DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Simba wameanzisha harambee ya kujenga uwanja wao. Tayari wana kiwanja cha kufanyia mazoezi, lakini hawana kiwanja cha kuchezea mechi.

Harambee iko moto mitandaoni. Mashabiki na wanachama wanachanga walichonacho katika utaratibu wa kutuma pesa uliowekwa na Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez na Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu. 

Watu wamehamasika, wanachanga kwa kasi kubwa. Pia kwa kiasi kikubwa. Ndiyo. Hili ni jambo jema na kubwa, japo lina changamoto zake, lakini kama watu wakiamua linawezekana. 

Uwanja wa Benjamin Mkapa umejengwa kwa zaidi ya Sh bilioni 100. Fedha ambazo Simba wanazo mpaka sasa ni Sh bilioni 2 zilizoahidiwa na Mohamed ‘Mo’ Dewji.

Timu zetu kubwa nchini si maskini kama tunavyoziona. Zina utajiri mkubwa, hasa wa rasilimali watu. Idadi kubwa ya watu ndio utajiri wenyewe. Muda mrefu timu zetu zimeshindwa kuwageuza wafuasi wao kuwa fedha. 

Hii ni tofauti na klabu kama vile Al Ahly na wababe wengine wa soka la Afrika. Wakubwa wengine wa Afrika wana mashabiki/wanachama wengi, lakini pia ni timu tajiri. Wamefanikiwa kuwageuza wafuasi wao kuwa fedha. 

Kuna sehemu ya moyo wangu inaniambia hili suala la Simba linawezekana. Kumbuka ilivyoanza safari ya Bunju Arena. Ilikuwa safari yenye kiza kinene, hatimaye sasa Simba wameshapata sehemu ya kufanyia mazoezi. 

Mwanzo wa uwanja wa Bunju ilikuwa dharau, vicheko, kebehi, watu wakiambiwa wakafyeke. Mpaka sasa tunapowaona Simba wanafanya mazoezi yao pale, inaonyesha kuwa hata hili la kutaka kuwa na kiwanja chao LINAWEZEKANA.

Siku hizi Simba wakikodi kiwanja ili kufanyia mazoezi ni uamuzi wao tu, lakini wana sehemu ya kufanyia mazoezi. Hii ni sehemu pia ya kuchezea mechi za majaribio. Baadhi ya mechi za aina hiyo wanazichezea pale pale Bunju Arena. 

Lakini mwanzo wa wazo la Bunju Arena lilipuuzwa kama linavyopuuzwa hili wazo la sasa la kujenga uwanja mkubwa wa mechi za mashindano. Ilionekana ni kama stori, lakini mwisho kabisa imekuja kuwezekana. Inataka moyo kuwaambia watu pale kiwanja cha Bunju Arena kuwa kulikuwa pori. 

Waanzilishi wa Bunju Arena wamegonga mihuri ya moto katika vifua vya Wanasimba. Hata hatua hili walilokuja nalo kina Mangungu na Barbara litawafanya wakumbukwe kama wanavyokumbukwa kina Hassan Dalali, Mwina Kaduguda, Ezekiel Kamwaga na wengineo waliokuja na mpango mahiri ulioacha alama Msimbazi.

Hata mpango huu ukikamilika na kina Barbara wakiwa si sehemu ya uongozi, haitaacha kufanya wasikumbukwe kwa vizazi vijavyo vya Simba. Watakumbukwa tu kwa uthubutu huu.

Kitendo cha kufikia kuwa na wazo la kiwanja ni moja ya mafanikio ya Simba. Hizi ni ndoto kubwa zinazolipiwa mabilioni ya fedha na matajiri. 

Wakosoaji huwa hawakosekani. Simba ndio waanzilishi wa harakati nyingi za kimaendeleo katika soka la Tanzania. Sijui kama wakosoaji wanalijua hili!

Ni Simba walioanzisha masuala ya kuwa na siku maalumu ya kuitambulisha timu, wachezaji na jezi mpya, wakaiita ‘Simba Day’. 

Hizi ni sherehe zinazokuja siku chache kabla ya kuanza kwa msimu mpya. Siku hizi kila timu ina tamasha lake lenye sura kama ya Simba Day. 

Ni Simba walioamua kwenda katika mfumo mpya wa kiuendeshaji. Hivi karibuni tumeziona timu mbalimbali zikifuata mfumo huu. 

Hivi karibuni pia tumeona Simba wakija na mabegi ambayo kuna timu nazo zimeiga, lakini wao wakiboresha kwa kuweka herufi ya jina la mchezaji na namba yake pembeni mwa begi. 

Mfano ni jina la Jonas Mkude. Wao wanaweka JM 20. Simba huwa inaanzisha vitu vingi vinavyoanza kubezwa kisha baadaye watu wanafuata. Hata hili la kiwanja nalo litaigwa tu.

344 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!