Mpendwa msomaji, Heri ya Mwaka Mpya 2017. Leo nimeona niandike mada inayohusiana na maisha. Nafahamu kuwa mwezi uliopita ulikuwa wa mapigo. Kwa wenzangu na mimi wanaofanya biashara za kubangaiza, umekuwa mwezi mgumu kuliko maelezo. 

Mwezi huu ndiyo usiseme. Kwa watu wengi kodi za nyumba zinaisha. Ada za watoto ziko mlangoni, na hakuna pa kupata mkopo.

Benki nyigi zimesitisha ukopeshaji. Baa nyingi zimefungwa. Baadhi ya hoteli zimegeuzwa hosteli. Wafanyakazi waliokuwa wanajenga kwa posho nyumba zimeishia madirishani. Shule za sekondari za St. zilizokuwa na ada kubwa zimekimbiwa na wanafunzi. Kinababa wengi kwa sasa wanawahi kurejea nyumba na familia nyingi ugomvi wa ulevi na ‘nyumba ndogo’ umepungua.

Madereva na wenye mabasi waliokuwa na jeuri ya kupandisha nauli Desemba iliyopita wameipata! Mashirika ya ndege yaliyokuwa yanaongezea wasafiri nauli bila kuwaheshimu sasa yanapumulia mashine. Kazi imeanza kupata tena heshima. Wapiga dili wanalia na kusaga meno. Takwimu za kiuchumi zinaonesha hali mbaya hadi kwa wakulima.

Sitanii, kuku waliokuwa wanauzwa Sh 6,500 sasa wanauzwa Sh 4,500. Eneo kama Banana, Dar es Salaam mambo yamechacha. Vibanda vingi vilivyokuwa vinatozwa kodi ya pango hadi Sh 800,000 sasa vimefungwa. Baa za kutosha zimefungwa kwa kukosa wateja. Hali haiko tofauti na mikoani. Kila mahala ukienda kilio ni ukosefu wa fedha.

Wakati hayo yakiendelea na shutuma nyingi zikielekezwa kwa Rais John Magufuli, ipo kada inayosherehekea. Usafiri wa anga unaimarika nchini. Tanzania sasa inazo ndege tatu, na kufikia mwaka 2018 itakuwa na ndege saba. Kati ya ndege hizi itakuwapo Dreamliner ambayo ni toleo la juu la ndege za kampuni ya Boeing.

Serikali imefanya uwekezaji wa maana na hakika mashirika kama Fastjet na Precision Air kwa sasa tunaheshimiana. Mteja amegeuka mfalme. Kwa kutumia ndege za ATCL mtu sasa anaweza kusafiri Dar-Bukoba-Dar kwa gharama ya Sh 490,000, ikilinganishwa na Sh 950,000 iliyokuwa inatozwa awali. Tumevunwa vya kutosha. Wahusika walikuwa hawaheshimu tena sheria za kimataifa.

Sitanii, ilikuwa ukichelewa kidogo tu, ndege unaisoma namba. Hakuna cha kulipishwa faini au adhabu ya kuchelewa, bali unapoteza nauli yote. Mizigo hatukuruhusiwa kusafiri hata na begi la kilo mbili. Leo ATCL inaheshimu kanuni za usafiri, watu wanasafiri na mabegi ya familia kwa raha zao. Hongera Rais John Pombe Magufuli kwa mageuzi haya katika usafiri wa anga.

Kwa upande wa watu wenye nyenzo za uzalishaji, maisha kwao sasa ni rahisi kuliko wakati wowote. Rais Magufuli amedhibiti bidhaa hewa na feki. Kwa sasa watu wenye viwanda vya kutengeneza pipi wanazalisha mara tatu hadi tano ya kiwango walichokuwa wanazalisha awali. Kama kuna mtu ana kiwanda cha karatasi, chuma au chochote tatizo sasa ni kutosheleza ukubwa wa soko.

Sitanii, najua tumelalamika mno. Kila kona tunasema maisha ni magumu. Sidhani kama tunapaswa kuendelea kulia. Sherehe sasa zimekwisha, turejee kazini. Kama kuna mtu alikuwa anafanya kazi saa 8 sasa naafanye kazi saa 12. Ikiwa kuna mtu hakuwa na shughuli yoyote, wakati wa kuwaza mipango ya kipato halali mbadala ni huu.

Kuendelea kukaa chini na kulia, ukiuza kila mali uliyokuwa nayo huku ukidai Rais amebana fedha, si suluhisho. Watanzania tuamke. Tuchangamshe ubongo na kutafuta fedha. Anachokifanya Rais Magufuli kitukumbushe kilichotokea wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa. Ukosefu wa fedha ulibatizwa na kutiwa “Ukapa”.

Hata hivyo, tunakumbuka yaliyotendeka. Mfumko wa bei ulishuka, jambo ambalo tayari nimeanza kuliona chini ya uongozi wa Rais Magufuli. Hii inamaanisha nini. Kuna watu walikuwa wanauza viwanja kwa ‘kuropoka’ tu. Hatua 15 kwa 17, anakwamba Sh milioni 8. Leo wenye viwanja wanabembeleza. Hata aliye na kiwanja anasita kukiuza.

Sitanii, naomba kuwashauri Watanzania wenzangu. Miaka minne ijayo sioni maisha yakipungua makali ikiwa hufanyi kazi. Hata hivyo, naiona neema kwa watu watakaoamua kufanya kazi halali kwa kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo na vya kati kwa maana ya kuongeza thamani ya bidhaa ambayo ingeuzwa kama malighafi. 

Rais Magufuli ameahidi kujenga viwanda. Mwaka wa 2017 tujipange kwa uwekezaji katika viwanda. Kivipi? Timiza wajibu wako.

1919 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!