DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Ni jambo jema kufanya kitu chenye masilahi mapana kwa nchi yako. Kama hivyo ndivyo, ninaomba tusafiri sote kupitia maandishi ya makala hii ili kumfahamu Meja Jenerali Zawadi Madawili.

Madawili ni mwanamke wa kwanza hapa nchini kuhudumu katika cheo kikubwa cha Meja Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Ndiyo. Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Kwa mujibu wa mahojiano yaliyorushwa hewani hivi karibuni katika kipindi cha ‘Nyota wa Wiki’ cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ni kwamba haikuwa kazi rahisi kwake kufika hapo hadi alipostaafu kazi jeshini na anasema kamwe hakukubali kushindwa na kusema hawezi.

Madawili ni mstaafu na ameitumikia JWTZ kwa miaka 36. Amezaliwa mwaka 1949 katika Kijiji cha Malangali, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Mwaka 1957 alipata fursa ya kujiunga na Shule ya Msingi Malangali na mwaka 1966 alijiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza iliyopo mkoani Mbeya.

Pia mwaka 1970 na 1971 alipata mafunzo ya utumishi wa umma na hatimaye Februari, 1972 akaanza safari yake jeshini na kuendelea kupata fursa mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya nchi na kumwezesha kupanda vyeo hatua kwa hatua hadi kufikia cheo hicho mwaka 2007 na kustaafu Juni 30, 2008.

Sababu zilizomfanya ajiunge JWTZ ni nini?

Madawili anasema: “Labda nirudi nyuma kidogo niwashukuru sana UWT, wao ndio waliibua wazo kwamba kuna kazi zinazojulikana kama kazi za wanaume, kazi hizi tungependekeza wanawake pia wawemo, na moja ilikuwa jeshi.” 

Anasema baada ya hapo serikali ikakubali na kuanza kuajiri wanawake jeshini na kilichomvutia ni kutaka kuona kama wanawake hawawezi.

“Nikasema hivi kweli siwezi, kama wao wanaweza kwa nini mimi nisiweze, hilo la kwanza,” anasema na kuongeza:

“Pili, nikasema basi nishiriki kwenye ulinzi wa nchi yetu kupitia JWTZ, na hasa baada ya Mwalimu Nyerere kusema kwamba ulinzi ni wa watu wote – wanawake na wanaume, kwa hiyo ilinivutia sana, nikaona ni vema na mimi nikajiunga.

“Nilipokwenda jeshini nilikuwa sifahamu kabisa, nilipofika ndiyo nikakutana na changamoto na fursa, kwa hiyo nikaendelea nazo hadi nilipomaliza. Kwa kweli zile wiki za awali mazingira niliyokutana nayo siku ya kwanza yalikuwa na changamoto zake kwa maana kwamba; kwanza, mafunzo yenyewe kweli yalikuwa magumu, hilo la kwanza.”

Pia anasema changamoto nyingine ilikuwa katika mavazi, kwa kuwa walilazimika kuvaa fulana na bukta na hali hiyo ikaleta changamoto kwa mtu aliyezoea kuvaa vitu vingine.

Pamoja na changamoto hizo, akakataa kwa kusema hapana, kwa kuwa amekuja kwa nia njema ya kuitumikia nchi hivyo atakabiliana nazo.

“Waliokuwa wanatoa mafunzo wote ni wanaume, kwa sababu bado kulikuwa hakuna mwanamke pale jeshini isipokuwa tulikuwa na matroni wetu ambaye aliazimwa kutoka JKT na huyo alikuwa mwanamke peke yake,” anasema na kuongeza:

“Wakati ninajiunga tulikuwa wengi na wenzangu, kwa hiyo wote tulijiunga kwa pamoja na wote tulifanya mafunzo kwa pamoja na wote tukamaliza kwa pamoja, nilikuwa mwanamke wa kwanza kuwa ofisa ndani ya jeshi. 

“Baada ya kufanya mafunzo ya awali na kumaliza ikabidi sasa jeshi liwe na viongozi wanawake, kwa sababu tayari limeshadhamiria na serikali ilikuwa imeshadhamiria kuajiri wanajeshi wanawake, kwa hiyo lazima kuwa na viongozi wanawake.”

Anasema hapo ndipo sasa ilipotokea hiyo hoja ya ‘mwanamke wa kwanza’ na kwa bahati mbaya wakati huo hakukuwa na chuo kinachofundisha wanawake maofisa kadeti kuwa maofisa.

Anasema ikabidi serikali wafanye mpango na wakapelekwa nchini Canada na aliporudi akawa luteni usu wa kwanza mwanamke kuwa ofisa.

“Mafunzoni Canada tulikwenda wanne, niliyefanikiwa kurudi mapema ni mimi. Sasa kutoka hapo kwa kweli nilikuwa ninafungua milango kwa wanawake wengine katika vyeo vyote hadi usajenti na ujenerali, kwa sababu baada ya kuwa luteni usu wa kwanza na nikawa meja wa kwanza, nikaendelea hivyo hadi nikawa meja jenerali,” anasema na kuongeza:

“Cheo cha kwanza kwa kila hatua ilikuwa si rahisi. Ilikuwa ni shida kidogo kwa sababu kama unavyosema unapokuwa wa kwanza au katika kitu chochote hata katika familia ya watoto wanakuangalia wewe unafanya nini, unajichukuaje, unaongeaje na wao wenyewe unawachukuliaje, unawashauri nini, sasa hiyo pia ilikuwa ni changamoto.”

Pia anasema haikuwa changamoto kwake kwa sababu jeshini kuna taratibu zake na kuna sheria zake zilizomsaidia kuwabeba wenzangu wengine.

Anasema alikuwa anafuata hizo taratibu na sheria na baada ya hapo akaenda na wenzake wakafuata, akiwamo Meja Jenerali Kodi, ambaye yuko Dodoma na walipokuwa JKT waliwashawishi kujiunga JWTZ na sasa ana cheo hicho.

Anaposema alipojiunga na jeshi alikuwa bado hajaolewa na sasa hivi hafahamu taratibu zikoje.

“Nakwambia nimestaafu mwaka 2008, kwa hiyo ni kitambo kidogo, muda huo sisi tunaingia jeshini mwanamke alikuwa hawezi kuolewa hadi awe ametumikia miaka sita ndipo anaolewa,” anasema na kuongeza:

“Sababu kubwa kwa kweli ni yale mazingira na maumbile, lazima tukubali kwamba mama ndiye mzazi, ndiye mlezi, ndiye hiki, ndiye hiki, sasa ukimfanya aolewe mapema anaanza kubeba mzigo wa nyumba mapema, kwa hiyo mzigo wa jeshi unaweza ukamshinda.

“Kwa hiyo unamwacha kwanza miaka sita afanye kozi zake, baadhi ya kozi afurahie jeshi. Kwa sababu ukiwa peke yako unaweza kwenda Tabora, unaweza kwenda Mara, hauhitaji ruhusa, unaweza kwenda Songea, unaweza ukapelekwa popote, kwa kweli unalifurahia jeshi na maisha yake.”

Anasema yeye aliolewa akiwa na umri wa miaka 33 na hakuona kama amechelewa, kwa sababu alikuwa na malengo mengine ya kifamilia yaliyomchelewesha.

“Kwa sababu unajua mimi ni mtoto wa kwanza katika familia ya mzee Madawili. Kwa hiyo kulikuwa na wadogo zangu ambao ilibidi niwavute kidogo wakue, waweze angalau kujitegemea na wengine wawavute tena wengine,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo nilikuwa na malengo pia ya kifamilia, kwa hiyo sikuona shida, kwa hiyo wazazi wakaniambia unajua sasa muda huu unajua unachelewa. Nikawajibu ninachelewa kwenda wapi, nikawaambia hapana, wao walitaka mjukuu mapema. Niliwaambia kwamba ngoja nifanye malengo niliyoyaweka halafu baada ya hapo mjukuu atakuja, haina shida.

“Baada ya hapo niliwapelekea mwanajeshi baada ya kuingia jeshini, basi tukafunga ndoa. Kuhusu kupiga saluti kwenye nyumba inategemea nani ni mwandamizi kipindi hicho. Kwa hiyo aliye mwandamizi alikuwa anapigiwa saluti na mwenzie. Kipindi nilipoolewa kwa kweli mume wangu alikuwa mwandamizi.

“Tulipokuja kuachana hapa mwishoni, mimi nikaja kuwa meja jenerali naye alikuwa bado brigedia jenerali. Nilipanda cheo, mume wangu tulipokuwa kazini ndiyo saluti, lakini unapokuwa nyumbani kama mama unatakiwa kutenganisha majukumu yako. Unasema sasa mimi ni mama, mimi ni mke niko nyumbani, kwa hiyo unatimiza majukumu yako, unashika nafasi yako, kwa hiyo unamwacha baba naye anashika majukumu yake.”

Anasema saluti na mambo ya kazi yake yaliishia kazini na akifika nyumbani anakuwa mama.

Kuhusu malezi ya watoto, anasema yana vitu vingi, na kwa kuwa yeye ni mwanajeshi hawezi kufanya vitu vya kijeshi kwa watoto, lakini inamsaidia, kwa sababu anaweza akaongea bila shida kuliko watu wengine na anaweza kuwaambia ni nini anataka.

Anasema watoto wanakuwa wanajua kwamba mama akisema hapana ni hapana na baba akisema  hapana ni hapana kweli.

Pia anasema walijitahidi kuwafanya watoto wao waweze kusimama wenyewe, bila ya kutegemea upande wowote kama baba ana hiki na mama ana hiki na mara nyingi walikuwa wanasema vitu wanavyoviona ni vya baba na mama. 

Katika hatua nyingine, anasema wakati wanaingia jeshini misheni hazikuwa nyingi lakini walishiriki hasa wakati wa Vita ya Kagera ambako walipigana kumkabili aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amini. “Labda nirudi nyuma, baada ya kuingia jeshini tulikuta hizi ni kazi za wanawake na hizi wanawake hawawezi kufanya. Lakini baada ya kukaa kwa muda mrefu tulisema haiwezekani lazima tugeuze hii meza,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo hata wakati wa vita  wachache waliweza kwenda, walikwenda kama watu wa mawasiliano na madereva, ila tuliobaki nyuma tulifanya kazi za utawala.

“Fursa ya kipekee ninayoikumbuka jeshini ambayo nisingekuwa huko nisingeipata ni fursa ya kukimbiza Mwenge. Ile nilipata nikiwa mwanajeshi na nafikiri ningekuwa huko uraiani nisingeipata. Lakini nilipata kwa sababu nilikuwa mwanajeshi. Mwaka 1975 nilikuwa kiongozi wa mbio za Mwenge, nilikuwa nina miaka mitatu nikiwa luteni, ilikuwa ya kipekee.

“Sisi kama wanajeshi tuliletewa taarifa kwamba ninatakiwa nijiunge na kikundi cha kukimbiza Mwenge kama kiongozi, sasa nilipokwenda kuonana na wenzangu pale makao makuu ya Umoja wa Vijana nilikuta kumbe tuko wanawake watupu, kilikuwa kikosi cha watu sita.”

Anasema kama mwanajeshi hakuweza kuuliza kwa nini walikuwa wanawake watupu.

Anasema anachofurahia ni kuiona Tanzania na kuifahamu na peke yake asingeweza kufanya hivyo kwa kufunga safari na kutembea nchi nzima.

“Nilijifunza mengi kwa kweli na katika kutembea kipindi kile miundombinu ndiyo ilikuwa changamoto kubwa hasa ya barabara, wakati ule barabara nyingi zilikuwa za vumbi, zilikuwa mbaya. Kuna sehemu tulikuwa tunatembea wakati wa mvua, sehemu zingine unakuta magari yanakwama, magari yanageuka yalikotoka lakini ndizo changamoto hizo,” anasema.

965 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!