Uamuzi unaotarajiwa kutangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu hatima ya Pori Tengefu la Loliondo, ndiyo utakaotoa mwelekeo wa uhifadhi nchini.

Kumekuwapo habari kwamba Serikali imeyumba kuhusu suala la Loliondo baada ya uamuzi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kutenga eneo la kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, ushoroba (mapito) na mazalio ya wanyamapori.

 

Baadhi ya wabunge wanasema endapo Waziri Mkuu atasalimu amri kwa shinikizo la wabunge kadhaa wenye asili ya eneo hilo, hatua hiyo inaweza kuibua migogoro mingi kwenye maeneo ya uhifadhi yanayopakana na mapori tengefu, hifadhi za taifa, na kadhalika.

 

Wanasema hatua hiyo inaweza kuwapa nguvu wananchi wa Mtwara kuendelea kung’ang’ania rasilimali ya gesi iliyopatikana mkoani mwao.

 

“Waziri Mkuu akitoa uamuzi tofauti na uliotangazwa na Waziri Kagasheki, ajue ataibua migogoro mingi sana nchini kwa sababu kila watu watadai maeneo yao. Uchunguzi wa kisayansi unaonesha kabisa kuwa eneo la Loliondo tayari limeanza kuathiriwa na shughuli za kibinadamu. Kwa sasa kilimo kinaendelea kwa kasi, huwezi kutarajia uhifadhi endelevu katika eneo hilo bila kuzingatia kilichoamuriwa na Kagasheki kisheria,” amesema mmoja wa wabunge.

 

Wakati kukiwa na taarifa hizo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake (Tanzania Bara) Mwigulu Nchemba, na baadhi ya mawaziri, akiwamo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye, wanashinikiza Serikali itengue uamuzi wa kulimega eneo hilo.

 

Hata hivyo, watu walio karibu na Rais Jakaya Kikwete wanasema kiongozi huyo anakubaliana na uamuzi uliochukuliwa na Kagasheki.

Please follow and like us:
Pin Share