Singasinga ‘anyooka’

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi, ikiwamo kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani  22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Watu wa karibu wa Harbinder Singh wameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba ‘huruma’ ya Rais Magufuli imekuja wakati mfanyabiashara huyo akiwa ameshahangaika kuona namna ya kujinusuru katika tuhuma zinazomkabili. 

Chanzo chetu kinasema, Singh yuko tayari kurejesha mali zote alizonunua kwa kutumia fedha alizozipata kutokana na ‘skendo’ ya Tegeta Escrow. Sehemu ya mali hizo ni pamoja na majumba ya kifahari yaliyoko nchini Afrika Kusini, mashamba yaliyoko Iringa, mtambo wa kufua umeme wa IPTL ulioleta kasheshe yote hii, pamoja na ndege ya kisasa Bombardier Challenger 350 inayodaiwa aliinunua kwa dola milioni 28. 

“Unajua Harbinder Singh alishaanza kufikiri namna ya kurejesha mali alizonunua kutokana na fedha ya Escrow… jambo hili si dogo kwake, unajua amekaa ndani kwa zaidi ya miaka miwili sasa, suala ambalo hakuwahi kuliwaza maishani mwake. Kutoka kulala hoteli ya bei yoyote duniani uitakayo ukaenda kulala sakafuni Segerea, si jambo la mchezo.

 “Ukizungumza naye unaona kabisa utayari wa kurejesha mali hizo ambazo kwa kweli ni za gharama kubwa, mfano hiyo Bombardier Challenger 350 inauzwa kwa zaidi ya dola za Marekani milioni 28, hapo hujaweka mtambo wa IPTL wala nyumba zake za kupangisha zilizoko Johannesburg na Pretoria nchini Afrika Kusini,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimesema pamoja na kufikiria hayo, umekuwapo mkanganyiko baina ya wawili hao ambao wanashitakiwa pamoja, hasa kutokana na ukweli kwamba James Rugemalira anataka suala lao liende hadi mwisho na mahakama itoe hukumu. 

“Unajua mzee (Rugemalira) anataka suala hili liendelee hadi mwisho na kupata suluhu ya mahakama. Wakati Singh alitaka kutubu na maisha mengine yaendelee. Alimwelewa Rais Magufuli vizuri, naye kwa hakika anataka arudi kushirikiana na Watanzania kujenga uchumi,” amesema mtoa habari wetu. 

Singh ambaye ni mtuhumiwa mkuu katika sakata la Escrow iwapo atafanikiwa kurejesha fedha hizo, basi atakuwa mtu wa tano kati ya ama walioonyesha nia au waliorejesha fedha. Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alikuwa wa kwanza kukabidhi fedha hizo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akisema alipewa na Rugemalira kama sehemu ya kumsaidia jimboni mwake.

Maaskofu wawili, Method Kilaini na Eusebius Nzigilwa nao walirejesha serikalini mgawo waliopewa na Rugemalira wakisema walizipokea kama msaada ila kwa kuwa zimethibitika kuwa na shida, basi wanazikabidhi serikalini hadi mvutano uishe. 

Katika hatua nyingine, kuna taarifa mbaya kwa watu waliopokea mgawo wa fedha za Rugemalira. Chanzo cha uhakika kimeliambia JAMHURI kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaandaa utaratibu wa kuwadai kodi wote waliopokea fedha kutoka kwa Rugemalira. 

“Unajua sheria za nchi hii ziko wazi. Zinasema kila fedha unayopata unapaswa kuilipia kodi. Sasa tumeangalia kwenye orodha na tukaangalia kila namba ya mlipakodi (TIN) za hawa waliopokea fedha, tukabaini kuwa hawakulipa kodi. 

“Sasa pamoja na kwamba Rugemalira na Singh walidaiwa wakalipa sehemu ya mapato yao, hata hawa waliopokea kuanzia Sh milioni 40 hadi Sh bilioni 1.6, walistahili kulipa kodi. Tunawasiliana na mamlaka nyingine za dola vikiwamo vyombo vya uchunguzi kama TAKUKURU, na majalada yameanza kuandaliwa kwa watakaokataa kulipa kodi bila kusubiri kusukumwa.

“Hapa tunachotaka ni haki itendeke kwa kila mtu. Wafanyakazi wanaopokea Sh 300,000 wanalipa SDL, wanalipa PAYE, lakini mtu anapokea Sh milioni 40 au bilioni 1.6, asilipe hata senti moja, haiwezekani. Hii inaweza kuwavunja moyo wafanyabiashara wanaolipa kodi, tena wakati mwingine kwa kukopa wadeni wao wakichelewa kuwalipa,” kimesema chanzo chetu kutoka TRA.

Alipoulizwa ni utaratibu upi utatumika kuwadai, akasema: “Tumepanga kuwapelekea barua kila mmoja kama ilivyo kwa mujibu wa sheria kumtaka aje alipe. Kwa kuwa hawa hawana biashara za kufunga, basi tunaandaa majalada. Kwa watakaokaidi, mtawaona Kisutu mahakamani. Ukamataji utaanza si muda mrefu.”

Mmoja wa wanufaika wa mgawo huo amezungumza na JAMHURI (jina linahifadhiwa) akasema: “Muda wote nilipoona wamekamatwa Rugemalira na Singh, nilijua hili litatokea. Nimesikia hizo fununu kuwa tutadaiwa kodi. Sasa hii ndiyo kasheshe. Mimi kwa kweli niliishazitumia zimeisha. Milioni 40 haidumu. Na sasa sina chanzo chochote cha mapato, biashara zangu zimekufa… nafahamu Rais [John] Magufuli hatanii. Najiandaa kisaikolojia kuishi gerezani Segerea maana sina jinsi.”

  

Tibaijuka ‘arejesha fedha ya mboga’

Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (69), wiki iliyopita tumeandika katika gazeti hili kuwa yuko tayari kurejesha Sh bilioni 1.6 alizopewa na James Rugemalira ili zimsaidie mfanyabiashara huyo atoke rumande.

Profesa Tibaijuka alikuwa miongoni mwa wanufaika wa mabilioni ya shilingi ‘yaliyomwagwa’ na Rugemalira aliyezipata kutoka kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta mwishoni mwa utawala wa Awamu ya Nne.

Kitendo cha Profesa Tibaijuka kuwekewa kwenye akaunti kiasi hicho cha fedha kilimfanya atenguliwe nafasi yake ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. 

Sasa anasema yuko tayari kurejesha fedha hizo ili zimsaidie Rugemalira endapo atataka kulipa na kuomba radhi ili atolewe rumande ambako amedumu kwa miaka zaidi ya miwili. 

“Ni clear (wazi) kwamba sisi kama shule sasa ni wakati mwafaka kurejesha fedha hizo zote zimsaidie mfadhili wetu Rugemalira kurejesha ili awe huru kama akiamua kukiri na kuomba radhi,” amesema Profesa Tibaijuka.

 Wiki mbili zilizopita Rais John Magufuli ‘alimshauri’ Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) akubaliane na watuhumiwa wa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ili walio tayari kurejesha fedha na kuomba radhi wafanye hivyo na hatimaye waachiwe huru. 

Rugemalira, mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, pamoja na Harbinder Singh, wako rumande wakikabiliwa na mashitaka ya rushwa na utakatishaji fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 20; na fedha za Tanzania zaidi ya Sh bilioni 300. 

Profesa Tibaijuka anajitetea kuhusu fedha hizo akisema: “…Usione tu dili, wengine tunajenga nchi. Tunaelimisha watoto. It requires resources na tunawashukuru waliotuchangia kama ndugu yangu Rugemalira na marehemu [Reginald] Mengi.” 

Profesa Tibaijuka amezungumza na JAMHURI akiwa New York, Marekani, na kusema: “Wakati niko huku najua Bodi ya Shule [Barbro Johansson] imekaa chini ya Mwenyekiti wake mzee Solomon Odunga na Mwenyekiti wa Parents Teachers Association, Dk. John Kyaruzi na kuamua fedha zirejeshwe kumsaidia mfadhili wetu, James Rugemalira kuachiwa.

“Tulisubiri mahakama iamue kama fedha zake ni haramu au halali. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Rais ametangaza amnesty [msamaha] tunaona ni wakati mwafaka kurejesha fedha hizo ambazo tulikaa nazo kwa sababu Rais Kikwete alisema James alipewa fedha hizo kihalali, kwani aliuza share [hisa] zake za IPTL.

“Sasa kama mchakato wa kimahakama umeshindikana na rais kwa hekima na huruma yake akatoa amnesty, hapo unarejesha fedha zimsaidie mtuhumiwa kukidhi masharti yaliyowekwa.  Huo pia ndio msimamo wangu binafsi. Nashukuru na bodi ya shule imeliona hilo. Namuombea ndugu yangu atoke salama.”

Ameongeza: “Hata bungeni nilisemea jambo hili la justice delayed is justice denied [Haki inayocheleweshwa ni haki iliyokoseshwa]. Ni wazi kwamba sisi kama shule sasa ni wakati mwafaka kurejesha fedha hizo zote zimsaidie mfadhili wetu Rugemalira …nchi itajengwa na wenye moyo. Watoto wahitaji wataendelea kuwapo. Tutaendelea kuwasaidia kupata elimu bora tutakavyoweza. Anayeshindwa kuona juhudi hizo na kuona ‘dili’, namuacha kama alivyo. Mungu atubariki na kutuongoza. Ampe Rais wetu hekima ya Mfalme Suleiman,” amesema Profesa Tibaijuka.

 

Wakubwa waliopokea mamilioni

Taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilionyesha orodha ya baadhi ya vigogo waliogawiwa mamilioni ya fedha kupitia akaunti ya Rugemalira katika Benki ya Mkombozi, Dar es Salaam.

 Katika orodha hiyo, pamoja na Tibaijuka ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wengine ni; watumishi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA); mawaziri wa zamani – Andrew Chenge, William Ngeleja na Daniel Yona; na majaji Profesa Eudes Ruhangisa na Jaji Aloysius Mujulizi.

Walipokea kati ya Sh milioni 40.2 hadi Sh bilioni 1.6. Chenge, Profesa Tibaijuka na Kyabukoba & Associate walipokea Sh bilioni 1.6 kila mmoja, huku Jaji Ruhangisa akipokea Sh milioni 404.2. Mfanyakazi wa Ardhi, na Rugonzibwa Theophil yeye alipokea Sh milioni 232.4.

 Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa RITA kwa wakati huo, Philip Saliboko aliyeteuliwa kuwa Mfilisi wa IPTL, aliingiziwa Sh milioni 40.2 kwenye akaunti yake. JAMHURI ilipowasiliana naye, alikiri kupokea fedha hizo, ila akasema ameangukia katika mkumbo.

 “Kaka mimi ni kweli, nilipokea fedha hizo, ila nimekuwa victim of the circumstance (mhanga wa mazingira). Nilinunua shamba kule Malela – Mkuranga karibu na Vikindu lenye ukubwa wa ekari 50 na jingine lenye ukubwa wa ekari 20.

“Mjomba wake Rugemalira akataka nimuuzie moja ya mashamba yangu hayo ya Vikindu. Nilimwambia nitamuuzia ekari 20 kwa Sh milioni 65. Alinilipa cash Sh milioni 5 nikabaki ninamdai Sh milioni 60. Baadaye akaniambia nifungue akaunti Benki ya Mkombozi mjomba wake atamsaidia kulipa deni hilo.

“Nikafungua akaunti, nikakuta ameniingizia Sh milioni 40 tu, kimsingi ikawa bado namdai. Sasa nikasikia kuwa fedha nilizolipwa zimetokana na hili suala la IPTL, nilisononeka. Sikushiriki kwa njia yoyote na wala sikuwa nikilipwa fadhila kwa njia yoyote,” alisema Saliboko.

Kwa upande wake, Jaji Ruhangisa aliyechotewa Sh milioni 404 alikaririwa akisema kuwa fedha hizo alipewa kwa masuala ya kifamilia kama sherehe, harusi na misiba.

Profesa Tibaijuka alisema fedha hizo alipewa ili kuendeleza shule zake.

Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilimkariri Katibu wa Rais, Prosper Mbena (wakati huo), akielekeza utoaji fedha ufanywe kama ilivyoshauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). AG wa wakati huo alikuwa Jaji Frederick Werema. 

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) [kwa wakati huo] alimtaja Mnikulu Gurumo kuwamo kwenye mgawo, akisema kuwa alipata Sh milioni 800.

Awamu moja ya ugawaji fedha hizo inaonyesha kuwa Rugemalira aligawa Sh 3,314,850,000 kwa siku moja. 

Majina ya waliopewa fedha na Rugemalira na kiwango kikiwa kwenye mabano ni Evelyn Rugemalira (Sh 808,500,000), Alice Kemilembe Marco (Sh 80,850,000), Rashid Abdallah (Sh 80,850,000, Annuciater C. Bula (Sh 40,425,000), Laureaan R. Malauri (Sh 40,425,000), Theophillo Bwakea (Sh 161,700,000), Jesca James Rugemalira (Sh 808,500,000), na Steven Roman Urassa (Sh 161,700,000). 

Wengine ni Michael Muhanuzi Lugaiya (Sh 80,850,000), Eric Sikujua Ng’maryo (Sh 80,850,000), Lucas Kusima Simon (Sh 40,425,000), Jerome Mushumbusi (Sh 808,500,000), Loicy Jeconia Appollo (Sh 80,850,000), Rweyongeza Alfred (Sh 40,425,000), Gaudence Talemwa (Sh 40,425,000) na Manzelline aliyepewa Sh 80,850,000.

Watu maarufu kwenye mgawo huo kwa wakati huo ni Balozi wa Heshima wa Botswana hapa nchini, Emmanuel ole Naiko (Sh 40,425,000), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh bilioni 1.6), Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh 40,425,000), Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja (Sh 40,425,000), Waziri wa zamani na aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Katiba, Paul Kimiti (Sh 40,425,000), Mchungaji Alphonce Twimann (Sh 40,425,000), Askofu Method Kilaini (Sh 80, 850,000) na Askofu Eusebius Nzigirwa aliyepata Sh 40,425,000.

Majaji wawili – Aloysius Mujulizi (Sh milioni 40.4) na Profesa Eudes Ruhangisa (Sh milioni 404.2). Pia wamo Mtendaji Mkuu wa RITA.

 

Sakata lilivyokuwa

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa bungeni iliwaanika aliyekuwa AG Werema na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.

CAG alifanya ukaguzi maalumu wa miamala (transaction) iliyofanyika katika akaunti ya ‘Escrow’ ya Tegeta pamoja na umiliki wa Kampuni ya IPTL. 

Takukuru baada ya kufanya uchunguzi ilikuta akaunti ya Kampuni ya VIP Engineering and Marketing iliyopo katika Benki ya Mkombozi jijini Dar es Salaam iliyopokea fedha kutoka BoT, ndiyo ilitumika kusambaza fedha hizo. 

Baada ya hukumu iliyotolewa na Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumaliza mgogoro kati ya Kampuni ya VIP inayomilikiwa na Rugemalira na Mechmar ya Malaysia, mgogoro mpya ulianza serikalini. 

Mgogoro huu ulihusu uhalali wa fedha hizo kulipwa au la, na hapo ndipo yalianza mashinikizo ya aina yake kutoka kwa watendaji na baadhi ya viongozi wa kisiasa.

 

Maswi akataa malipo yasitolewe

Taarifa ya CAG iliyowasilishwa bungeni inaonyesha kuwa Kampuni ya PAP baada ya kuwa wamepata hukumu Septemba 5, 2013 walipeleka maombi Wizara ya Nishati na Madini wakitaka serikali iwalipe fedha kwa kigezo kwamba walikuwa wamiliki halali wa fedha na mali za IPTL. 

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alikataa kuidhinisha malipo. Baada ya mvutano mkali, aliandika barua akiomba ushauri wa kisheria kwa AG Jaji Werema. 

Kupitia barua yenye Kumb. Na. CBR.88/147/29 ya Septemba 16, 2013; Maswi alimwandikia AG akipinga malipo hayo kwa hoja mbili: 

Hoja ya kwanza, alisema haamini kama fedha zote zilizokuwa katika akaunti ya Escrow zilikuwa za PAP kwa vile ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana na mgogoro wa tozo za ‘capacity charge’ ambazo ni gharama za uwekezaji kati ya TANESCO na IPTL. Akasema umiliki halisi wa fedha hizo ungefahamika pale tu mgogoro huo utakapotatuliwa. 

Hoja ya pili, asisisitiza hoja ya kwanza kuwa PAP anastahili kupata malipo ya kiasi kitakacholipwa kwa IPTL baada ya mgogoro huo kutatuliwa na si kiasi chote kilichokuwa kwenye akaunti ya Escrow. Alihitimisha kwa kuagiza pande zinazohusika kukaa na kukokotoa stahiki ya TANESCO na IPTL. 

Taarifa ya CAG ilisema Sepemba 26, 2013 Maswi alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, yenye Kumb. Na. CDB.88/417/31 kutaka kiitishwe kikao cha pamoja kujadili suala la malipo hayo. 

Kikao hicho kilifanyika Sepemba 24 na kuhudhuriwa na maofisa wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, BoT na TANESCO. Kikao kiliunda kamati ndogo ya kufuatilia suala hilo na kuazimia kuwa IPTL na TANESCO wamalize mgogoro wao kwanza ndipo malipo yafanyike.

Ikumbukwe mgogoro uliomalizwa Septemba 5 na Jaji Utamwa, ulikuwa kati ya VIP Engineering na Mechmar waliokuwa wakigombea malipo ndani ya IPTL, hivyo Maswi alikuwa akisema mgogoro kati ya TANESCO na IPTL uliowasukuma kufungua Escrow ulikuwa bado upo hai, hivyo fedha haziwezi kutolewa. 

Baada ya msimamo mkali wa Maswi, Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Likwelile, Gavana wa BoT, Profesa Ndulu na AG Werema waliendelea kuwasiliana wao kwa wao hadi malipo yakafanywa.

 

Werema aagiza PAP walipwe

Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile aliamua kuanza kuwasiliana na AG Jaji Werema na kumwacha kando Maswi. 

Sepemba 30, 2013 Dk. Likwelile alimwandikia Jaji Werema barua yenye Kumb. Na. CAC/184/211/01/23 iliyojibiwa na Jaji Werema kupitia barua yenye Kumb. Na. AGCC/E.80/6/65 ya Oktoba 2, 2013. 

Ripoti inasema: “Alimwarifu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile kuwa ameipitia ripoti husika na kwamba jambo pekee linaloweza kuleta tatizo ni kuhusu fedha zilizowekezwa na Benki Kuu katika hati fungani. 

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishauri kuwa fedha hizo zilipwe kwa IPTL ili jambo hilo lifungwe na kuiwezesha serikali kujiepusha na mashauri yasiyo na tija kwake, na kusisitiza kuwa uamuzi wowote wa kutoa fedha kwenye akaunti ya Escrow unalindwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania (Jaji Utamwa) ya tarehe 5, Sepemba, 2013.”

 

Kasi ya Gavana kulipa

Gavana Ndulu, Novemba 25, 2013 aliandika barua kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Singh Sethi na Novemba 28, 2013 Sethi akafungua akaunti katika Benki ya Stanbic, kisha tarehe hiyo hiyo akaijulisha BoT taarifa za akaunti aliyoifungua na tarehe hiyo hiyo mabilioni yakalipwa. 

“Baada ya BoT kupokea maelekezo ya Bw. Harbinder Singh Sethi, malipo ya kwanza ya kiasi cha Sh 8,020,522,330 na US$ 22,198,544 yalifanyika Novemba 28, 2013 katika akaunti za PAP zilizofunguliwa katika Benki ya Stanbic. 

“Baada ya malipo hayo kufanyika, umiliki wa hati fungani zenye thamani ya Sh 157,622,910,000 ikijumuisha mtaji (principle amount) wa Sh 146,567,363,967 na riba ya Sh 11,055,546,033 ulihamishwa kwenda PAP Desemba 6, 2013,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

 

Werema aagiza kodi isilipwe

Baada ya uamuzi wa Mahakama, TRA ilidai kodi, lakini ikagonga mwamba. “Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia barua Kumb. Na. AGCC/E.080/6/70 ya tarehe 18, Novemba alimfahamisha Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu kuwa hakukuwa na kodi ya VAT katika fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow, hivyo kutokuwepo kwa kodi iliyopaswa kukusanywa. 

“Hata hivyo, katika mahojiano tuliyofanya na Kamishna Mkuu wa Kodi, alithibitisha kuwa TRA wanaendelea na hatua za kuikusanya kodi husika kutoka IPTL,” inasema taarifa ya CAG.

Taarifa hiyo imebaini udanganyifu wa hali ya juu, ambapo wakati Piper Link ilinunua hisa 7 au asilimia 70 ya hisa kutoka kwa IPTL kwa gharama ya dola milioni 6 (karibu Sh bilioni 10 kwa wakati huo), baadhi ya watumishi katika TRA walishiriki udanganyifu na kuonyesha kuwa hisa hizo ziliuzwa kwa Sh milioni 6.

Kampuni ya Piper Link nayo iliuza hisa hizo 7 siku hiyo hiyo iliyozinunua kwa Kampuni ya PAP kwa gharama ya dola milioni 20 (karibu Sh bilioni 36), lakini kwa udanganyifu wa hali ya juu maofisa wa TRA wakaonyesha kuwa PAP ilinunua hisa hizo kwa dola 300,000 (sawa na Sh milioni 480). Ni kwa njia hiyo, serikali ilipoteza kodi.

JAMHURI lilipowasiliana na AG Jaji Werema (wakati huo) kupata maelezo yake juu ya ripoti hii ya ukaguzi na kumjulisha kuwa zipo taarifa alihongwa dola milioni 5 kufanya uamuzi huu; alijibu kwa Kiingereza na katika tafsiri isiyo rasmi alisema: 

“Unayaamini hayo kwa chembe yoyote? Ikiwa unayaamini, basi nitakie safari njema ya kuondokana na umaskini. Ikiwa huyaamini, basi sikitika kama nifanyavyo.” 

Baada ya kuhoji kwanini atajwe yeye, alisema wapo watu waliojipanga kumharibia jina na anafahamu jinsi wanavyopokea au wanavyoomba kupokea rushwa ya magari na fedha tasilimu, lakini wanataka sasa kuhamishia mpira kwa watu wengine. 

Mwisho wa mazungumzo, akasema: “Umetaka maelezo yangu. Bunge linapaswa kujizuia kujadili IPTL kwani masuala yanayoibuliwa ni masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama. Kuna kesi nne katika Mahakama ya Biashara. 

“Ukaguzi wa akaunti ya IPTL ni suala la kawaida, lakini uhalali (kisheria) wa kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow ni suala linalosubiri mashitaka mahakamani. 

“Ni dharau kwa Mahakama kuifanyia mzaha. Hata nje ya Tanzania, SCB ina kesi katika uhamishaji (wa fedha). Naomba tupigane vita katika uwanja sahihi. Bunge si moja ya viwanja hivyo, ambako sheria ya asili hutawala, na ambako mbilikimo na mapandikizi ya watu hawakutawazwa kutoa haki,” amesema Jaji Werema. 

Mataifa yanayounda Umoja wa Wahisani yalizuia misaada kwa Tanzania yakitoa masharti kuwa Tanzania ijadili na kutolea uamuzi suala la kashfa ya IPTL kwanza, na wahusika wachukuliwe hatua ndipo waruhusu misaada.

Hata hivyo, ukiacha hatua chache za kutikisa kiberiti ambapo Rugemalira na Singh walilipa kodi kiasi, waliogawiwa mamilioni ya fedha hizo hawakuguswa wala kuchukuliwa hatua yoyote.