Bila mama yake angekuwa wapi? (2)

Baada ya kuhitimu elimu yake ya sekondari mwaka 2006, mwaka uliofuata – 2007, Diamond akajikita rasmi katika shughuli za muziki ili kujaribu kutimiza ndoto zake.

Hata hivyo, hakupata mserereko kama ambavyo alitarajia, kwani alipitia mambo magumu sana katika kipindi hicho.

Ilifikia muda akaanza kutafuta vibarua sehemu mbalimbali ili aweze kupata riziki na kuepuka hali ya kushinda nyumbani.

Diamond alipitia kazi ya kuuza mitumba, kuuza mafuta katika vituo vya mafuta, kupiga picha, kupigisha simu katika vibanda na kazi za viwandani.

Alilazimika wakati mwingine kuingia kwenye makundi ya kucheza kamari za mitaani ili aweze kupata pesa za kuingia studio kurekodi nyimbo zake.

Juhudi zake hizo hazikuweza kuzaa matunda, lakini pia hali hiyo haikumkatisha tamaa. Akiwa na ari ya kufikia malengo yake, ilimlazimu kuuza pete ya dhahabu ambayo alipewa na mama yake mzazi.

Baada ya tukio hilo, akamdanganya mama yake kuwa pete hiyo imepotea!

Alifanikiwa kupata fedha zilizomwezesha kuingia studio kurekodi wimbo wa kwanza alioupa jina la ‘Toka Mwanzo.’

Ukosefu wa mazoea ya kurekodi, ulisababisha kushindwa kutengeneza wimbo mzuri, hivyo haukukubalika sana miongoni mwa wapenzi wa muziki.

Lakini kupitia wimbo huo watu wengi wakabaini kipaji ambacho Diamond anacho. Tofauti na wageni wengi katika ‘gemu’ walivyokuwa wakifanya, Diamond alionekana kama mzoefu katika kazi hiyo.

Baadhi yao wakaamini kuwa akipata nafasi ya kurekodi mara kadhaa, angeweza kufanya vitu vikubwa zaidi.

Wimbo ule ulimfanya aweze kukutana na Chizo Mapene ambaye alijitolea kumsimamia. Wakaanza kurekodi albamu. Wakiwa katikati ya kurekodi albamu hiyo, aliyekuwa akimsaidia kwa bahati mbaya alipata matatizo ya kifedha, hivyo hakuweza tena kumsaidia.

Diamond ilimbidi aanze upya kuzunguka katika studio mbalimbali kuomba kusainiwa kwenye ‘record label’.

Lakini kote alikopita hakuweza kufanikiwa. Wote walimwambia bado hajafikia kiwango cha kuimba, wakaacha kumsikiliza kabisa.

Kilikuwa ni kipindi kigumu sana, maana hata aliyekuwa mpenzi wake alimkimbia baada ya kuchoshwa na ndoto hewa za Diamond ambazo alikuwa akiziota kila siku kuwa ipo siku atafanikiwa kimuziki.

Ndoto za Diamond zilikuwa kwamba angekuwa mwanamuziki mkubwa, yeye na mpenzi wake huyo wangeishi maisha mazuri.

Kitendo cha mpenzi wake huyo kilimchanganya na kumuumiza sana Diamond, hususan kwa kauli aliyomuambia – “Sikiliza Diamond, mimi kwa sasa siwezi kuwa na mwanaume ambaye hana masilahi kwangu.” Akajiona kama mtu mwenye mikosi.

Mwaka 2009 Diamond alikutana na Msafiri Peter, maarufu kama Papaa Misifa, ambaye alikubali kumsaidia kimuziki na kurekodi wimbo wa kwanza uliokwenda kwa jina la ‘Nenda Kamwambie.’

Wimbo huo aliuimba kwa uchungu kuhusu mpenzi wake, Sarah Sadiki, aliyemuacha akielezea ni kiasi gani aliumia kwa yeye kumuacha.

“Mungu si Athumani.” Usemi huu ulijionyesha baada ya nyota ya Diamond kuanza kuchomoza taratibu kupitia kibao hiki.

‘Nenda Kamwambie’ ulikuwa ukichukua chati siku hadi siku na kufanya maisha ya Diamond kuanza kubadilika hadi kuweza kununua gari aina ya Toyota Celica.

Februari 14, 2010 Diamond aliachia albamu yake ya kwanza iliyokuwa na nyimbo 10 za ‘Kamwambie’, ‘Mbagala’, ‘Nitarejea’, ‘Nalia na Mengi’, “Binadamu’, ‘Nakupa’, ‘Usisahau’, ‘Uko Tayari’, ‘Wakunesanesa’, ‘Toka Mwanzo na ‘Jisachi’.

Ilipotimu Aprili 4, 2010, aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo tatu za Tanzania Kili Music Awards.

Tuzo hizo ni za Msanii Bora Chipukizi, Wimbo Bora wa Mwaka – Kamwambie, na Wimbo Bora wa R&B. Tuzo hizo zilimfanya achaguliwe kuwa Balozi wa Malaria nchini Tanzania.

Baada ya kuachia wimbo wake wa pili unaoitwa ‘Mbagala’, Diamond akapata nafasi ya kuwa kati ya wasanii waliokuwa wakitumbuiza katika timu ya kampeni ya urais wakati huo Dk. Jakaya Kikwete akiwania tena nafasi hiyo kwa mara ya pili.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa magazeti na mitandao mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0767331200, 0736331200.

1461 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons