Ardhi Temeke kikwazo

Zaidi ya kesi 100 za migogoro ya ardhi zimekwama kutolewa hukumu katika Baraza la Ardhi Wilaya ya Temeke kwa sababu ya kukosa printer na vifaa vingine muhimu.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, mmoja wa walalamikaji hao, Aidan Amon, ambaye ni miongoni mwa waliocheleweshewa hati za hukumu za kesi zao, amesema kesi yake Namba 17 ambayo aliipeleka katika Baraza hilo la Ardhi 11/10/2018 ilikuwa ni ugomvi wa mipaka yeye na jirani yake, ambapo kwa sasa imefikia hatua ya hukumu lakini bado hajapata hukumu hiyo kutokana na changamoto hiyo.

Amesema kadhia hiyo inawakumba wengi na kwamba hayuko peke yake. Amon amesema wamekuwa wakipigwa danadana tu na ofisi hiyo kwa madai ya kwamba printer ni mbovu hazifanyi kazi, kwa hiyo wasubiri mpaka itakapokuwa imepona ndipo wawape hukumu zao, ambapo hawajui ni lini na muda unakwenda.

Amesisitiza kuwa yeye na wenzake wanachohofia mpaka sasa ni muda wa kesi zao kusubiri hukumu kwa ajili ya rufaa  kuwa mrefu.

“Mwenendo uliopo katika Baraza hili la Ardhi unaonyesha dhahiri watu wengi tutapoteza haki zetu, hasa sisi wenye kusubiri hukumu na rufaa tutakuwa tumepoteza haki zetu, kwani wengi wetu tuna kesi ambazo muda wake wa hukumu au rufaa siku zimekwisha kutokana na  kesi hizo kuwa nje ya muda wa siku 60,” amesema Amon.

Ameiomba serikali na mamlaka husika kuangalia umuhimu wa baraza hilo kuboreshewa mazingira ya kufanya kazi ili kesi hizo kwisha haraka, kwani mahakama hizo zimebeba  jukumu kubwa la kujishughulisha na jamii katika suala la ardhi.

Baada ya taarifa hizo Gazeti la JAMHURI lilifika katika baraza hilo ili kujionea hali halisi na kukuta vifaa vingi vikiwa chakavu na vingine vimeharibika.

Mwandishi wetu ameshuhudia jinsi mafaili mengi yaliyokuwa tayari kutolewa uamuzi na baraza hilo yakiwa yamerundikana.

Mmoja wa watumishi wa mahakama hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, amekiri kwamba wanacholalamika wananchi ni sawa kabisa, lakini anachojua kuna changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi.

“Nadhani kuna uzembe, maana taarifa zimekuwa zikitolewa kwenye mamlaka husika ila hakuna kinachofanyika. Labda kwa kuwa ninyi mmekuja mkiandika na wakubwa wakaona watachukua hatua,” kimesema chanzo chetu.