BUKOBA

Na Phinias Bashaya

Sina uhakika na kisa hiki kama ni kweli au ni hadithi za ‘sungura akasema’, ingawa kinatajwa katika mji wa Bukoba na pengine ndivyo ilivyokuwa.

 Kwamba, mkazi mmoja wa mji huu alifunga safari akiwa na zawadi kumkaribisha mkuu mpya wa Mkoa wa Kagera. Miongoni mwa zawadi hizo ni maziwa.

 Kilichomtokea zawadi hazikupokewa na badala yake waliitwa walinzi na kuelekezwa huyo mgeni anywe maziwa yote akimaliza aondoke.

 Hakupewa fursa ya kueleza kusudio lake. Kiongozi huyo hakuwa tayari kutoa nafasi kwa watu wakarimu wanaojaribu kujenga ‘urafiki wa shaka’ katika kazi yake.

 Hapo hakuna wa kulaumiwa, pengine tayari alikuwa na mtazamo hasi kuhusu mji huo na watu wake. Hakutaka kunasa kwenye mtego wa wenyeji wenye ajenda binafsi mifukoni mwao.

 Kiongozi yeyote lazima ashangae. Watu wenye ajenda za pamoja za maendeleo hawawezi kushindwa kukubaliana kuhusu ujenzi wa kituo cha mabasi na soko jipya.

 Tangu tupate Uhuru mpaka leo abiria na magari yao wanaogelea kwenye tope. Bila shaka jambo hili litamshangaza sana Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali Charles Mbuge, na kutuondoa kwenye mkwamo.

Kutuondoa kwenye mkwamo ili kuficha aibu, kwa kuwa tunategemea ongezeko kubwa la wageni wa ndani na nje baada ya mkoa kuwa na hifadhi tatu za taifa; Burigi-Chato, Ibanda na Rumanyika.

 Aibu kwa wageni watakaofika Kagera kutekeleza mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga ambao kwa vyovyote vile wasingependa kunasa kwenye tope la sokoni.

 Wageni ambao hawawezi kukaa na kufanya matumizi kwenye mji unaomezwa na giza kuanzia saa mbili usiku kwa kukosa taa za barabarani. Hii ni kazi ya Baraza la Madiwani na hawahitaji ziara za mafunzo ili kujua kinachotokea kwenye miji mingine.

Badala yake madiwani wanahangaika eti kutafuta Sh milioni zaidi ya 400 kujenga kingo za Mto Kanoni kama suluhisho la mafuriko katika mji huu. Hizi ni ajenda binafsi za kisiasa kama yule aliyejificha kwenye zawadi ya lita za maziwa.

 Eti madiwani wa Bukoba wana haraka ya kujenga ukuta kwenye Mto Kanoni wakati tatizo la mafuriko ni ongezeko la shughuli za binadamu kando ya mto, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makazi hadi kwenye hifadhi ya mto.

Madiwani walewale hawana uchungu na mamilioni ya shilingi kwenye mradi wa kituo cha kuosha magari eneo la machinjioni uliotelekezwa. Hivi sasa mradi huo umegeuka shamba za viazi na mihogo.

 Hizi ni fedha zinazotokana na ushuru wanaotozwa mama lishe na wavuja jasho wengine. Kuruhusu matumizi yoyote mabaya ya fedha yao kupitia miradi ya aina hii ni kuhujumu jasho lao.

Baada ya stendi ya zamani kujaa tope, busara imewaelekeza kwamba magari ya abiria, isipokuwa yaendayo mikoani, kuhamia mbele ya Shule ya Msingi Rumuli kwenye vumbi. Wanasubiri tope likauke na kurejea tena.

Tunaona ni bora kuvuruga utulivu wa mazingira ya shule na usumbufu kwa wanafunzi na walimu kuliko kuruhusu kutumika kwa stendi mpya ya Kyakailabwa iliyoazimiwa miaka miwili iliyopita.

 Filamu ya stendi mpya ya Bukoba pamoja na makandokando yake inaweza kumsikitisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Baraza la Madiwani na mkurugenzi wao waliwahi kukubaliana tarehe ya kuhamia stendi mpya. Baadaye mpango uliyeyushwa na watu wasiojulikana.

 Msimamo wa Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali Mbuge, uko wazi na tayari ameonya kuwa kwa ngazi alizopitia hakuzoea lugha ya mchakato unaendelea na asingependa iwe hivyo Kagera.

 Kikao kazi chake cha kwanza alikutana na wadau wa kahawa, zao linalotegemewa kiuchumi kwa wananchi walio wengi. Hii ni dhahabu nyeusi inayotajwa kusomesha watoto wengi wa wakulima wa mkoa huu.

 Watoto wa wakulima ambao baada ya kunusa kuta za vyuo vikuu ndani na nje ya nchi wamesahau kwamba huko nyumbani katika mji wa Bukoba hakuna tawi la chuo kikuu, ukiondoa Chuo Kikuu Huria. 

 Miongoni mwa mambo mengi yaliyomshangaza ni wakulima kukaa na kahawa kwa muda mrefu baada ya kuvuna huku wakilazimika kusubiri kukamilika kwa mchakato wa kufungua msimu wa kununua.

Hii ni kero ya muda mrefu miongoni mwa nyingine nyingi kwa wakulima. Miaka mitano iliyopita walitangaziwa mnada wa zao hilo utaanza kufanyika mkoani hapa kama njia ya kujibu baadhi ya kero. Mchakato haujakamilika.

 Pamoja na umuhimu wa zao hili ni kilimo kisichowavutia vijana na hawana uvumilivu wa kusubiri kuuza kilo moja ya maganda  kwa Sh 1,200, tena kwa mkopo.

Bei ambayo haikuwahi kuongezeka kwa miaka mingi pamoja na juhudi za serikali za kufuta tozo, kero zaidi ya 10 ambazo ilitegemewa kiasi kilichokombolewa kingeongezwa kwenye bei ya kahawa.

Juhudi pia inatakiwa kuelekezwa katika kuhamasisha kilimo cha mazao mengine mbadala ya kiuchumi kama alizeti, parachichi na ufugaji wa samaki.

Wataalamu wamewahi kunukuliwa wakisema bonde lote la Mto Ngono linafaa kwa kilimo cha mpunga wa kutosheleza mahitaji ya ndani na ziada ya kuuza nje kama utafanyika uwekezaji mkubwa.

 Miaka miwili iliyopita mkoa ulikuwa na Wiki ya Kagera iliyokwenda sambamba na makongamano, pia maonyesho mbalimbali. Zilitajwa fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta tofauti katika wilaya zote za Kagera.

 Kwamba hili ni lango la kiuchumi, hasa kwa wawekezaji watakaokuja na mitaji yao ili kufanya uzalishaji huku wakilenga kuyafikia masoko mbalimbali kwenye nchi takriban tano zinazopakana na Mkoa wa Kagera.

 Hiyo ilikuwa ni mipango ya kwenye karatasi, kilichobaki ni miundombinu ili yaliyoandaliwa na wataalamu yatekelezeke. Siyo unashawishi watu wawekeze kwenye huduma ya hoteli za kitalii wakati mji wako umeshindwa kuweka taa za barabarani.

Bila shaka utatembelea soko la Kata ya Kashai na kuona kama hiyo ndiyo heshima wanayostahili kupewa wananchi ambao kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwenye makadirio ya watu mwaka 2016 ilikuwa na wakazi 34,944, wanawake wakiwa 18,274.

 Ni miongoni mwa kata zenye idadi kubwa ya watu nchini. Wakazi wa mji huu huenda wanafuatilia kwa karibu mjadala wa pendekezo la kuanzisha mkoa mpya wa Chato na si umuhimu wa kuigawa kata hiyo.

 Kuna visingizio vingi vinavyojenga sababu ya anguko la mkoa, hasa kiuchumi, nyuma yake tukiwa na ubinafsi wa wanasiasa. Karibu Meja Jenerali Charles Mbuge kwa ajili ya mwanzo mpya.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge, akipokea nyaraka kutoka kwa mtangulizi wake, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, aliyehamishiwa Mkoa wa Mtwara.

749 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!