*Wananchi kadhaa walia kuwapo dalili za ubaguzi

*Mmoja adai kigezo cha kupitia JKT kinaumiza

*Mbunge: Sababu ni Serikali kukosa mfumo imara

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Serikali imetangaza ajira takriban 1,450 kwa vijana kwa ajili ya kujaza nafasi kwenye taasisi zake mbili nyeti, lakini tayari malalamiko ya ‘ubaguzi’ yameibuliwa na baadhi ya waombaji.

Malalamiko haya yanakuja wiki chache baada ya vijana waliohitimu kidato cha nne na kupata ufaulu wa madaraja ya juu kunyimwa ajira na kuchukuliwa waliopata daraja la nne na la tatu.

Ajira zilizotangazwa kupitia Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma (PSRS) ni 1,097 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na nafasi 350 kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Miongoni mwa vigezo vilivyowekwa na Takukuru kwa vijana wanaotakiwa ni kuwa wawe wamepitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mmoja wa wazazi wa kijana aliyehitimu kidato cha sita na kufaulu vizuri anasema kigezo hicho kinamtupa nje ya mchakato mtoto wake.

“Nimefuatilia suala la ajira zinazotolewa na serikali na kigezo kikiwa ni lazima waombaji wawe wamepita JKT. Mimi ninaona kama hiki kigezo ni cha kibaguzi kwa kiwango fulani,” anasema mzazi huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Anasema nafasi za vijana kujiunga JKT siku zote huwa finyu na si wahitimu wote wa sekondari (kidato cha nne na cha sita) wanaozipata.

“Pamoja na ukweli huo, nafasi za kazi zinadai mtu anayetakiwa lazima awe na kigezo hicho,” anasema.

Anatoa mfano wa mdogo wake aliyehitimu kidato cha sita mwaka 2016 na kupata daraja la II, akisema vijana waliokwenda JKT mwaka huo kwa mujibu wa sheria ni waliokuwa wamefaulu kwa daraja la I.

“Kuna wakati wanatumia kigezo cha alfabeti za majina ya vijana; mfano wenye majina yanayoanzia ‘A’ tu ndio wanakwenda JKT kwa mwaka husika.

“Sasa kama nafasi za Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na sasa Takukuru (nafasi 350) zote hizo moja ya vigezo ni mafunzo ya JKT, mbona vijana wengi wataachwa mtaani bila kujaribu bahati yao kuomba nafasi hizi?” anahoji kwa masikitiko.

Anashauri kuwa kigezo cha kupitia mafunzo ya JKT kisiwe cha lazima kujiunga kwenye majeshi, bali kiwe nyongeza tu kwa waliokidhi vigezo vingine vya elimu na usaili.

Mbunge mstaafu azungumza

Akizungumza na JAMHURI kuhusu kigezo cha kupitia JKT kutumika kuengua hata vijana wenye sifa za kujiunga kwenye majeshi, aliyekuwa Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi, anasema hali hiyo inatokana na serikali kukosa mfumo imara.

“Ni kama lile suala la wenye ufaulu wa juu kukataliwa kujiunga Uhamiaji na Polisi. Ukitazama kwa kina ni sahihi, kwa kuwa ni kweli kuna kada fulani ya waajiriwa inayotakiwa kwa vigezo vyao.

“Lakini kwa ujumla ni kwa sababu Tanzania tumekosa mfumo imara wa ajira na hata wa elimu. Tumeua vyuo vya kati na kuvipandisha hadhi vingine kuwa vyuo vikuu.

“Sasa kila kijana ana shahada na ukiwa na shahada kuna kazi huwezi kupewa au kuzifanya! Hizo zinastahili watu wa kada fulani ya elimu (chini ya shahada).

“Unakuja kwenye suala la JKT. Ule mfumo wa zamani tumeuondoa, sasa wanaokwenda JKT ni wenye bahati.

“Ukizungumza na vijana, utaona namna walivyokatishwa tamaa kwa kuwekewa kigezo hicho. Mtu anatamani kwenda JKT, lakini nafasi hakuna, unaikosa fursa hiyo kwa sababu mfumo hauwezi kuwachukua vijana wote! Halafu anakuja kuambiwa kama haukupita JKT haupati kazi.

“Hapa lazima kutakuwa na malalamiko ya upendeleo. Lakini ukweli unabaki palepale, hatuna mfumo mzuri unaotoa uhuru wa vijana kushindana kwenye soko la ajira,” anasema Arfi ambaye amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Tangazo la ajira

Nafasi zilizotangazwa kupitia tangazo lililotolewa na Katibu wa PSRS, Xavier Daudi, Oktoba 22, mwaka huu linapatikana pia katika tovuti ya Gazeti la JAMHURI (www.jamhurimedia.co.tz). Ajira hizo na idadi ya wanaotakiwa ikiwa kwenye mabano ni:

Tax Management Officer II nafasi 294; Tax Management Assistant II (326); Customs Officer II (167); Customs Assistant II (114), Ofisa Uhusiano (3), na ICT Technician II (30).

Nafasi nyingine ni ICT Officer II (computer systems analysis and development) nafasi 31; Officer II (network administrator) (2); ICT Officer II (database administration) (6); ICT Officer II (systems risks and security) (6); ICT Officer II (computer/business application support) (6); ICT Officer II (computer system administration) (19); ICT Officer II (business analyst-computer systems analysis and development) (1) na ICT Officer II (business analyst-database administration).

Nafasi nyingine ni ICT Officer II (business analyst-systems risks and security) (1); Records Management Assistant II (18); madereva II (59); Legal Counsel (3); Rating II (1); Accounts Assistant II (4) na Katibu Binafsi II (5).

Mbali na sifa nyingine za kitaaluma kwa nafasi hizo za kazi pia tangazo hilo limeainisha baadhi ya sifa za jumla kwa waombaji wote kuwa ni uadilifu, uwajibikaji, uwezo wa kutatua matatizo na kufanya uamuzi, uwezo wa kuongoza na uwezo wa kutumia kompyuta.

Sifa nyingine kwa waombaji hao ni lazima wawe Watanzania wasiozidi umri wa miaka 45 isipokuwa kwa wale ambao ni watumishi wa umma.

“Walioomba nafasi za ajira za TRA kupitia tangazo la Juni Mosi, mwaka huu lenye kumbukumbu namba EA.7/96/01/L/126 nao wanaruhusiwa kuomba tena. Mwisho wa kupeleka maombi kwa nafasi hizo ni Novemba 4, 2021,” inasomeka sehemu ya tangazo hilo.

Takukuru kwa upande wao wametangaza nafasi 350 za ajira; 200 zikiwa za maofisa wachunguzi na 150 kwa ajili ya maofisa wachunguzi wasaidizi.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Oktoba 23, mwaka huu linalopatikana pia katika tovuti ya Gazeti la JAMHURI, sifa za jumla za kitaaluma za waombaji wote wa nafasi hizo ni kuwa raia wa Tanzania.

Waombaji wa nafasi za maofisa wachunguzi wanatakiwa wawe angalau na elimu ya shahada ya kwanza iliyotolewa na chuo kinachotambuliwa na serikali katika fani yoyote, ikiwamo mambo ya kale na utalii, sheria, uhasibu, teknolojia ya habari, elektroniki, misitu, kilimo, ununuzi, uchumi na mipango, mifugo na usimamizi wa rasilimali watu.

Fani nyingine ni takwimu, utawala wa umma/serikali, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi na uthamini wa ardhi, mafuta na gesi, ukadiriaji wa ujenzi, uhandisi wa umeme, uhandisi katika kemia, usanifu majengo, mambo ya anga, uhandisi wa mitambo, uhandisi wa ujenzi na uhandisi wa maji.

Waombaji wa nafasi za maofisa uchunguzi wasaidizi wanatakiwa wawe na cheti cha elimu ya kidato cha nne au kidato cha sita, astashahada au stashahada ya fani yoyote inayotolewa na taasisi au chuo kinachotambuliwa na serikali katika fani za kupaka rangi, ufundi magari, vifaa vya muziki, utunzaji kumbukumbu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), maendeleo ya jamii, uhazili na menejimenti ya hoteli.

Waombaji wote wanatakiwa wawe Watanzania wenye umri usiozidi miaka 30 na wawe wamepitia mafunzo ya JKT.

“Wawe waadilifu na barua zote ziandikwe kwa mkono kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Mwisho wa kutuma maombi hayo ni Novemba 8, mwaka huu. Watakaoajiriwa watapangiwa kazi kadiri ya uamuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,” inasomeka sehemu ya mwisho ya tangazo hilo.

1807 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!