plan. Naibu Waziri wa Ardhi Mh. E Mwambulukutu alitembelea eneo la barabara hiyo na kumshauri Waziri wa Ardhi Mh. E. Lowasa kwamba lipimwe viwanja. Eneo hili lilipimwa na kupatikana viwanja tisa ambavyo Mh. Naibu Waziri wa Ardhi aliagiza vigawanywe kwa watu wafuatao:-

Na. 1843 – Martha Mollel. Na. 1844 – M. Y. C. Lumbanga (Mfange M. Mtunguja?). Na. 1845 – Mariam Ashrafu, Na. 1846 – Lucia Andrea Salema, na Na. 1847- Regina Amuri. Aidha aliagiza kwamba barua ya ‘Offfer’ kwa Nd. Mollel apewe mwenyewe na nyingine zote apewe Nd. Said Nguba ambaye ataziwasilisha kwa wenyewe.

Uongozi wa Msasani Slipway Ltd. Uliandika barua kumb. NC/Cu/IGWILIZI ya tarehe 19/10/1995 kwa Mkurugenzi wa Jiji na nakala kwa Kamishna wa Ardhi kulalamika kuhusu uamuzi wa kupima na kugawa viwanja katika ‘ROAD  RESERVE’ ya barabara hiyo.

Tarehe 17/11/1995 Wizara ya Ardhi iliandika barua yenye Kumb. Na. LD/126370/26/EM ya kufuta miliki ya viwanja hivyo. Aidha katika eneo la Kijitonyama nako kuna viwanja 33 vilivyopimwa na kugawiwa watu katika eneo ambalo lilikuwa limetengwa kwa ajili ya barabara.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anazungumziaje adha aliyopata Mzanzibari kutoka kwa mfanyabiashara? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu uleule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

1928 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!