NA MWANDISHI WETU

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amesema kwamba amemwelekeza Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuunda tume mbili za uchunguzi kuhusu uagizwaji na uingizwaji wa magari ya Jeshi la Polisi nchini.

Amesema ameagiza kuundwa kwa tume ya kuchunguza mkataba huo ambayo itakuwa na wataalamu wa sheria na mikataba, ambao wataangalia suala zima la mkataba ikiwa ni pamoja na mchakato mzima wa mkataba huo.

Pia, tume nyingine itawahusisha wataalamu na masuala ya ufundi wa magari (mafundi waliobobea), ambayo itachunguza iwapo magari hayo yamekuja yakiwa yanakidhi viwango na kama kuna upungufu ni yapi.

Ninachotaka kazi ifanyike vizuri, sijali kama tume hizo zitakuwa na idadi ya watu wangapi, ila nahitaji ripoti hiyo mapema iwezekanavyo,” amesema Masauni.

Amesema kwamba kwa sasa Jeshi la Polisi lina uhaba wa usafiri na wa polisi wanachelewa kupata gari za matumizi, hivyo ripoti hiyo anaihitaji mapema ingawa hakusema itafanya uchunguzi kwa muda gani.

Alipoulizwa kwanini hakutoa muda wa tume hiyo kukamilisha uchunguzi, amesema kwamba uchunguzi huo unafanywa na wataalamu na unafanywa kitaalamu, hivyo hataki kufanya siasa katika mambo ya kitaalamu.

Wataalamu wana vitu vingi vya kuangalia, sasa wakisema wanaweza kutumia wiki moja mi nikasema nipeni siku tatu. Wakiniandikia ripoti ambayo haijawa ‘very comprehensive’ itakuwa haina tija. Tutakaa tutasema turudie. Mimi naamini nimetoa maelekezo ifanyike haraka,” amesema Masauni.

Kuhusu magari ambayo yameonekana kuwa tayari yametumika, amesema anasubiri ripoti ya uchunguzi ili aweze kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuona iwapo Serikali inakubaliana na mkataba huo au la.

Masauni amesema kwamba Serikali haiwezi kuvumilia utovu wa nidhamu wa aina yoyote, hivyo anasubiri ripoti hiyo ili aweze kuchukua hatua kutokana na kile alichokiona.

Yapo ambayo niliyaona na ndiyo maana nikataka kuundwa kwa tume, yakishabainishwa na mengine kutoka kwenye tume nitachukua hatua. Kwa sasa naisubiria hiyo ripoti na ninatamani niipate hata kesho ili niweze kushughulika nayo,” amesema Masauni.

JAMHURI limewasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Motorrama (T) LTD, ambayo ni Wakala wa Magari aina ya Ashok Leyland kutoka nchini India, Jitesh Ladwa, ili kupata ufafanuzi kuhusiana na magari hayo ambaye amekataa kuzungumzia.

Jitesh aliahidi kukutana na JAMHURI kwa mazungumzo, lakini siku aliyosema alipokumbushwa ahadi hiyo alitaka kufahamu sababu za kukutana kupitia ujumbe wa maneno. Na kusema kwamba mambo hayo ameyasoma kupitia vyombo vya habari hajui lolote.

Amesema anayeweza kuzungumzia suala hilo ni ubalozi wa India.

I read in news, contract is between Indian govt and Tanzanian govt. U should contact Indian High Commissioner. He can help u.” amesema Jitesh.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, amesema hawezi kuzungumzia hilo kwa sasa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Masauni mwanzoni mwa mwaka huu alimwagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuunda kamati  itakayoshirikisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali kupitia upya mikataba ya uagizwaji wa magari ya Polisi, huku akikitaka chombo hicho kufanyia ukaguzi wa magari 53 yaliyopelekwa katika Chuo cha Polisi Kurasini baada ya kutolewa bandarini Dar es Salaam kufuatia agizo la Rais John Magufuli.

Mhandisi Masauni ametoa maagizo hayo Jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara bandarini kuangalia iwapo maagizo ya Rais Magufuli yametekelezwa baada ya kutaka magari hayo yaliyoagizwa yaanze kutumika.

Masauni alisema kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likikabiliwa na tatizo la uhaba wa magari lakini ameshangazwa na utaratibu wa uagizwaji wa magari ya aina moja ambayo ni malori, jambo linalotia shaka  mikataba ya uagizwaji wa magari hayo.

Amesema kwamba licha ya agizo la kuondoa magari bandarini kutekelezwa, bado baadhi ya magari yanaonekana kuwa ni mabovu mno huku yakidaiwa kununuliwa yakiwa mapya.

Baada ya kukagua unaona kabisa mengine ni mabovu na kunaleta shaka, kwani kwa mujibu wa mkataba magari yanayopaswa kuagizwa ni lazima yawe mapya. Hivyo, ninaomba uchunguzi huo uangalie na ubora wa magari hayo tujue iwapo ni mapya au la na kamati hiyo itakuwa huru,” alisema Masauni.

Jumla ya magari 119 yaliagizwa kwa awamu ya pili ambayo tayari yameshawasili katika Bandari ya Dar es Salaam na yameagizwa kusambazwa haraka katika maeneo husika huku yakisubiri maagizo ya Rais.

Oktoba 2015, Serikali ya Tanzania ilisaini mkataba wa ununuzi wa magari kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini na Kampuni ya Motorrama (T) LTD ambayo ni Wakala wa Magari aina ya Ashok Leyland kutoka nchini India. 

Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Job Masima, pamoja na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo ya Utengenezaji wa magari, Bhimasena Rau, ukishuhudiwa na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada mkataba huo kusainiwa, aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja, aliishukuru Serikali kwa msaada huo ambao utasaidia kutatua tatizo la uhaba wa magari katika Jeshi la Magereza.

“Utekelezaji wa mpango huu katika Jeshi la Magereza utakuwa na manufaa makubwa kwani utapunguza tatizo la uhaba wa magari kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na utawala, pamoja na utekelezaji wa jukumu la kuwasafirisha mahabusu kwenda mahakamani na kurudi magerezani,” alisema Minja.

Lengo kubwa la ununuzi wa magari hayo ulilenga kuboresha huduma za usafiri, pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa nchini.

4045 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!