Macho, masikio kwa Polepole

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

Miongoni mwa makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioitwa kujieleza mbele ya kikao cha Halmashauri Kuu, jina la Humphrey Polepole limegonga vichwa vya watu wengi.

Pamoja na kwamba Askofu Josephat Gwajima na Jerry Slaa nao waliitwa, Polepole anatazamwa kama mtu atakayewaokoa wenzake wasifukuzwe ndani ya chama.

Akizungumza baada ya kumalizika kikao hicho, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, anasema chama kimebaini upungufu wa kutotimia kwa masharti ya uanachama wao.

Upungufu wa Polepole, Mbunge wa Kuteuliwa na kijana aliyewahi kushika nafasi ya uenezi unatokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ukosoaji wa wazi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Ukosoaji huo amekuwa akiufanya kupitia kipindi cha shule ya uongozi kinachorushwa kupitia TV ya mtandaoni; ‘Humphrey Polepole Online TV’.

Kwa upande wa Gwajima, Mbunge wa Kawe, dosari za uanachama wake ni kuonekana kwenda kinyume cha  msimamo wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kuhusu chanjo ya corona.

Gwajima amekuwa akitumia kanisa lake kuhamasisha wananchi kutochanjwa, akidai kwamba chanjo haijathibitishwa kama kweli ni kinga dhidi ya corona.

Msimamo huo ni kinyume cha ule wa serikali, ambapo yenyewe imeweka wazi kuwa watu watachanjwa kwa hiari.

Kinachomponza Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa na kuuweka uanachama wake rehani, ni tuhuma za kudanganya Watanzania na Bunge.

Akiwa bungeni, Silaa amewahi kutamka wazi kwamba mishahara ya wabunge haikatwi kodi, hali ambayo ilizua mtafaruku nchini.

Baada ya kikao kubaini dosari, wanachama na wafuatiliaji wa siasa wanatega masikio wakisubiri hatima za makada hao.

Wapo wanaoamini kuwa kwa misimamo ya Gwajima na Polepole huenda watu hawa wakabwaga manyanga mapema pasipo kusubiri hukumu ya Kamati Kuu ya CCM.

Msimamo wa Polepole ndio unasubiriwa kwa hamu zaidi baada ya kuelezwa uanachama wake una dosari.

Wapo wanaoamini kauli zake na kuamini kuwa huenda amejitoa kukitetea kile anachokiamini na kwamba yuko tayari kufukuzwa ubunge na uanachama ili mradi dhamiri inayomsukuma kufanya anayoyafanya itimie.

Ni ukweli kuwa jina lake ni gumzo nchini, hali inayoibua mgawanyiko kwa wananchi, baadhi wakiamini kuwa asipodhibitiwa atakisambaratisha chama.

Tayari ameanza kudhibitiwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusema kipindi chake kinakiuka maadili ya kitaaluma.

Wapo wenye imani kwamba kusimamishwa kwa shule ya uongozi kunalenga kumnyamazisha kwani hoja ambazo amekuwa akitoa kupitia kipindi hicho ni vigumu wahusika kuzitolea ufafanuzi.

Kwa mujibu wa TCRA, Polepole hakufuata sheria, msingi na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari na leseni yake.

Wengine wanamuona Polepole kama shujaa ambaye ameamua kuwakosoa viongozi wakiwamo wa chama chake.

Wanaoamini hivyo wamejikita kwenye hoja ambazo nyingi Polepole huzijenga akilenga kuonyesha upungufu wa kiuongozi anaouona kwa sasa nchini.

Inaaminika kuwa Polepole hakubaliani na mambo mengi ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inayafanya.

Wenye mtazamo kama huo wanaona hatua iliyochukuliwa na TCRA kuwa ya kiungwana na kustahili kupongezwa.

Hoja hiyo inapingwa na upande mwingine, ukidai kuwa kusimamisha kipindi hicho ni mwendelezo wa kuwanyima watu uhuru wa kujieleza na kuminya vyombo vya habari.

Wapo waliofurahishwa na taarifa za kufungwa kwa kipindi hicho wanaodai madhumuni yake hayakuwa ya kizalendo, bali kililenga kuichafua Serikali ya Rais Samia.

Wengine wanadai kuna watu wapo nyuma ya kipindi hicho ambao humtumia Polepole kufanikisha malengo dhidi ya serikali.

Watu hao wanadhaniwa kuwa kwenye mtandao wa wanaomchukia Rais Samia ambao hawakupenda yeye kukalia kiti hicho na kuiongoza Tanzania.

Zimekuwapo hisia mseto juu ya msimamo aliouonyesha Polepole ambapo baadhi wanaamini ana hasira ya kushushwa cheo.

Wapo wanaodhani kuwa huenda Polepole amekumbwa na sononeko baada ya kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu wakidai alikuwa karibu naye na alimuamini sana.

Wenye fikra hizo wanadhani kuwa anayoyafanya Polepole yanatokana na kupoteza nafasi muhimu ambazo kupitia kwa rais huyo angepata kwa siku za mbeleni.

Kwa upande mwingine wapo wanaoamni kuwa Polepole ana taarifa muhimu za chama na kwamba yote anayofanya anatafuta sababu ili akiguswa au kuchukuliwa hatua iwe rahisi kwake kuziweka wazi.

Katika moja ya kauli zake Polepole zinazothibitisha kwamba anaweza kuwa na mengi ni ya kusema kwamba Rais Magufuli hakufanikiwa kumaliza tatizo la wahuni serikalini na ndani ya chama.

Kauli hiyo imeungwa mkono huku pia ikipata wapinzani wa waziwazi.

Wapo wanaomtuhumu pasipo kuweka ushahidi kuwa alishiriki kwenye sakata la kununua viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kwa kigezo cha kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Mashambulizi dhidi ya Polepole kutokana na kauli hiyo yaliendelea ambapo siku chache baadaye chumba chake anachoishi jijini Dodoma kilivunjwa na vitu kusambaratishwa.

Tukio hilo lilitafsiriwa kama hatua ya kumuonyesha kuwa anaopambana nao wana nguvu na muda wowote wanaweza kumpata wakimtaka.

Msimamo wa Polepole umemuibua Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, ambapo kupitia ukrasa wake wa twitter amekuwa akirusha vijembe ambavyo watu huvitafsiri kama vinaelekezwa kwa Polepole.

Baada ya Nnauye kurusha vijembe hivyo, wapo wanaotafsiri kitendo hicho kama kinyongo alichonacho dhidi ya Polepole kutokana nafasi ya katibu mwenezi ndani ya chama ambayo wote wamewahi kuitumikia.

Mwingine ni Abdallah Bulembo, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi, ambapo alimtahadharisha Polepole kuacha kukosoa jitihada za Rais Samia katika kufungua fursa za ushirikiano wa kimataifa.