SIMBA SC imeendelea kushikiria record yake ya kutokufungwa kwenye Ligi Kuu baada ya leo kuifunga Mbeya City kwa Mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unawafanya Simba wafikishe pointi 55 baada ya kucheza mechi 23, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 47 katika nafasi ya pili.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi, Hance Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Rashid Zongo wa Iringa, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 3-1.

Nyota Mganda, Emmanuel Arnold Okwi alianza kuwainua vitini mashabiki wa SImba SC dakika ya 20 baada ya kukutana na mpira uliookolewa na kipa wa Mbeya City, Mmalawi Owen Chaima kufuatia shuti la Nahodha, mshambuliaji John Raphael Bocco.
Beki Mghana, Asante Kwasi akaifungia bao la pili Simba SC dakika ya 36 akitumia bega lake kumalizia krasi ya winga Shiza Ramadhani Kichuya, bao ambalo hata hivyo lililalamikiwa na wachezaji wa Mbeya City wakidai alifunga kwa mkono.
Juhudi za Mbeya City ya kocha Mrundi, Ramadhani Nswazurimo zilizaa matunda dakika ya 37 baada ya kufanikiwa kupata bao leo pekee lililofungwa na mshambuliaji wake, Frank Ikobela aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Danny Joram.
Hata hivyo, Nahodha mshambuliaji John Raphael Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 38 akimalizia krosi ya beki Shomary Kapombe kutoka upande wa kulia.
Kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa zamu, Mbeya City wakianza vizuri dakika ya 20 za mwanzo kabla ya Simba SC ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre kutulia na kuanza kujibu mashambulizi.
Kikosi cha Simba SC Kilikuwa: Aishi Manula, Nicholas Gyan/James Kotei dk87, Asante Kwasi/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk72, Juuko Murshid, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco/Laudit Mavudo dk79 na Shiza Kichuya.
Mbeya City: Owen Chaima, Rajabu Isihaka, Majaliwa Shaaban, Ally Lundenga, Haruna Shamte, Eliud Ambokile, Danny Joram/Mohammed Samatta dk61, Victor Hangaya/Geoffrey Muller dk76, Baab Ally Seif na Frank Ikobela.

By Jamhuri