Maadhimisho ya Siku ya Wanawake yalifikia kilele wiki iliyopita. Shamrashamra zilikuwa nyingi karibu maeneo yote ndani na nje ya nchi.

Wanaotambua na kuthamini utu wa mwanamke, kwao hadhi ya mwanamke iko palepale muda wote. Hawasubiri siku maalumu kulitambua au kulionyesha hilo.

Mkoani Geita kuna tukio lililonishawishi kuandika haya ninayoandika leo. Si jambo zuri kwa umoja na mustakabali wa mama zetu.

 

Kina mama kadhaa waliamua kuadhimisha siku yao kwa kuomba wawe wao kulingana na itikadi zao. Wapo walioomba kibali cha maandamano na mkutano wao kama wafuasi wa chama fulani cha siasa. Polisi wakawagomea.

Wakaamua kwenda kule walikoelekezwa kuwa ndiko kulikopangwa kwa ajili ya sherehe za kina mama ‘wote’. Walipofika eneo la tukio wakawakuta wenzao wakiwa kwenye sare za chama chao. Hawa waliofika mwishoni wakaketi upande wao tofauti na wale waliowakuta wakiwa wamekwisha kuketi.

 

Sherehe zikapambwa na sare za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Eneo la sherehe likawa kama jukwaa la uwanja wa mpira ambako mashabiki hutambulika kwa sare zao.

Bahati nzuri Watanzania ni watu waliolelewa kwa namna ambayo si rahisi sana kuwafananisha na watu wengi. Wanapendana, japo kuna juhudi kubwa za kuleta utengano. Kama si kupendana, hali kama hii kwenye maadhimisho ya kina mama ingeweza kusababisha vurugu kubwa.

Hulazimiki kuwa mtabiri kutambua kuwa utengano wa kiitikadi ulioonyeshwa na kina mama wa Geita ni shangwe na nderemo kwa kina baba wengi. Ni ukweli ulio wazi kwamba wanawake ni kete muhimu ya ushindi kwenye chaguzi mbalimbali za kisiasa. Wagombea wengi, hasa wanaume huwategemea zaidi wanawake kupata ushindi.

 

Wapiga kura wengi wanaojitokeza siku ya kupiga kura ni wanawake. Kwa mtiririko huo huo, wanawake wengi wanaogombea nafasi za uongozi huangushwa zaidi na wanawake wenzao. Laiti kama wanawake wangeamua kuwa wamoja, ni wazi kuwa ni wanaume wachache mno wangeshinda udiwani, uwakilishi, ubunge au hata urais.

Ni bahati mbaya sana kuwaona wanawake wakiendelea kubaguana hata kwenye sherehe za siku yao maalumu. Kitendo cha wao kushindwa kuvaa sare moja, badala yake wakaamua kujitambulisha kwa sare za vyama vyao, si dalili nzuri ya wao kujikomboa dhidi ya madhila wanayofanyiwa na baadhi ya wanaume.

 

Lakini tukio hili la Geita si la kulitazama kwa namna nyepesi kama tulivyoona. Kuna kitu kikubwa na kizito kinachotoa ujumbe wa aina ya jamii tunayoelekea kuijenga. Kuna hatari naiona. Tumeanza kuyabadili matukio ya kijamii kuwa na chembe za kibaguzi, na kwa bahati mbaya tunajidanya kwa kudhani kuwa ubaguzi wa kiitikadi si ubaguzi hatari kama zilivyo aina nyingine za ubaguzi.

Matukio ya umma yanapaswa yabebe sura ya umma. Leo tunaona mikutano ya kiserikali inayohutubiwa na viongozi wa kiserikali kwenye ziara za kiserikali ikibeba sura ya u-chama. Ni ukweli kuwa si rahisi kutenganisha mambo haya kwa kiwango tunachofikiria, lakini kuzima hisia za kuenea kwa hali hiyo ni jambo linalowezekana kwa kiongozi yeyote anayeipenda nchi hii.

Nakumbuka kuna kauli ya kijasiri ya Rais Magufuli, kwenye ziara moja alipokataa kujihusisha na masuala ya chama chake kwa maelezo kuwa ziara aliyokuwa nayo ilikuwa ya serikali, kwa hiyo masuala ya chama yasubiri ziara ya kichama. Hii ilikuwa kauli njema ingawa pamoja na kusema hivyo hapakuonekana tofauti yoyote kubwa.

 

Viongozi wa kiserikali ni viongozi wa taifa. Wanawaongoza watu wote wenye vyama na wasio na vyama vya siasa. Baadhi yao wanachaguliwa na Watanzania bila kujali itikadi zao. Kama ndivyo, ni haki kabisa shughuli za kiserikali zisifunikwe na itikadi za vyama. Kufanya hivyo ni kuwakwaza baadhi ya Watanzania waaminifu wasiopenda kufungamana na itikadi za vyama.

Kama tulidhani kufanya hivyo kuna tija, basi tulitazame tukio la kina mama wa Geita wiki iliyopita kisha tuone kama kweli huko tuendako tunakwenda sehemu salama.

 

Tunapodhamiria kuziba njia za ubaguzi, tuzibe njia zote. Tusichague. Tusipofanya hivyo tutakuwa na taifa ambalo mtu kuharibu mali ya umma anaona anaharibu mali ya ‘Wana CCM’ – kitu ambacho si kweli hata kidogo.

Viongozi wetu wanapozindua miradi ya kijamii watambue kuwa kinachotawala hapo ni umoja na utaifa wetu kama watu wamoja, maana fedha za hiyo miradi zinatoka kwa watu wa itikadi tofauti.

Mwisho, niwaombe kina mama wawe makini dhidi ya utengano kama huu wa Geita. Wanapohudhuria shughuli za wanawake, wafanye hivyo kama watu wamoja wenye malengo yanayofanana. Kujipambanua kwa sare za vyama vya siasa kwenye Siku ya Wanawake Duniani ni moja ya udhaifu wa hali ya juu utakaofanya waendelee kuwa dhaifu mbele ya wanaume. Wasidhani wanaume wanakasirika. Wajue wanafurahi sana kuona wanabaguana. Kwa kufanya hivyo, wanajua wamefanikiwa mpango wao wa ‘divide and rule.’

530 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!