Wiki iliyopita makala hii ilichapishwa. Hata hivyo, kimakosa kuna aya mbili zilikatika na kuifanya makala hii kupoteza maana ya kwa nini imeandikwa. Kutokana na wasomaji wengi kunipigia simu kuuliza ilihusu nini, naomba kuirudia makala hii. Pia naomba radhi kwa usumbufu uliotokana na kukatika kwa aya hizo. Endelea na nakala iliyosahihishwa sasa…

Wiki iliyopita (wiki mbili sasa) rubani wa ndege ya Shirika la Precision inayoruka kutoka Nairobi kuja Dar es Salaam, Rizwan Remtura amelifanyia taifa letu kazi ya kupigiwa mfano. Rubani huyo amefanya tukio ambalo hakuna aliyepata kuliwaza na ni tukio ambalo likitazamwa kwa mapana linaweza kuwa chimbuko la faida kubwa kwa taifa letu.
Remtura wakati anaendesha ndege ya Precision katika safari zake za kawaida kutoka Nairobi kuja Dar es Salaam, aliichepusha ndege kidogo. Aliamua kukata kona na kuuzunguka Mlima Kilimanjaro nyuzi 360. Kwa lugha ya kawaida aliuzunguka mlima wote na kurejea kwenye njia ya ndege ya kawaida.
Kwa njia ya ndege ya Nairobi – Dar es Salaam, ndege zote zinaruka kupita Mashariki ya Mlima Kilimanjaro. Siku hiyo kilele cha Mlima Kilimanjaro kilikuwa kinaonekana kwa uwazi wa hali ya juu na wote waliokuwa kwenye ndege walipata burudani ya aina yake.

Upande wa Magharibi, ndege hazipiti kwani katika umbali usio mrefu kutoka kilele cha Mlima Kilimanjaro, kuna kilele cha Mlima Meru. Hata hivyo, kuna nafasi isiyohatarisha ndege inayopita katikati ya vilele hivi viwili, na hili limethibitika baada ya Remtura kuipitisha ndege hiyo.
Sitanii, mwaka 2004 niliposafiri kwenda nchini Misri nilipata fursa ya kupanda dege aina ya Airbus na rubani akatutangazia kuwa angefanya uendeshaji wa kitalii. Nilichoshuhudia ni simulizi ya aina yake. Rubani huyo alikuwa analaza ndege upande na kutupa fursa ya kuliona Jangwa la Sahara, na alilenga mto Nile akawa anaufuata ulivyokatiza jangwani.
Tulipofika Aswan tulirushwa juu ya mnara unaozalisha umeme wa Aswan High Dam. Urushaji huu ulikuwa wa faida ya pekee kwetu tuliokuwa kwenye ndege hii. Nilichokishuhudia kwa kuona Aswan High Dam na Low yake, kilinivutia sijapata kusahau. Nafahamu tupo Watanzania wengi tungetamani siku moja kupanda Mlima Kilimanjaro.
Wapo wazee ambao wana ukwasi wa kutosha kutoka hapa nchini na katika nchi za Kigeni ambao wangetamani kufika au kuona kilele cha Mlima Kilimanjaro, lakini hawajafanikiwa na kwa umri wao kusema wapande mlima ule na kukiona kilele itakuwa sawa na kutaka kuondosha uhai wao kabla ya wakati wao.

Sitanii, alichokifanya Remtura, kimeamsha hisia zangu. Kwanza nikasema Remtura apewe tuzo na Bodi ya Utalii Tanzania. Pili, kuanzia sasa uwekwe utaratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania kuwa na safari maalum ya utalii wa ndege. Utalii wa aina hii utaiwezesha nchi yetu kupata fursa ya aina yake. Fursa haitakuwa nyingine, kwani kwa wale wasio na uwezo wa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa miguu wanaweza kuupanda kwa ndege.
Mwonekano wa Mlima Kilimanjaro, barafu inayoonekana kwenye picha iliyochukuliwa kwa simu ya mkononi, unahamasisha. Alichofanya Remtura kikifanywa kwa njia ya utalii, unaweza kukuta ndege ya kuruka kuzunguka Mlima Kilimanjaro inagombewa. Nasema sasa uanzishwe utalii wa kurusha ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuzunguka mlima na kutua tena.
Ni bahati mbaya kuwa nchi zetu hizi huwa hatutambui kazi zilizotukuka kama hii aliyofanya Remtura. Badala ya kuona alichofanya kuwa ni fursa ya kuliingizia taifa letu mapato kwa njia ya utalii, unaweza kukuta anapewa barua ya onyo. Anaweza kuambiwa alikuwa anahatarisha maisha ya wasafiri. Sitashangaa kwa nchi yetu likitokea hilo.

Sitanii, unaweza kukuta akitokea Mzungu akafanya kitu hicho hicho, hata vitabu vinaandikwa. Hakuna ubwege unaonikera kama huo. Leo tunasoma historia eti Johannes Rebmann, ndiye Mzungu aliyegundua Mlima Kilimanjaro. Tunaaminishwa kuwa Wamachame na Wachaga waliopo kwenye kingo za Mlima Kilimanjaro ilikuwa hawauoni hadi alipofika Mzungu!
Nasema alichofanya Remtura kinapaswa kutambuliwa. Kitambuliwe na ikiwezekana apewe Ubalozi wa Heshima ya kutangaza Mlima Kilimanjaro. Nasema hivi kwa kuwa nafahamu maeneo mengi ambayo baadhi ya watu (si vyombo vya habari) wanafanya mambo makubwa kama kubainisha wizi wa uliokuwa unafanyika Bandari, lakini hadi leo wanatambulika kwa mchango wao. Si ajabu waliobaini kilichotokea na wakasaidia kuziba mianya, huenda leo hawatambuliki.

Twende mbali kuwa mtu kama Rais John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kufumua sekta ya madini, basi tujitahidi tumtambue kazi yake. Ikiwezekana Rais Magufuli apewe tuzo kwa kazi hii ya kufumua mikataba ya madini. Ni bahati mbaya haya tutakuwa hatuyasemi wakati watu hawa tukiwa nao. Wakati umefika sasa tubadilike. Tutambue kazi za watu.
Sitanii, naomba kuhitimisha makala hii kwa kusisitiza kuwa Tanzania ianzishe utalii wa ndege kuzunguka Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ambayo ni vivutio vya aina yake. Tukitambuliwa kuwa tunafanya kazi ya aina hiyo, nchi yetu itakuwa kwenye nafasi ya kuvutia watalii wa kutosha. Mungu ibariki Tanzania, Mungu isaidie nchi hii ipate vyanzo vipya vya mapato.

 

Na Deodatus Balile
Dar es Salaam
Simu: 0784 404 827

Email: [email protected]

By Jamhuri