*Yawaonya wageni waliojipenyeza kuimiliki kinyemela

Serikali imeendelea kuwapiga marufuku wageni kutoka mataifa jirani na Tanzania, kujipenyeza na kumiliki ardhi kinyemela hapa nchini.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesisitiza kuwa wegeni na wenyeji watakaobainika kuuziana au kukodishana ardhi, hawataonewa huruma.

 

Waziri Tobaijuka amerejea msimamo huo wa Serikali wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, bungeni mjini Dodom, juzi.

 

“Sheria za ardhi Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999 zinatoa miongozo muhimu ya kumiliki ardhi Tanzania na inalinda vyema maslahi ya wananchi.

 

“Wageni wengi, hasa kutoka nchi jirani wameendelea kujipenyeza ili kumiliki ardhi kwa njia za udanganyifu na mara nyingine wakisaidiwa na baadhi ya wananchi na hata viongozi waliopoteza maadili.

 

“Ninaendelea kuikemea tabia ya kuwasaidia wageni kujipatia ardhi kwa njia zisizokuwa halali. Wafuate njia zilizoainishwa kisheria. Ninarudia kusisitiza kuwa wenye tabia hiyo waiache mara moja maana wakibainika, hawatavumiliwa kamwe na sheria itachukua mkondo wake,” amesema.

 

Katika kutekeleza Sheria ya Ardhi Na. 4 ya 1999, Waziri huyo amesema hadi Aprili, mwaka huu Wizara ilitoa hatimiliki 21,846 sawa na asilimia 54.62 ya lengo la kutoa hatimiliki 40,000 kwa mwaka; ilishughulikia maombi ya uhamisho wa milki 672 kati ya lengo la kushughulikia uhamisho wa milki 1,700 kwa mwaka na ilani za ubatilisho 3,053 zilitumwa kwa wamiliki waliokiuka masharti ya umiliki.

 

“Napenda kusisitiza na kutoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinamilikisha viwanja vyote vilivyopimwa na kuandaa hati ili wananchi waweze kuwa na milki salama. Wizara inakusudia kushughulikia ubatilisho wa milki zote zinazokiuka masharti ya uendelezaji wa viwanja na mashamba ili ardhi iliyomilikishwa itumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

“Mwaka 2012/2013 Wizara iliweka lengo la kutoa Vyeti 2,007 vya Ardhi ya Kijiji, lakini hadi Aprili, 2013 Wizara ilitoa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji 469. Kutokufikiwa kwa lengo hili la utoaji wa vyeti vya Ardhi ya Vijiji kunatokana na mabadiliko ya mipaka ya vijiji inayolazimu upimaji wa mipaka ya vijiji kurudiwa, na wakati mwingine migogoro kuhusu mipaka hiyo kuibuka na kuchelewesha upimaji,” amesema.

 

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho, Wizara iliratibu uandaaji, usajili  na  utoaji wa Hati za Hakimilki ya Kimila 32,155 katika Halmashauri za Wilaya ikilinganishwa na lengo la kutoa Hatimilki za Kimila 50,000. Pia, Masjala za Ardhi 122 zilianzishwa katika vijiji na wilaya mbalimbali nchini.

By Jamhuri