DAR ES SALAAM

Historia ya nchi yetu inawataja Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume kuwa waasisi wa Muungano wa nchi mbili zenye mashabihiano ya kihistoria.

Nchi hizo ni Tanganyika iliyotawaliwa na Ujerumani (1885-1918) baadaye Uingereza (1919-1961) ilipopata uhuru wake, na Zanzibar iliyotawaliwa na Uingereza chini ya usimamizi wa Sultani. 

Mwaka 1964, Field Marshal John Okelo akiwa na kikundi cha watu wenye silaha (wengi wao wakiwa wanachama wa ASP, wakishirikiana na wanachama wa Umma Party cha Abdulrahman Babu kwa maelekezo ya Sheikh Abeid Aman Karume) waliipindua serikali ya Sultani, hivyo Sheikh Karume kuunda serikali iliyojulikana kwa jina la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Sheikh Karume akawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Kassim Hanga akawa Makamu wa Rais na Abdulrahaman Babu na viongozi wengine wa ASP wakawa mawaziri katika serikali hiyo. 

Aprili 22, 1964, Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walisaini makubaliano ya kuziunganisha nchi mbili hizi; yaani Tanganyika na Zanzibar, mkataba huo ulipelekwa bungeni kupata baraka za Bunge na uhalali wa kisiasa na kisheria (Legal and Political Legitimacy) Aprili 25, 1964. 

Baada ya kujadiliana kwa kina wabunge waliridhia Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT). 

Kwa kipindi chote cha miaka 56 ya uhai wa Muungano wetu, Zanzibar ilikuwa imetoa Rais mmoja tu kuongoza Jamhuri ya Muungano; mzee Ally Hassan Mwinyi (1985-1995), ilhali Tanganyika ikiwatoa marais wanne ambao ni Mwalimu Nyerere (1961-1985), Benjamin Mkapa (1995-2005), Dk. Jakaya Kikwete (2005-20015) na Mwalimu Dk. John Magufuli (2015-2021).

Hatimaye katika mwaka wa 57 wa Muungano, Zanzibar imerejea tena katika kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano na kuandika historia mpya kwa mwanamke kuongoza ofisi ya juu kabisa nchini (Ofisi ya Rais – Ikulu), kwa hiyo kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi yetu, kwa sasa Muungano wetu umekuwa imara zaidi si kwa sababu Zanzibar imetoa Rais wa JMT, bali upande wa pili, yaani wanawake, ambao ni jeshi kubwa kwa sasa, wako Ikulu, kusimamia na kusukuma ajenda za maendeleo ya nchi yetu kwa ujasiri na weledi zaidi.

Ni imani yetu kwamba katika kipindi chote ambacho Mama Samia Suluhu Hassan atakuwa Ikulu, Muungano wetu utaimarika zaidi na zile changamoto ndogondogo za Muungano atazishughulikia kwa nguvu kubwa ili kuimarisha umoja na mshikamano baina ya Wazanzibari na ‘Wazanzibara’ hali kadhalika kwa kushirikiana na Dk. Hussein Ali Mwinyi, ataimarisha uhusiano baina ya Pemba na Unguja ili kuleta mshikamano na maendeleo visiwani kupitia sera ya Uchumi wa Bluu ya Dk. Mwinyi.

Katika kipindi hiki ambacho Rais wetu anatuunganisha sote; wa Tanzania Bara na Zanzibar, basi ni vema nasi tukamuunga mkono kwa kutenda na kuhamasisha amani na utulivu, hali kadhalika kwa kutenda yafuatayo:

Mosi, wapinzani, hususan CUF na ACT – Wazalendo (vyama vyenye uhai Zanzibar), tumuunge mkono Rais kwa kuondoa tofauti baina yetu kwani Waswahili wanasema umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. 

Haileti afya kwa watu tunaojenga nyumba moja kugombea fito, bali tunapaswa kupokezana fito.

Pili, tuhamasishe wananchi kujiletea maendeleo yao kwa kufanya kazi, kutunza na kulinda rasilimali tulizonazo (za asili na za kutengeneza), zaidi tuwaombe wafuasi waiunge mkono serikali katika jitihada zake kuwaletea maendeleo wananchi wote bila kujali maeneo ya kijiografia, rangi, dini, kabila au itikadi za kisiasa. 

Tatu, viongozi wa dini zote wasisitize kuitii mamlaka iliyo kuu (Serikali ya JMT), wasisitize umoja na mshikamano kwa waumini wao, vilevile watilie mkazo kuyaishi maadili mema kama zielekezavyo dini zao. 

Katika mafundisho yao, wasisitize wosia uliomo katika Rumi 13:1-6, hali kadhalika wawaelekeze kwamba asiyefanya kazi na asile. 

Nne, katika kuishi kwetu kama wananchi wa Tanzania ni vema tukakumbushana kanuni ya dhahabu (Golden Rule) kwamba yale yote tutakayo tutendewe na watu (ikiwamo Serikali ya Awamu ya Sita) nasi tuwatendee (tuitendee serikali) vivyo hivyo kwani hiyo ndiyo torati (sheria) na Manabii (Mathayo 7:12).

Tano, tofauti za kimtazamo na kiitikadi zinaweza kuwapo kwa kuwa hatufanani kifikra, kimtazamo, kimapokeo na kiitikadi hata maadili yetu hayafanani lakini tofauti zetu zisitutenganishe bali zituimarishe zaidi kwa ajili ya ustawi na uhai wa taifa letu kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.

Sita, nitumie fursa hii vilevile kuwaomba wale wote wanaomshauri Rais wafanye hivyo kwa busara na hekima kubwa, wasiongozwe na umimi, ukabila, wala ukanda au itikadi. Weledi ndio nguzo pekee inayoweza kututoa hapa tulipo na kusonga mbele zaidi. 

Saba, kwa sababu za kihistoria, Tanzania ni taifa linaloheshimika sana kusini mwa Jangwa la Sahara, Rais wetu ni mwanadiplomasia mbobezi, hivyo sina shaka na mahusiano ya kimataifa, niombe Watanzania wote waishio nje ya nchi yetu wawawakilishe nchi vema, waeneze sifa njema ya nchi yetu huko ugenini waishiko. 

Daima wakumbuke kwamba Tanzania ndiyo nyumbani kwao, wanaishi ugenini lakini babu, bibi na jamaa zao bado wanaishi katika nchi hii, hivyo wana wajibu wa kusaidia maendeleo ya nchi hii kimawazo, kifedha na kimkakati katika nyanja zote (uchumi, siasa na kijamii).

Nane, wizara inayohusiana na masuala ya Muungano ni vema ijikite kushughulikia kero chache ndogondogo za Muungano, ili Muungano wetu uendelee kuwa imara zaidi na kudumu kwa miaka mingi. 

Yale yote yanayoleta ukakasi (kama yapo) basi ni vizuri yakapatiwa majibu stahiki ili kuziba vinyufanyufa vinavyo tamkwatamkwa. Historia baina ya nchi hizi mbili (Zanzibar na Tanganyika) inaunganishwa na udugu wa damu. 

Kwamba utumwa na biashara ya utumwa imesababisha uwepo wa kina Mapunda, Mwakanjuki, Chacha, Mwita, Masawe kule Zanzibar. Hali kadhalika Wapemba na Waunguja wanapatikana katika maeneo mengi sana kwa upande wa Tanzania Bara. 

Hii ni ishara ya umoja na mshikamano tulio nao kama taifa. Hali hii haijaota tu kama uyoga, bali ni matokeo ya jitihada za muda mrefu, na kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya watu. 

CCM na serikali yake imelisimamia hili kwa busara na juhudi za kupigia mfano. 

Pale walipoishia watangulizi wake, Rais SSH anaanzia pale kusonga mbele kwa weledi, kasi na maarifa makubwa zaidi ili kufikia uchumi wa juu zaidi, kuongeza pato la mtu mmoja mmoja (per capita income) na pato la taifa (National Income). 

Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais Mama SSH. Amina.

Tuwasiliane: paulomapunda78@gmail/.com

0755671071

520 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!