Home Kitaifa TUNAHITAJI AMANI KWENYE KAMPENI

TUNAHITAJI AMANI KWENYE KAMPENI

by Jamhuri

NA MICHAEL SARUNGI

Katika chaguzi ndogo za udiwani zilizofanyika mwaka jana, kuliripotiwa uwepo wa vurugu kiasi cha kusababisha baadhi ya vyama vya siasa kususia chaguzi zilizofuata katika majimbo ya Songea Mjini na Singida Kaskazini.

Taarifa za uwepo wa vurugu katika chaguzi hizo hazikuwa nzuri kwa kila mpenda demokrasia nchini, na kuanza kuashiria mgogoro wa kisiasa huku lawama nyingi zikielekezwa kwa vyombo vya ulinzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Hili ni tatizo ambalo likiachwa linaweza kuja kuwa na madhara makubwa ndani ya Taifa. Kwa kulifahamu hilo, ni jukumu la kila mamlaka husika kuhakikisha inatenda haki ili kuliepusha Taifa na lolote baya linaloweza kutokea.

Leo vyama vyetu vinapoendelea na kampeni za uchaguzi katika majimbo ya Siha na Kinondoni hatutarajii kushuhudia yale tuliyoyashuhudia katika chaguzi za marudio za udiwani zilizofanyika mwaka jana na kusababisha malalamiko mengi.

Katika miaka ya hivi karibuni nchini, hali ya ukuaji wa demokrasia ya vyama vya upinzani imeanza kutia moyo japokuwa kuna malalamiko kutoka kwa viongozi wa vyama hivyo ya kutotendewa haki na mamlaka husika.

Kwa mantiki hiyo, kuna haja ya mamlaka husika kuelewa kuwa ili kutimiza matakwa ya demokrasia, busara inatakiwa zaidi badala ya kutumia mabavu kuhalalisha mifumo ya utawala katika kipindi hiki cha kuelekea chaguzi hizi ndogo.

Lakini kwa upande mwingine, Jeshi letu la Polisi linapaswa kujiepusha na matumizi ya nguvu kubwa kupita kiasi kukabiliana na hamasa ya wapenzi wa vyama vya upinzani wakati wa mikutano yao na hata wakati wa kutangazwa kwa matokeo.

Ni wazi kuwa endapo Jeshi la Polisi litafanya kazi kwa weledi bila ya kuwa na upendeleo dhidi ya vyama vya upinzani linaweza likasaidia vyama  hivyo kukosa visingizio pale vinapokuwa vimeshindwa katika chaguzi mbalimbali hapa nchini.

Ni matumaini ya walio wengi kuwa kuelekea uchaguzi huu wa majimbo haya mawili hapatakuwa na malalamiko yaliyosikika katika chaguzi za kata 43 za udiwani, na kuacha malalamiko mengi na kusababisha baadhi ya vyama kususa.

You may also like