Sababu ya Ukoloni  Mamboleo ni hiyo hiyo: ni kulinda  mirija ya wakubwa. Na madhali mirija ya wakubwa inalindwa, wakubwa wataendelea kutajirika na nyinyi waswahili mtaendelea kuwa masikini. Hivyo ndiyo sababu ya kwanza ya unyonjaji.

Sababu ya pili ni ile ambayo ningependa kuiita sheria ambayo nimepata kuitaja wakati mwingine nayo ni ile ambayo ningependa kuiita sheria ya mito na bahari. Ipo sheria ya mito na bahari kwamba mazingira yake yalivyotengezewa maji lazima yatoke mtoni yaingie baharini! Hata ule mto ulioko Ugogo lazima maji yake yaende baharini. Mto  ukipenda au usipende maji ya mto yatakuja tu! Bahari haiwezi ikasema haya maji ya Ugogo nayo yanakuja hapa, sikubali maji ya Ugogo!   

Kwa hiyo maji ya mito mikubwa kama vile Nile, na ya mito midogo, na ya vijito vyote yanakwenda, huko huko baharini. Si hiyari ya mto wala si hiyari ya bahari, bali ni mazingira yake yalivyotengezewa. Maji yakipatikana na mahali popote yatavutwa tu yaende baharini isipokuwa kama mkiyaziba kwa nguvu; lakini mkiyaacha yatakwenda kwa sheria yake.

Sasa, Waheshimiwa, ipo sheria hii vilevile kwa uchumi. Mali ya masikini lazima iende kwa tajiri. Masikini akipenda asipende itakwenda! Na tajiri  si lazima awe mnyonyaji, hata kidogo: na wala si lazima awe ana nia mbaya. Bali yeye ni kama bahari. Hawezi akasema hata mali ya Tanzania nayo inakuja kwangu, hii na irudi. Hawezi! Itakwenda tu kwa tajiri na itakwenda kwa sheria ile ile kama ya maji.

Nitaeleza sababu zake baada kidogo. Inasemekana mambo haya ni magumu sana kuelewa, lakini kwa kweli si magumu sana; ni mepesi angalau kujua yalivyo. Kujua sababu zake kunataka wataalamu, lakini kujua yalivyo si jambo la jabu sana madhali mtu ana jicho la kuona. Jambo muhimu ni bei ya vitu. Mnafahamu ya kuwa vitu vyao, na sisi masikini tunavyo vyetu, ingawa masikini. Basi bei ya vitu vinatengenezwa na matajiri inapanda wakati wote. Sitaki miniulize kwa nini; mimi najua hivyo ndivyo ilivyo. Kaa mwenyewe ufikirie bei ya trekta  mwaka 1959 ilikuwa nini? Na sasa, baada ya miaka kumi, bei ya trekta ile ile imekuwa nini. Na chukua kitu kingine chochote kinachokuja hapa kutoka kwa wakubwa; kama kiatu, kama ni kofia, kama kilemba, hata hizi rangi kina mama wanapaka midomo:  chochote kile! Utaona wakati wote kimeongezeka bei na tunakilipia zaidi sisi kuliko tulivyokuwa tunakilipa miaka kumi huko nyuma. Sisi  hapa kwetu tunataka trekta tulime; lazima tununue kwao. Kwa hiyo mwaka 1959 nilikuwa nalipa kiasi fulani leo nalipa zaidi. Kwa ajili ya kupata kitu kile kile lazima nifanye kazi kwa saa nyingi zaidi kukigharamia kuliko ilivyokuwa inanibidi nifanye miaka kumi huko nyuma. Ndiyo maana yake. Kama ni trekta la kulima, kama ni lori la kusomba vitu, au ni injini ya gari la moshi, kama ni vitu vingine ambavyo wewe unavihitaji kwa lazima, basi bei ya vitu hivyo inaongezeka tu! Huwezi kusema sasa sisi bwana madhali bei ya injini zimeongezeka tutachukua bidhaa kwa punda; huwezi! Utaendelea kuyanunua mainjini hayo vile vile na huwezi kuyakataa. Huwezi kuacha kununua maroli utumie farasi; huwezi utanunua tu! Huwezi kusema lazima utanunua na bei inapanda. Wala huwezi kusema sasa tuache kununua nguo kwanza; tutashughulika na nguo baadaye. Na madhali unaendelea kununua nguo kwao, utazinunua kwa bei inayopanda. Kuna vitu vingine vingi vya namna hiyo ambavyo  mnaweza wenyewe mkatengeneza orodha yake.

 Sasa chukua vitu  vyetu. Sisi kwanza tumekwisha pata hasara. Tumenunua kitu kwao ambacho jana kilikuwa shilingi mbili leo kimekuwa shilingi tatu. Na chetu sisi kinyume chake. Jana tulikuwa tunauza shilingi moja; leo tunauza senti 60! Nitawapeni mifano miwili tu, mingine mnaweza mkaifikiria wenyewe. Kwanza mnamo mwaka 1952, 1953 au 1954, bei ya pamba ilikuwa nadhani senti sitini na mbili kwa ratili moja; leo ni senti hamasini!

Ngoja niwaeleze mambo. Kama bei ya pamba ingebaki pale pale senti sitini na mbili kwa kilo, mkulima wa pamba tayari angekuwa amepata hasara! Kwa nini? Kwa sababu thamani ya senti sitini na mbili za mwaka 1959 siyo ile ile. Senti 62 mwaka ule ziliweza kununua vitu vingi zaidi kuliko leo; thamani yake imeteremka. Mtu aliyekuwa na senti 62 kwa ratili leo, bado mkulima wa pamba angekuwa na haki ya kunung’unika! Angesema, ”Vitu vimepanda bei na mimi thamani ya pamba yangu imebaki pale pale; inakuwaje?

 Sasa haikuwa hivyo basi; hata hivyo bei haikubaki pale pale bali imeanguka mpaka kufikia senti 50! Kala nani faida hii: hili faida kapata nani? Faida kapata mnunuzi! Kama mnunuzi yule angebaki na bei ile ile ya miaka kumi nyuma, alikuwa nainunua pamba kwa bei ya ratili senti 62 na leo bado anainunua senti 62, ingekuwa bado ana nafuu, na angeshukuru. Lakini bei imeteremka kaipata.

 Sasa ungefikiria kuwa madhali bei yetu ya pamba imeteremka, na bei za nguo za waheshimiwa hawa watatuteremshia vile vile! Lakini sivyo: wanapandisha tu! Sababu ya kwanza hiyo: bei. Bei yao inapanda na yetu inateremka; kununua lazima ununue kwao na kuuza lazima uuze kwao. Ndiyo ile sheria niliyokuambia kwamba lazima yataondoka maji mtoni, yapende yasipende, lazima yaende baharini. Na ukipenda au usipende utanunua kwao na utauza kwao, basi. Hiyo ndiyo nasema ni sababu ya kwanza.

Uingeweza kusema kama hivyo ndiyo, vitu vyao vinapanda bei na vyetu vinateremka, kwa nini tusitengeneze vyetu wenyewe? Na kwa nini  tuendelee kununua vyao tu badala ya kujitengeneza vyetu wenyewe sisi hapa hapa? Tunanunua matrekata yao haya bei inaongezeka: nasi tunayachukua hayo hayo kwa nini? Kwanini tusitengeze yetu? Malori bei imeongezeka tunayachukua malori yao, kwa nini na sisi tusitengeneze yetu?  Mkipenda NUTA  , kuuliza maswali kama hayo yaulizeni, na mimi napenda muulize!

 Ziko sababu zinazotufanya tushindwe, ndipo nitakwambia iko ile sheria ya mito na bahari inayofanya maji yaende baharini yapende yasipende. Kwanza hatuna ufundi! Kuna vitu fulani hivyo kutengeneza vinataka ufundi. Hatuna. Mzanaki hana ufundi huo, waje kukusadia. Pili hatuna mataji. Vitu hivyo kuvitengeneza vinataka sana mataji! Wewe  unafikiri kiwanda cha malori ni sawa na kusuka mkeka! Na tatu ni soko. Ukiwa na kiwanda cha cha kutengeneza malori au cha kutengeneza magari- moshi, halafu uyauze wapi? Humu humu Tanzania? Utagundua kisoko chako hakitoshi! Sasa mtu anaweza kuuliza kwa nini tusiuze kwao hata na sisi? Mbona wao wanunua kwetu na sisi tusiuze kwao! Ukijaribu kuuza kwao wanakataa. Watakuzuia kuuza kwao, watakuwekea vizingiti usiweze kuuza kwao, hata kama ungeweza kutengeneza.

 Hivyo ndivyo hali inayofanya ninyi mbaki papo hapo, kwa hiyo mtaendelea kununua kwao. Nitaweleza baadaye habari za vile ambavyo tunaweza kutengeneza. Vingine manaweza kutengeneza; vingine hamuwezi kutengeneza mipaka kwanza hali yenu ibadilike! Kwa sasa mtaendelea kununua kwa bei inayopanda na mtaendelea kuuza kwao kwa  bei inayoteremka: mkipenda msipende!

 Hiyo sababu moja nimesema inayoeleza sheria ya mito na bahari. Nataka kueleza sababu nyingine ndogo inayoeleza sheria hiyo. Tukipenda tusipende, tutapata hasara tu, na wenzetu watapata faida. Kuna fedha za kufanyia biashara duniani,  waheshimiwa. Biashara za siku hizi ni za fedha. Kama unavyojua hapa ukitaka kwenda kununua muhogo sokoni, sharti uwe na hela mfukoni.  Huwezi kujiendea tu. Una jembe, sijui, umkute mwenye nyanya sokoni unampa jembe akupe nyanya. Biashara hiyo ya kubadilishana vitu ilikuwako zamani, lakini siku hizi haiwezekani; huwezi hata kuiona. Siku hizi sharti uwe na fedha, na fedha zako zikubalike.

Huwezi kujiendea na makaratasi tu, unampa mtu sokoni. Karatasi  hii ni fedha!’’ Atasema hizi karatasi si fedha; hili ni karatasi la kusokotea tumbaku! Na zile karatasi mpaka zikubalike ziitwe fedha, lazima kwa sheria ya Tanzania zijulikane kwamba ni fedha. Halafu ukimpa mtu anakubaliana nawe, ukitaka ugoro unaweza ukapata ugoro kwa karatasi hii. Na biashara ya dunia vile vile. Ukitaka kufanya biashara  ya dunia  itabidi uwe na fedha. 

 

>>INAENDELEA

By Jamhuri