Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Bi. Rukia Zuberi, ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya viongozi pamoja na wataalamu ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.
Alitoa wito huo alipotembelea kata zilizopata athari za mvua kubwa, akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya wilaya, kwa lengo la kujionea hali halisi na kuchukua hatua stahiki za kulinda maisha ya watu na mali zao.
“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo yanayotolewa na viongozi pamoja na wataalamu ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema Mkuu wa Wilaya hiyo.
Kutokana na mvua hizo, hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu, isipokuwa uharibifu mdogo wa baadhi ya mashamba ya wananchi katika maeneo yaliyoathirika.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari kufuatia uwepo wa mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku ikiwataka kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.




