Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam
Miili miwili ya watu, mwanaume na mwanamke, imeokolewa katika matukio mawili tofauti jijini Dar es Salaam baada ya kupatikana ikiwa inaelea juu ya maji katika maeneo ya Salenda.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 4, 2026, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Mabusi Peter, amesema tukio la kwanza lilitokea jana katika eneo la Stakishari, ambapo walipokea taarifa ya mtu kuonekana akielea majini.
Amesema Kikosi cha Zimamoto kilifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kuutoa mwili wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 60 uliokuwa ndani ya mto.
“Baada ya kuufikia mwili huo, tulitekeleza jukumu la uokoaji na kisha kuukabidhi kwa vyombo husika kwa ajili ya uchunguzi zaidi kubaini chanzo cha kifo,” amesema Mabusi.
Katika tukio la pili lililotokea leo majira ya saa tano asubuhi, Jeshi hilo lilipokea taarifa ya kuwepo kwa mwili wa kijana mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 20 ukiwa unaelea juu ya maji katika eneo la Daraja la Salenda.
Mabusi amesema kikosi kilifika eneo hilo na kuutoa mwili huo kisha kuukabidhi kwa mamlaka nyingine kwa ajili ya uchunguzi wa kina.
Amesisitiza kuwa jukumu la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni kufanya uokoaji, huku hatua za uchunguzi zikifanywa na taasisi nyingine ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.Uchunguzi wa matukio hayo unaendelea.


