Inatoka toleo lililopita.

Jicho la kulia linaona dini ni mojawapo ya ngao zake katika kuwadhibiti na kuwahukumu raia wake wenye kutenda maovu au kwenda kinyume cha sheria za dola.

Si hivyo tu, serikali inatuhumiwa kama mshirika mkubwa katika vitendo vya udini, na ni ngao ya kukinga malalamiko na madai dhidi ya udini. Yote hayo kwake serikali ni ndumakuwili.


Ifahamike kwamba suala la udini halikuanza hivi karibuni kama baadhi ya watu wanavyotaka kutuaminisha. Udini nchini mwetu ulianza tangu ukoloni ulipoingia na kuanzisha utawala wake. Naanzia hapo kwa sababu ndiyo chanzo cha udini na mtafaruku ulipo hivi sasa.


Mwaka 1885, wakati wakoloni wa Kijerumani walipoingia Afrika Mashariki na kuanza kupanua utawala wao kutoka pwani hadi bara, walikuta lugha ya Kiswahili ikitumiwa na wafanyabiashara wa pwani na bara. Pia lugha hiyo ilikuwa ikitumiwa na Wamisionari katika kueneza mafunzo ya Biblia.


Lakini wamisionari wa Kijerumani na wa madhehebu ya Kilutheri walipinga sana matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa sababu:


Kiswahili ni lugha ya kitumwa iliyotumiwa na Waarabu katika kuendeleza utumwa. Kiswahili kinaambatana mno na dini ya Kiislamu, kwa hiyo kikiruhusiwa kutumika kitafanya kazi ya kueneza dini ya Kiislamu kwa urahisi na hivyo kuhatarisha maendeleo ya uenezi wa dini ya Kikristo hasa huko Bara.


Wakristo hao walidai lugha za kikabila ndizo zitakazofaa kutumika katika mafunzo ya Biblia. Walutheri walidai pia serikali ilikuwa inawaajiri watumishi wenye ujuzi wa Kiswahili ambao wengi wao walikuwa Waislamu wa pwani, kwa hiyo serikali ilikuwa inaendesha upendeleo kwa dini ya Kiislamu na  kuiweka kando dini ya Kikristo.


Lakini madhehebu ya Kikatoliki na ya UMCA (Anglikana), yaliunga mkono uamuzi wa serikali wa kutambua lugha ya Kiswahili katika shughuli zake mbalimbali na kufundisha shuleni. Makanisa ya Kiroma na ya UMCA yalitumia Kiswahili kwa kuanzisha magazeti.

UMCA walianzisha gazeti la Habari za Mwezi mwaka 1895.


Wakatoliki walianzisha gazeti la Kiongozi mwaka 1905.

Hatimaye Walutheri walikubali uamuzi wa serikali kutumia Kiswahili na wao kuanzisha gazeti la Pwani na Bara mwaka 1910.


Ulipoingia utawala wa Kiingereza mwaka 1919, nao ulileta elimu iliyokuwa ya ubaguzi wa rangi na dini. Shule nyingi ziliendeshwa na mashirika ya dini mbalimbali. Kwa sababu ambazo si za dini yalijenga tabia ya uhasama mkubwa baina ya vijana wa madhehebu haya na yale, au wa madhehebu yale yale.


Serikali yenyewe ilisomesha vijana kwa lengo au madhumuni maalum ya kuwapa kazi ambazo hazitahatarisha utawala wake. Vijana waliokuwa na nidhamu ya woga walipendwa na wale waliokuwa wadadisi walifukuzwa shule mapema. Elimu ilikuwa si kwa wote kwani ilikuwa ama ya gharama au vizingiti.


Waarabu walijikita zaidi katika kufundisha dini ya Kiislamu na kufanya biashara. Hivyo wenyeji wa pwani hadi bara waliipokea dini ya Kiislamu wakawa Waislamu.


Hivyo ni vigumu Mwislamu kuacha dini yake ya kweli kwa mujibu wa kitabu chake, yaani Qur’an na kufuata dini nyingine. Hata hivyo, Waislamu wachache mno walikubali ubatizo (Ukristo) ili wapate elimu.

ITAENDELEA

841 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!