Bila mama yake angekuwa wapi? (1)

Licha ya nongwa na maneno ya kumchafua kwenye mitandao ya kijamii, Diamond Platnumz, anaendelea kutesa katika gemu la muziki wa kizazi kipya nchini na sehemu nyingine duniani.

Hivi karibuni msanii huyo alitunukiwa tuzo ya kuitangaza lugha ya Kiswahili kupitia muziki iliyotolewa na taasisi ijulikanayo – Swahili Vision International Association (SVIA).

Kabla ya hapo, Diamond Platnumz alishinda tuzo kwa kipengele cha ‘The Best Collaboration Award’ iliyotolewa na AEAUSA nchini Marekani Oktoba 20, mwaka huu.

Diamond amekuwa akipokea mialiko lukuki kwenda kutumbuiza katika nchi za Bara la Ulaya na Asia. Anafanikiwa kupata mialiko hii kwa sababu anakubaliwa na watu wanaoupenda muziki wake katika maeneo hayo yote.

Hivi karibuni alimshirikisha mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fally Ipupa, katika wimbo ‘Inama’, ambao umeibuka kuwa miongoni mwa nyimbo ambazo zinatamba hivi sasa katika vituo vya redio humu nchini.

Hili linamfanya Diamond aanze pia kulikamata soko la muziki nchini DRC.

Ukichukulia umri wake wa miaka 30 tu, Diamond bado anaonekana kuwa na uwezo na muda wa kufanya mambo makubwa zaidi katika muziki.

Alipozaliwa Oktoba 2, 1989 katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, alipewa majina ya Nasibu Abdul Juma.

Kwa bahati mbaya, hakupata malezi ya baba na mama yake, kwa kuwa wazazi wake walitengana akiwa na umri mdogo.

Baba yake alimuacha bila msaada wowote, ikabidi yeye na mama yake mzazi wahamie Tandale Magharibi kuishi pamoja na nyanya yake (mzaa mama), hapo ndipo yakawa makazi yao.

Historia yake ni ya kusikitisha kama alivyoelezea kwenye wimbo wa ‘Binadamu Wabaya’.

Mwaka 1995 alianza kupata elimu ya awali katika Shule ya Chakula Bora iliyopo Tandale Uzuri. Baada ya hapo akajiunga na elimu ya msingi mwaka 1996 katika Shule ya Tandale Magharibi.

Ilipofika mwaka 2000 akiwa darasa la tano, Diamond alionekana kuanza kupenda sana muziki, hivyo alianza kukopi na kukariri baadhi ya nyimbo za wasanii waliokuwa ‘wakihit’ ndani na nje ya nchi kwa kipindi hicho.

Nasibu akawa anaziimba nyimbo hizo sehemu mbalimbali.

Kwa kumuunga mkono, mama yake mara nyingi akawa anamnunulia kaseti za albamu za wasanii mbalimbali waliokuwa ‘wakihit’ kipindi hicho. Alidiriki hata kumuandikia baadhi ya nyimbo za wasanii hao ili mwanawe aweze kuzishika na kuimba kirahisi.

Mama huyo wakati mwingine alikuwa akimpeleka katika matamasha mbalimbali ya kuonyesha vipaji ili Diamond apate nafasi ya kuimba.

Baadhi ya ndugu wa familia yao waliona kama mama yake anampotosha na kumharibu mtoto huyo badala ya kumhimiza kimasomo.

Maisha yao yalikuwa magumu sana, kwa kuwa mama yake Diamond hakuwa hana njia ya kumuingizia kipato, ilibidi atumie kiasi kidogo anachokipata kutoka kwenye kodi ya vyumba viwili alivyopewa na mama yake, yaani nyanya yake Diamond.

Aidha, alikuwa akifanya biashara zake ndogondogo kwa mikopo ili aweze kumsomesha na kumlea mwanawe Diamond.

Hali ilivyozidi ‘kubana’, walilazimika wote kuhamia katika chumba cha nyanya huyo, wakapangisha vyumba vile viwili alivyopewa Mama Diamond.

Baada ya kuhitimu shule ya msingi mwaka 2002, Diamond akataka kuanza masomo ya sekondari mwaka 2003.

Mama yake alimshauri aachane na mambo ya muziki kabisa, badala yake ajikite katika masomo ili apate elimu itakayomsaidia hata katika muziki wake hapo baadaye.

Mama huyo akamwambia kwamba haiwezekani kushika vitu viwili kwa pamoja muda huo.

Diamond akaanza masomo ya sekondari huku akiendelea kufanya muziki kisirisiri bila mama yake kumbaini.  Ilipofikia mwaka 2004 taratibu akaanza kujifunza kuandika nyimbo zake mwenyewe.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa magazeti na mitandao mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0767331200, 0736331200 na 0713331200.

2778 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!