Serikali imeingiza kipato cha Sh bilioni 114.4 kutoka kwa watalii 6,730,178 waliozuru nchini wakitokea mataifa mbalimbali, katika misimu ya 2001/2002 na 2011/2012.

Takwimu hizo, kwa mujibu wa Gazeti la Daily News toleo la Machi 28, mwaka huu, zimetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Allan Kijazi.


Kijazi amesema kuwa katika kipindi cha mwaka jana pekee, Taifa lilikusanya Sh 109,372,608,221 kutoka kwa watalii 945,794, ikilinganishwa na Sh 102,515,251,757 zilizokusanywa mwaka juzi kutoka kwa watalii 1,019,027.


Amesema mapato hayo ya mwaka jana ni makubwa ikilinganishwa na Sh 15,748,972,000 zilizokusanywa kutoka kwa watalii 345,796 katika msimu wa 2001/2002.


Hadi sasa nchi zinazoongoza kwa watalii wengi wanaozuru hifadhi mbalimbali za Taifa nchini, ni Marekani, Uingereza, Afrika Kusini, Ujerumani, Ufaransa na Uhispania.


Kwa mujibu wa Kijazi, Programu ya Uzalishaji Mapato ya TANAPA iliyozinduliwa mwaka wa fedha 2004/2005, ilianzishwa kwa ajili ya kushughulikia mapendekezo ya tathmini ya mwaka 2000, 2006 na 2010.


Amesema utafiti huo uliofanyika kabla ya mapendekezo hayo kukusanywa, ulionesha kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa wa mapato katika jamii zinazopakana na Hifadhi za Taifa.


Ametaja ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya matumizi ya ardhi jirani na Hifadhi za Taifa, kama moja ya changamoto zinazoikabili TANAPA.


Amesema kuwa kumekuwapo pia na baadhi ya wananchi kuvamia hifadhi pamoja na migogoro ya kugombea mipaka ya ardhi kati ya shirika hilo la umma na wanavijiji.


Ametaja changamoto nyingine kuwa ni umaskini na uelewa mdogo miongoni mwa jamii, mahitaji makubwa ya faida kwa jamii, migogoro ya binadamu na wanyama, na vitendo vya ujangili hifadhini.

Please follow and like us:
Pin Share