Wote tunakubali kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Kumnyima mtu au kundi moja ni sawa kumnyima mtu au kundi hilo maendeleo ya maisha yeke au yao katika uchumi madaraka, ajira na tija nyinginezo.

Tangu kupevuka kwa harakati za kudai Uhuru mwaka 1953 chini ya TAA (Tanganyika African Association) na kushamiri kwa harakati hizo chini ya TANU, mwaka 1954; suala la elimu lilipewa nafasi pekee katika mazungumzo na mipango ya kudai uhuru katika vikao mbalimbali. Waasisi wa TANU walio wengi walikuwa Waislamu walionyimwa elimu na Mkoloni kwa sababu tu ya udini lakini walitambua thamani ya elimu kutoka katika elimu yao ya dini ya Kiislamu.


Rais wa TANU, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikiri mara kadhaa kuwapo ubaguzi wa utoaji elimu katika mazingira ya kidini kwa wananchi, na hasa Waislamu waliodhulumiwa haki yao ya elimu na kupewa wenzao wasio Waislamu. Mwalimu aliahidi kuondoa kasoro hiyo TANU itakapotawala nchi.


Baada ya mkutano wa kwanza wa TANU tangu kuzaliwa na kumchagua Mwalimu Nyerere kuwa Rais wa kwanza; madhumuni ya TANU yalitangazwa. Moja ya madhumuni hayo ni kuhusu elimu. TANU ilisema lazima watoto wa wananchi wapate nafasi zaidi ya kusoma katika shule zote za msingi na sekondari.


Imani ya kupata elimu zaidi na bora ilijengeka pale TANU ilipofanya Mkutano Mkuu wa mwaka mjini Tabora mwaka 1958 na kupitisha Azimio la kuanzishwa Chuo Kikuu. Aidha, umuhimu wa elimu ya ufundi na elimu kwa wote pamoja na elimu ya watu wazima.


Lakini, ukweli ni kwamba matatizo ya kutumia dini yaliendelezwa tangu wakati wa kuunda TANU mwaka 1954 na baada ya Uhuru. Kwani aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU, Sheikh Sulemani Takadir katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika mjini Tabora mwaka 1958, alitoswa baada ya kutoa madai ya kutumika udini katika shule ya mchanganyiko ya Ugweno kwa kusema; “Nimepata barua kutoka shule ya Waislamu ya Ugweno kuwa nafasi zote zimechukuliwa na Wakristo na kwamba watoto wa Waislamu wanateswa.”


Kwa kauli hiyo alinyang’anywa kadi ya TANU ya uanachama na kufukuzwa chamani, kwa madai ya kutaka kutia sumu ya dini ya TANU. Mwaka 1960 baadhi ya masheikh na walimu wa Kiislamu waliunda chama cha siasa cha All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT). Baada ya kuundwa chama hicho, Kamati kuu ya TANU iliunda tume yenye wajumbe mchanganyiko wa Wakristo na Waislamu kupinga kuwapo kwa chama hicho kwa madai kuwa ni cha dini. Pili, kuwaelewesha Wakristo na Waislamu madhumuni ya TANU na ubaya wa kutumia vyama vya dini kuwagawa wananchi.


Tume hiyo ilipofika Kigoma iligundua karatasi zilizotayarishwa na mapadre kuwashawishi Wakristo, kwamba Waislamu hawakuwa na elimu na kuwataka Wakristo wote popote walipo waungane kuwanyima Waislamu nafasi za uongozi wa Taifa.


Katika Uchaguzi Mkuu wa Pili wa Tanganyika uliofanyika Julai 1960, katika Wilaya ya Mbulu mkoani Arusha, iliyokuwa ‘Mbulu Tribal Council’ iliazimiwa kwamba Chifu Amiri Dodo, mjumbe wa TANU, asipewe kura.


Naye Chifu Sarwatt alitoa agizo kwa wajumbe wake kuwa kura apewe mwanawe Herman Ngildi Sarwatt na baadhi ya wakuu wa madhehebu ya dini walikuwa wanahubiri kwamba Chifu Amiri Dodo ni Mwislamu, kwa hiyo wampigie kura Herman Ngildi Sarwatt ambaye ni Mkatoliki. Katika uchaguzi huo, TANU ilishindwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za udini na ukabila.


Baada ya kueleza yote hayo hebu tutafakari kauli zifuatazo, zilizowahi kutolewa na viongozi wafuatao:


I. “Tulikuwa hatujali kabisa dini ya mtu hata kidogo. Tulikuwa hatuchagui mtu kwa dini yake, kwani anakuja kusalisha hapa?” Kauli hii ilitolewa na Mwalimu Julius K. Nyerere.

II. “Katika hali halisi kuna ukiukaji wa haki na matumizi mabaya ya madaraka, ambapo tabia hii inaelekea kukubalika na kupewa hadhi ya utamaduni.” Hii ilitolewa na Padre Vic Missiaen.


Kwa leo katika sehemu hii ya kwanza ya udini, napiga magoti kwa serikali na kuiambia yafuatayo:


Nasema mapema kwa serikali suala la udini lipo na limetamalaki. Katika suala hili serikali iache purukushani. Ichukue hatua za haraka na kuzingatia busara katika kuliondoa kwani hata tume ya marekebisho ya Katiba imekiri hadharani kuwa udini upo.


Lakini pia serikali isijadili na kuhukumu matokeo ya udini, bali itafute kwa kina chanzo cha udini na maana halisi ya neno ‘Udini’. Wahenga walisema ‘mdharau mwiba mguu huota tende’.

1160 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!