Na Deodatus Balile
 
Miaka ya 1950 wakati Tanganyika inapigania Uhuru lengo kuu lilikuwa ni kukomboa watu wetu kutokana na unyanyasaji wa hali ya juu waliokuwa wanafanyiwa na Wakoloni. Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa upande wa Zanzibar dhidi ya Waarabu. Wakoloni hawa walikuwa wanatulimisha kwa faida yao binafsi. Watu wetu walilima pamba, korosho, karafuu, mbaazi, karanga, kahawa na mazao mengine ya biashara kwa faida ya mataifa yao.
Tumenyonywa mno kupitia mazao haya. Nitatumia mfano wa pamba. Kwa masikitiko makubwa sisi tunalima pamba katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita. Shati la kawaida lina uzito wa gram 200. Hii ina maana kwa chini sana kilo moja inaweza kuzalisha mashati hadi matatu, kwani kilo moja ina gram 1,000. Cha ajabu, wakati kilo moja ya pamba inauzwa Sh 1,200, shati moja linauzwa kwa chini Sh 20,000 likitoka huko tunakowauzia pamba.
Kilimo moja kama imezalisha mashati matatu, ina maana ukinunua mashati yote matatu unapaswa kulipa Sh 60,000. Kwa hiyo, ingawa kuna gharama za usindikaji, kwa maana ya kupata nyuzi, kutengeneza vitambaa na hatimaye kukata na kushona shati ukilinganisha na bei ya Sh 1,200 anayolipwa mkulima tofauti ni dunia na mbingu.
Kahawa kwa mfano, mkulima anapewa Sh 1,300. Nilikuwa London, mwaka jana, nikaenda kwenye mgahawa wa Sainsbury, niliuziwa kikombe cha kahawa paundi 1, sawa na Sh 3,200. Kijicho cha chai kina gram 1.8. Wanasema kahawa yetu haina ubora, kilo moja inatoa gram 550 za kahawa iliyosagwa. Hii ina maana kilo moja inatoa vikombe 305 vya kahawa, sawa na Sh 977,777. Mkulima anapewa 1,300.
Sitanii, leo nimeandika mada hii kwa nia ya kuamsha fikra. Wazee wetu walipigania uhuru wa kisiasa. Ni zamu yetu sasa kupigania uhuru wa kiuchumi. Ebu wewe msomaji wangu unayesoma makala hii jiulize swali kisha ukipata fursa unijibu japo kwa kunitumia jumbe mfupi. Najaribu kuorodhesha vitu vichache hapa kwa ufupi kukufikirisha.
Ukiamka asubuhi angalia kuanzia mswaki, maji unayooga, mafuta unayopaka, sabuni uliyotumia, dawa ya meno, taulo, sukari, majani ya chai au kahawa, kikombe, kisosi, kijiko cha kukorogea chai, suruali, sketi, shati au gauni ulilovaa, viatu, soksi, kitana, kioo, heleni kwa kina mama, lipstick, lotion, kitambaa cha kufutia jasho, kijiti cha kuchokonolea meno, nyama ya mbuzi, samaki, maharage, kuku au yai ulilokula asubuhi, pikipiki, gari binafisi au daladala uliyopanda.
Chakula cha mchana – ugali (unga), mboga za majani, chumvi, mchele, pilipili, kompyuta, meza, kiti, simu, kiyoyozi, pangaboi, luninga, mlango, jengo – mabati, saruji, rangi (nyumba), umeme, maji, mkaa, hapo sijataja mashuka uliyotumia, kitanda ulicholalia na vitu vingine vingi. Tafta kati ya hivyo ni kipi kimeandikwa; Made In Tanzania. Kwa siku mwanadamu kwa uchache anatumia bidhaa zaidi ya 30. Ukiacha maneno na soga unazopiga ukiwa na marafiki ni bidhaa ipi unayoizalisha ukaiuza ikakuingizia kipato wewe na familia yako kwa mwaka?
Sitanii, binafsi namshukuru Mungu nimepata fursa ya kutembelea nchi mbalimbali duniani. Nimepata fursa ya kuishi Ulaya, nimefika Amerika na Mashariki ya Mbali, hasa China. Kama kuna nadhiri tunapaswa kuiweka sisi sote kila mtu kwa wakati wake ni kujipangia kuwa na kiwanda kimoja kwa uchache, bila kujali ukubwa wa kiwanda. Angalau uzalishe kitu kimoja tu katika familia yako kiuzwe na kuiingizia familia pato. Hicho ndicho kitu kinachoitwa kiwanda.
Nilichokikuta China ni suala la pekee. Tunaposikia Wachina kuwa wameendelea, haikutokea kwa bahati mbaya. Nchi ile taifa linawezesha watu wake. Unasajili kampuni ndani ya saa 1. Nimekuwa nikiandika suala la muhogo na Mungu akipenda nitarejea tena China mwaka huu kujifunza zaidi juu ya taratibu za kulima muhogo, usindikaji wa muhogo na soko la muhogo. Nimeona siasa zimetosha. Nitaandika juu ya uwekezaji kuanzia sasa angalau nipate Watanzania 1,000 watakaoamua kuwa wawekezaji. Tukutane wiki ijayo.
4314 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!