Wiki iliyopita rubani wa ndege ya Shirika la Precision inayoruka kutoka Nairobi kuja Dar es Salaam, Rizwan Remtura amelifanyia taifa letu kazi ya kupigiwa mfano. Rubani huyo amefanya tukio ambalo hakuna aliyepata kuliwaza na ni tukio ambalo likitazamwa kwa mapana yake linaweza kuwa chimbuko la faida kubwa kwa taifa letu.

Sitanii, mwaka 2004 niliposafiri kwenda nchini Misri nilipata fursa ya kupanda dege aina ya Airbus na rubani akatutangazia kuwa angefanya uendeshaji wa kitalii. Nilichoshuhudia ni simulizi ya aina yake. Rubani huyo alikuwa analaza ndege upande na kutupa fursa ya kuliona Jangwa la Sahara, na alilenga mto Nile akawa anaufuata ulivyokatiza jangwani.
Tulipofika Aswan tulirushwa juu ya mnara unaozalisha umeme wa Aswan High Dam. Urushaji huu ulikuwa wa faida ya pekee kwetu tuliokuwa kwenye ndege hii. Nilichokishuhudia kwa kuona Aswan High Dam na Low yake, kilinivuitia sijapata kusahau. Nafahamu tupo Watanzania wengi tungetamani siku moja kupanda mlima Kilimanjaro.

Wapo wazee ambao wana ukwasi wa kutosha kutoka hapa nchini na katika nchi za Kigeni ambao wangetamani kufika au kuona kilelel cha Mlima Kilimanjaro, lakini hawajafanikiwa na kwa umri wao kusema wapande mlima ule na kukiona kilele itakuwa sawa na kutaka kuondosha uhai wao kabla ya wakati wao.
Alichokifanya Remtura, kimeamsha hisia zangu. Kwanza nikasema Remtura apewe tuzo na Bodi ya Utalii Tanzania. Pili, kuanzia sasa uwekwe utaratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania kuwa na safari maalum ya utalii wa ndege. Utalii wa aina hii utaiwezesha nchi yetu kupata fursa ya aina yake. Fursa haitakuwa nyingine, kwani kwa wale wasio na uwezo wa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa mguu wanaweza kuupanda kwa ndege.

Mwonekano wa Mlima Kilimanjaro, barafu inayoonekana kwenye picha iliyochukuliwa kwa simu ya mkononi, unahamasisha. Alichofanya Remtura kilifanywa kwa njia ya utalii, unaweza kukuta ndege ya kuruka kuzunguka Mlima Kilimanjaro inagombewa. Nasema sasa uanzishwe utalii wa kurusha ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuzunguka mlima na kutua tena.

Ni bahati mbaya kwa nchi zetu hizi huwa hatutambuli kazi zilizotukuka kama hii aliyofanya Remtura. Badala ya kuona alichofanya kuwa ni fursa ya kuliingizia taifa letu mapato kwa njia ya utalii, unaweza kukuta anapewa barua ya onyo. Anaweza kuambiwa alikuwa anahatarisha maisha ya wasafiri. Sitashangaa kwa nchi yetu likitokea hilo.
Sitanii, unaweza kukuta akitokea Mzungu akafanya kitu hicho hicho, hata vitabu vinaandikwa. Hakuna ubwege unaonikera kama huo. Leo tunasoma historia eti Johannes Rebmann, ndiye Mzungu aliyegundua Mlima Kilimanjaro. Tunaaminishwa kuwa Wamachame na Wachaga waliopo kwenye kingo za Mlima Kilimanjaro ilikuwa hawauoni hadi alipofika Mzungu.

Nasema alichofanya Remtura kinapaswa kutambuliwa. Kitambuliwe na ikiwezekana apewe Ubalozi wa Heshima ya kutangaza Mlima Kilimanjaro. Nasema hivi kwa kuwa nafahamu maeneo mengi ambayo baadhi ya watu wanafanya mambo makubwa kama kubainisha wizi wa uliokuwa unafanyika Bandari. Si ajabu waliobaini kilichotokea na wakasaidia kuziba mianya, huenda leo hawatambuliki.

Twende mbali kuwa mtu kama Rais John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kufumua sekta ya madini, basi tujitahidi tumtambue kazi zao. Ikiwezekana Rais Magufuli apewe tuzo kwa kazi hii ya kufumua mikataba ya madini. Ni bahati mbaya haya tutakuwa hatuyasemi wakati watu hawa tukiwa nao. Wakati umefika sasa tubadilike. Tutambule kjazi za watu.
Sitanii, naomba kuhitimisha makala hii kwa kusisitiza kuwa Tanzania ianzishe utalii wa ndege kuzunguka Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ambayo ni vivutio vya aina yake. Tukitambuliwa kuwa tunafanya kazi ya aina hiyo, nchi yetu itakuwa kwenye nafasi ya kuvutia watalii wa kutosha. Mungu ibariki Tanzania, Mungu isaidie nchi hii ipate vyanzo vipya vya mapato.

 

Na Deodatus Balile
Dar es Salaam
Simu: 0784 404 827

Email: balile@jamhurimedia.co.tz

951 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!