Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za nishati na miundombinu kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais Samia amebainisha kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji ili kurahisisha biashara na usafirishaji wa bidhaa.

Amesema takribani asilimia 70 ya mizigo ya Rwanda hupitia katika bandari za Tanzania, huku wastani wa tani milioni 1.6 za shehena ukisafirishwa kila mwaka, jambo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha miundombinu hiyo.

Katika sekta ya nishati, Rais Samia ameeleza kuwa kuna mradi wa pamoja wa uzalishaji umeme wa maji katika Maporomoko ya Rusumo unaoshirikisha pia Burundi, ambapo umeme wa megawati 80 unazalishwa.

Amesema hatua zimechukuliwa kuuzindua rasmi mradi huo pamoja na kuanza utekelezaji wa makubaliano ya kuuziana umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na shirika la umeme la Rwanda.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara katika mataifa hayo mawili.

Ziara ya Rais Kagame imeendelea kufungua fursa mpya za ushirikiano katika sekta mbalimbali, hususan nishati na miundombinu, ambazo ni nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi wa kisasa.