Naandika makala hii nikiwa hapa jijini Tanga. Nashiriki mkatano wa mwaka wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wanahabari. Nimepata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Msitu wa Amani. Msitu huu ulioko Muheza ni wa aina yake. Msitu uko kwenye bonde na kingo za milima.

Msitu umehifadhiwa na unayo miti iliyokomaa usipime. Miti hii inakua, inazeena na kuanguka au kuangushwa na upepo, lakini hakuna anayeruhusiwa kuukata ubao au kuchanja kuni ndani ya msitu huu. Tumeelezwa kuwa msitu huu ni wa hifadhi. Hata mti ambayo unaweza kukatwa hadi mbao 1,000 ukianguka, unakatwa vipande na kusogezwa kando uoze. Basi.

Ardhi ni yoevu. Tumeingia katikati ya msitu, kila ukikanyaga ardhi unaridhika kuwa imeshiba maji. Tumeambiwa msitu huo ni chanzo cha mito mingi, ukiwamo mto Pangani. Kwenye kilele cha milima ya Usambara, inapandwa chai. Kuna nyumba za kutosha za watumishi wanaofanya kazi kwenye mashamba ya chai.

Sitanii, mashamba ya chai yalivyopangiliwa, barabara zinavyokatiza kupanda milima kutoka chini hadi kileleni, hakika ni utalii wa aina yake. Ukifika kilele cha milima ya Usambara, upande wa pili unakuwa ukiiona milima ya Lushoto. Bondeni unakuwa ukiuona mji wa Korogowe na Mombo. Mhifadhi Mama Kijazi ametujuza kuwa Serikali ina mpango wa kuweka miavuli ya kurusha wageni kutoka milima ya Usambara kwenda bondeni.

Ukiacha hiyo miti ya asili wahifadhi wamepanda miti aina ya mitiki. Miti hii inauzwa wastani wa Sh 900,000 kwa mita ya ujazo moja. Kutokana na thamani yake huwezi kuuza hii miti hadi upate kibali cha Serikali. Hakika kwa mtu anayelima miti hii anafanya uwekezaji wa dhati.

Sitanii, wakati akili yangu ikiwa imebarizi, baada ya kuona miti hiyo, maua na vipepeo, nikafanikiwa kuondoa moshi wa daladala kichwani, ghafla nikasikia dude linaamka huko Chama cha Wananchi (CUF). Mwanzo nilifikiri ni mchezo. Nikasikia kuwa CUF imepeleka barua kwa Spika kuomba wabunge wake wanane wafukuzwe bungeni.

Jioni hiyo nikahojiwa na Shirika la Utangazaji la Sauti ya Amerika (VOA), nikawambia kwa mawazo yangu sidhani kama Spika anaweza kukubaliana na wazo hili la CUF. Nilisema hivyo kwa kutilia maanani barua ya Spika kwamba alikuwa anaitafakari barua ya CUF iliyoandikwa na “Kaimu Katibu Mkuu”, Magdalena Sakaya.

Kwa uelewa wangu mdogo wa kisheria, nilifahamu na najua hata Spika anafahamu kuwa CUF kuna mgogoro wa kimamlaka, ambapo upande mmoja unapigania haki za kisiasa na mwingine unapigania masilahi ya tumbo. Kwamba pande hizi mbili zimepeleka shauri lao mbele ya Mahakama ipitie Katiba CUF na Sheria ya Vyama vya Siasa, na kwa kutumia mamlaka inayopata kutoka Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama itamke nani mwenye haki.

Kabla hilo halijatokea, nikasikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikitangaza kuwa imepokea taarifa ya Spika kuwa CUF imewafukuza wabunge wake wanane uanachama. Hili likanipa shida kidogo. Nikasema ebo! Spika amesahau kuwa kesi iko mahakamani au yupo kazini? Pia nikakumbuka kuwa Spika alikuwa nje ya nchi!

Sitanii, wakati nikiendelea kushangaa nikapata mshtuko wa mwaka. Prof. Lipumba akakaririwa na gazeti moja akikiri kubadili majina ya wabunge watarajiwa waliokuwa katika orodha ya kupata ubunge kule Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume nayo ikateua majina mapya aliyowasilisha Lipumba. Hili linakiogofya.

CCM tumeshuhudia muda wote na NEC hii hii imekuwa ikitueleza kama sisi Wakristo tunavyosali sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni, bila kuikosea wala kuibadili kizazi hadi kizazi kuwa orodha ya wabunge inayokuwa Tume ndiyo hiyo hiyo. Kunapotokea mabadiliko kwa wabunge wa Viti Maalum, anatolewa aliyeko bungeni na anayefuatia kwenye orodha ya chama iliyoko Tume ndiye anateuliwa kuwa mbunge.

Sasa gazeti limemkariri Lipumba akisema, “wamebadili” orodha ya wabunge iliyopelekwa na Maalim Seifu. Nikajiuliza. Wameibadili kwa kuitisha uchaguzi au kwa kufanya uteuzi? Ninaye rafiki yangu, mara zote yeye huwa ni kinyume katika kauli.

Nakumbuka siku moja ilikuwa namwambia, Elimu Haina Mwisho. Yeye akaniambia ni kweli ndugu yangu, ila na mimi nisikilize: “Ujinga Hauna Mwisho.” Wakati naandika makala hii, nimelazimika kuangalia Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Oxford toleo la Mwaka 2010, Ukurasa wa 428 kuhusu neno ujinga.

Kamusi hiyo inasema, Ujinga ni “hali ya kutojua kitu fulani; ubozi, ujahili, upumbavu.” Sina uhakika kama mtu aliyesoma na kutunukiwa heshima ya kuwa Profesa anaweza bado akawa mjinga. Nawaza kwa sauti tu, ila nashawishika kukubaliana na Kamusi ya Kiswahili Sanifu.

Kwamba ni hali ya kutojua kitu fulani; ubozi, ujahili… hili la mwisho nadhani Kamusi ina uchochezi. Profesa Lipumba hawezi kuwa mmoja wa wale aliowasema Rais (mstaafu) Bejamin Mkapa wakati wa uzinduzi wa Kampeni za CCM pale Jangwani mwaka 2015!

Nimekuwa mwanafunzi wa diplomasia, na nimehitimu diplomasia. Namfahamu Mama Shahari aliyeingizwa kwenye orodha ya kutimuliwa na Sakaya. Najaribu kuwaza kwa sauti, kwamba je, tumesahau msemo wa wahenga wa kuweka akiba katika kila tutendalo?

Najiuliza leo Mhe. Sakaya, najua anaweza kujitutumua tu akisoma makala hii akasema yeye alishinda kwa uwezo wake, lakini kama si upepo na wimbi la mabadiliko hivi kweli Sakaya alikuwa na uwezo wa kumshinda Prof. Kapuya? Kweli? Hii inafikirisha. Hivi leo tuna ujasiri wa kutukana wakunga wakati uzazi ungalipo?

Ndugu yangu Sakaya, ogopa ukaribisho wa panya kwenye harusi ya paka. Soma alama za nyakati. Karibuni nimeona picha kupitia WhatsApp simba akimnyonyesha mtoto wa chui. Ni katika muktadha huo paka anaweza kukumbatiana na panya.

Sisi Wakristo wakati wa Kwaresima, neno hili kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Oxford niliyoinukuu hapo juu, ukurasa wa 204 linamaanisha “siku arubaini za mfungo wa Wakristo kabla ya sikuukuu ya Pasaka.” Ndani ya kipindi hiki huwa tunafunga.

Nafahamu hata dini nyingine huwa wanafunga, na kwa hiyo hatuli mchana, sawa na dini nyingine zisivyokula mchana. Katika kipindi kama hicho, panya akikutana na paka mchana akiwa kwenye kipindi cha Kwaresima, kwa maana kwamba amefunga mchana, kukumbatiwa si ajabu.

Lakini pia yapo mazingira kuwa inawezekana paka anaweza kuwa ameshiba, hivyo akashirikiana na panya kucheza “pool” au na mwisho kabisa, paka anaweza kuwa mgonjwa, hivyo akila chochote anatapika, basi katika mazingira hayo akikutana na panya kumkumbatia sitashangaa!

Sitanii, Prof. Lipumba na Mhe. Sakaya, wala mimi sitathubutu kutamka yanayotajwa kuwa ushirika wenu jiwe kuu la pembeni limeegeshwa kwenye ukabila. Kwamba mnatoka mkoa mmoja, mnazungumza Kinyamwezi pamoja, mnakwenda “kusalimia na kupokea maelekezo ya kutoboa mtumbwi” pamoja… ila naazima maneno ya Mhe. Jakaya Kikwete, “Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.”

 Mimi ni mpenzi wa timu imara ya Simba. Kwa kweli ikiwa Yanga inacheza na timu ya nje ya Tanzania, hiyo ndiyo fursa pekee huwa naishangilia Yanga. Nalifanya hili kwa misingi ya uzalendo na utaifa.

Kombe wakilipata Yanga la nje ya nchi, anayesikia Yanga, atauliza hiyo ni timu kutoka nchi ipi, watasema Tanzania, na mimi ni Mtanzania, kwa mantiki hiyo adui yeyote nje ya mipaka ya Tanzania ni adui wa Watanzania. Mashindano yoyote ya nje ya nchi ni mashindano ya Tanzania, bila kujali anatuwakilisha Yanga, Simba au Lipuli.

Nakiri kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Lakini nashawishika kusema ukweli. Siwezi kuvumilia kuona mwanachama aliyeko CCM, akiendelea kuwa ndani ya CCM, lakini anafanya siasa za Chadema, CUF, TLP, UDP… Na kinyume chake ni sahihi. Huwezi kusajiliwa mtibwa, ukachezea African Sports. Ukitaka hilo, nenda huko huko, vinginevyo unafanya usaliti kama mwanadamu.

Sitanii, ukurasa huu, nadhani unaanza kuwa mfupi, sasa nihitimishe. Nasema, nimeshtuka kweli kusikia tangazo la Lipumba kufukuza wabunge wanane wa chama chake. Nimeshtuka zaidi kusikia Spika wa Bunge “amesahau” kuwa CUF wana kesi mahakamani ya mgogoro wa uongozi.

Lakini moyo wangu umepasuka kusikia Lipumba et al, wameweza kubadili majina ya wabunge waliokuwa kwenye orodha ya Tume ya Uchaguzi mwaka 2015. Baadhi ya mambo ni aibu ya kimya kimya. Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako. NEC najiuliza sheria imebadilika lini? Spika ameanza kusahau lini?

Si hilo tu, ila najiuliza bado tena. Umetoka wapi ugumu wa kulazimisha makocha wetu kuhamisha milingoti ya magoli kuhakikisha hata mwenye makengeza akipiga mpira kwenye kibendera cha kona ukutane na tundu la goli kwenye kona ya uwanja?

Sitanii, mwisho nasikitika. Nikiri mimi ni mtetezi wa utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya vya habari, uhuru wa kujieleza, haki za kisiasa na kidemokrasia. Siamini katika kumpiga mtu kibao eti kwa sababu mfadhili au mtu aliyeko nyuma yangu ameniambia piga.

Niliamini, na hasa nilipokaa na Prof. Lipumba baada ya Januari 21, mwaka 2001 kutokana na CUF kutoa siku 90 habari ambayo niliiandika mimi, baadaye Lipumba aliposema tusamehe, ila tusisahau, kuwa alikuwa mwanamageuzi wa kweli. Sitaki kuamini kuwa sasa anashiriki kuchoma kiota au nyumba aliyoko ndani.

Prof. Lipumba piga moyo konde. Tazama mikanda yako yote ya mwaka 2001 hadi 2005, kisha jiulize na upime kama bado upo kwenye reli au unaendeshea mabehewa kichakani. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

 

Na Deodatus Balile, Tanga

By Jamhuri