*Lafikia Sh trilioni 77.9 kutoka Sh trilioni 10.8 (2005), Sh trilioni 14.2 (2010), Sh trilioni 63.9 (2019)

KIBAHA

Na Costantine Muganyizi

Mzigo wa deni la taifa umezidi kuongezeka ingawa kiasi cha takriban Sh trilioni 77.9 ambazo Tanzania ilikuwa inadaiwa hadi mwishoni mwa Agosti mwaka huu bado si tishio kwa uchumi wa taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Maana yake kitaalamu na kiuchumi ni kwamba, deni hilo bado ni himilivu.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), deni hilo lilikuwa himilivu hata Agosti 2005 na 2010 lilipokuwa Sh trilioni 10.8 na Sh trilioni 14.2 mtawalia. 

Kati ya Agosti 2015 na Agosti 2019, lilikua kwa asilimia 57.4 hadi kufikia Sh trilioni 63.9 kabla ya kupaa hadi kufikia Sh trilioni 68.8 Agosti mwaka jana lakini bado likaendelea kuwa himilivu.

“Uhimilivu wa deni ni hali ambayo mkopaji anatarajiwa kulipa madeni yake bila kuhitaji msamaha, kuwa na malimbikizo ya malipo, na bila kuathiri ukuaji wa uchumi,” Ofisa Mwandamizi wa Hazina ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, ameliambia JAMHURI katika mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita.

Wakati anawasilisha Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2021/22, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, aliliambia Bunge kuwa viashiria vya deni la serikali bado viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

Deni la serikali ndilo sehemu kubwa ya deni la taifa ambalo kiongozi huyo anasema pamoja na kuongezeka kwake, bado linaendelea kuwa himilivu.

Uhimilivu huo si mtazamo wa serikali peke yake kupitia msimamizi mkuu wa deni la taifa ambaye ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) lakini pia ndio msimamo wa hata taasisi za fedha za kimataifa; likiwamo Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambalo ndilo kiranja wa masuala hayo kimataifa.

Taasisi nyingine zenye mtazamo chanya wa deni la Tanzania pamoja na kuongezeka kwake kwa kiasi cha kutia hofu kwa baadhi ya watu hasa kwenye miaka ya hivi karibuni ni pamoja na Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC) ambayo wiki jana ilibaini dosari kadhaa kwenye deni hilo nayo inaamini bado fedha Tanzania inazodaiwa ndani na nje ya nchi si tishio wala hatarishi kiuchumi.

“Tumeangalia viwango vinavyokubalika ambapo imeonekana deni letu ni himilivu na halina shida. Lakini changamoto iliyopo, nchi imeingia katika kipato cha kati, kwa hiyo ina maana hata vigezo vya mkopo vinabadilika ili tujue vigezo vyetu sasa ni vipi,” anasema Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga.

Agosti 2015, miezi miwili kabla ya kuanza muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu Tano, deni hilo lilikuwa Sh trilioni 40.6. Kwa hesabu za haraka haraka, deni la taifa limeongezeka kwa Sh trilioni 37.3 katika kipindi cha miaka sita kati ya Agosti 2015 na Agosti mwaka huu.

Huu ni wastani wa ukopaji wa Sh trilioni 6.2 kwa mwaka na ukuaji wa asilimia karibu 92 katika kipindi hicho cha miaka sita. Februari mwaka huu, deni la taifa lilikuwa Sh trilioni 72.5 na Sh trilioni 33.5 mwezi huo mwaka 2015.

“Kukopa si tatizo kama hilo linafanyika kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo na yenye tija kwa taifa, na kwa namna tofauti, linachochea uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi kwa ujumla,” Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini, Jens Reinke, anabainisha.

Wanaoliangalia suala hili tofauti, wanasema kasi ya kuongezeka kwa deni la taifa si rafiki sana kimaendeleo hasa ikizingatiwa hali halisi ya uchumi na uwekezaji ambayo sasa hivi inakabiliwa na changamoto nyingi, hususan zile zinazotokana na janga la Uviko-19.

Miongoni mwa mambo ambayo kundi hili linapendekeza kama njia sahihi ya kudhibiti kuendelea kupaa kwa deni la taifa ni serikali kuwa inapata idhini ya Bunge kila inapotaka kukopa. 

Na ili hilo lifanyike kikamilifu, iwepo sheria inayoibana serikali kutokopa bila baraka za Bunge.

Wenye mtazamo huu wanasema kuibana serikali kisheria kutasaidia kupunguza kasi ya kuongezeka kwake ambayo imekuwa si ya kawaida tangu mwaka 2015.

Wengi wao wanahoji kuwa deni hilo linakuwa himilivu kivipi wakati linazidi kuwa kubwa na mzigo kifedha, kwani ulipaji wake unaligharimu taifa fedha nyingi kila mwaka.

Kwenye bajeti ya mwaka huu, Sh trilioni 10.66 zitatumika kwa ajili ya ulipaji wa deni la serikali peke yake, kiasi ambacho ni kama asilimia 29 ya matumizi yote ya mwaka huu wa fedha. 

Kwa mujibu wa wataalamu wa BoT, kuna tofauti kati ya deni la taifa na deni la serikali. Deni la taifa linajumuisha deni la serikali (la ndani na nje) na deni la nje la sekta binafsi. Deni la nje la serikali linajumuisha pia deni la taasisi za serikali.

Wakati Sh trilioni 10.66 zitatumika kulipia madeni ya serikali, fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwenye bajeti ya 2021/22 ni Sh trilioni 13.33 pekee. 

Kiasi hicho ni zaidi ya mara nane ya fedha za mkopo wa IMF wa kukabiliana na changamoto za Uviko-19 ambao Tanzania iliupata mwezi uliopita.

Shirika hilo la fedha linasema pamoja na janga hilo kuongeza mzigo wa deni la taifa, hasa kwa kuathiri ulipaji wa deni la nje, bado nchi iko salama, kwa sababu deni hilo limeendelea kuwa himilivu wakati wa kipindi hiki kigumu.

By Jamhuri