M

atukio ya ujambazi wa kutumia silaha, mauaji ya polisi na viongozi wa vijiji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, yanahusishwa na vikundi vya vijana wanaopata mafunzo kutoka kwenye kundi la al-Shabaab nchini Somalia, JAMHURI limefahamishwa.

Kwa miaka minne hadi mitano iliyopita, vijana kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Rufiji, hasa Ikwiriri, wamekuwa wakisajiliwa na kundi hilo la kigaidi, huku wazazi wao wakiambulia ujira wa dola 3,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 6).

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wakazi wa Ikwiriri ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini kwa sababu za kiusalama, amesema kumekuwa na wimbi la vijana wenye umri wa miaka 16-25 kupelekwa kwenye mafunzo huko Somalia.

“Hapa Ikwiriri katika kipindi cha miaka kama mitano iliyopita kumekuwa na wimbi la vijana wadogo kupelekwa Somalia. Inasemekana wanakwenda kujiunga na kikundi cha al-Shabaab, lakini vijana hao wamekuwa wanapatikana kupitia kwa mawakala kadhaa kwenye misikiti.

“Si kweli kwamba polisi hapa Ikwiriri hawajui, maana hata ukifuatilia wale viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakitoa taarifa za vijana hao wamekuwa wakiuawa kwa staili inayofanana… sasa hapo unaweza kuona namna zoezi linavyokuwa gumu,” amesema.

Chanzo chetu kingine kimemtaja mtu ambaye jina lake tunalifupisha kwa kifupi kama S.B., kuwa ndiye hufanya kazi ya udalali wa kuwapeleka vijana hao nchini Somalia, huku wazazi wa watoto hao wakiambiwa kuna kazi wanakwenda kuifanya huko.

Chanzo hicho kimesema hata baada ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji kupeleka taarifa za uhusika wa S.B. kilichofuata ni mauaji.

“S.B. alipotea hapa Ikwiriri kwa takribani miaka mitatu, hata baada ya kurejea amekuwa na mali nyingi. Mali ambazo si za kurithi na haziendani na utafutaji wa halali katika kipindi hicho kifupi. Yamekuwa yanasemwa mengi, lakini ukimgusa andaa sanda kabisa,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo chetu kimeliambia JAMHURI kuwa vijana zaidi ya 27 kutoka maeneo mbalimbali wilayani Rufiji, wamechukuliwa kwenda kujiunga na al-Shabaab, chini ya udalali wa Bwana S.B.

Chanzo hicho kimesema mmoja na vijana ambaye alichukuliwa alishindwa aina ya kazi na akarudi.

Habari ambazo JAMHURI, limezipata zinaonesha kwamba kikundi hicho cha wauaji kimekuwa kikimtumia mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka 18, kuwapelekea chakula huko msituni eneo la Mparange wilayani Rufiji. Jina la mtoto huyo tunahifadhiwa kwa sababu za kitaaluma.

“Kijana huyo mdogo amekuwa akitumiwa na hao wauaji kuwapelekea chakula. Mtoto huyo amekuwa akiwahudumia pasipokuwa na simu. Akikamatwa huyo anaweza kusaidia sana upelelezi wa polisi… hapa kila mtu amejaa hofu kuhusu usalama,” kimesema chanzo chetu.

 

Ushauri

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya usalama waliozungumza na JAMHURI wametoa ushauri kwa Serikali wa namna ya kukabiliana na wimbi la mauaji ya viongozi na polisi yanayoendelea Mkuranga, Kibiti na Rufuji mkoani Pwani.

Serikali inashauri wa kuwahusisha viongozi wa dini na wataalam wa saikolojia katika kutatua vitendo hivyo.

Akizungumza na JAMHURI, mchambuzi wa masuala ya usalama mwenye makazi yake Johannesburg, Afrika Kusini, ambaye kwa maudhui ya kiusalama tunamtambulisha kwa jina moja la Alexandre, anasema sehemu kubwa ya Afrika Mashariki inakabiliwa na matatizo ya usalama, hivyo njia pekee ya kukabiliana na tatizo hilo ni kuzihusisha pande zote.

Alexandre, anasema kumekuwapo tatizo linalohusishwa na vitendo vya ujambazi (ugaidi) katika Pwani ya Bahari ya Hindi, ukanda wa Mombasa, Tanga, Zanzibar, Mtwara, Lindi na Dar es Salaam.

“Ninashauri kwamba mamlaka; hasa vyombo vya usalama visifikirie kuhusu ‘confrontation’ na vikundi hivyo…Polisi wanapowaua, hao ‘majambazi’ nao wanahakikisha wanalipa kisasi. Katika mambo kama hayo ni busara wanasaikolojia pamoja na viongozi wa dini wakaingilia kati.

“Wanasaikolojia wanatakiwa kufanya utafiti, kwanini matukio kama hayo yamekuwa yanajirudia katika eneo hilo hilo katika siku za hivi karibuni? Hapo inawezakana kukawa na jambo kubwa zaidi…” amesema.

 

Hali ilivyo Mkuranga, Kibiti na Rufiji

Hali ya usalama katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji imezidi kuwa ya wasiwasi, huku vyombo vya usalama vikiweka zuio katika maeneo hayo.

Baadhi ya mazuio hayo ni marufuku ya kuendesha pikipiki kuanzia saa 12:00 jioni, wananchi hasa maeneo ya Ikwiriri wilayani Rufiji wamekuwa wakitakiwa kulala mapema.

Akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando, anasema hali si nzuri kutokana na ukweli kwamba wananchi hata yeye mwenyewe wako katika sintofahamu ya kiusalama.

JAMHURI: Mheshimiwa Pole kwa yanayotokea jimboni kwako

UNGANDO: Asante sana kaka, nimeshapoa!

JAMHURI: Unaweza kuzungumzia kuhusu hali ya usalama jimboni kwako?

UNGANDO: Yaani katika hili, naomba nisiwe mzungumzaji maana mwenyewe niko katika ‘danger zone’ viongozi wangu wa vijiji wanauawa, huoni kwamba anayefuata hapo ni mimi? Nisingependa kulizungumzia hata kidogo, unanitafutia balaa, sitaki kuongea kwenye vyombo vya habari, maana nikiongea utaandika kwenye magazeti, na hao wenzetu (wauaji) wanasoma. Hapa mimi nasubiri hatma yangu kaka!

JAMHURI: Umeshapata ujumbe wowote kutoka kwa wauaji?

UNGANDO: Hata kama nimepata ujumbe siwezi kusema maana hali ya usalama imekuwa tishio kwangu na wananchi wenzangu. Jitihada za pamoja zinahitajika katika kutatua tatizo hili, si kazi ya mbunge pekee.

Wakati Mbunge wa Kibiti, akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, yeye amesema hawezi kuzungumzia jambo hilo, badala yake anasubiri uchunguzi wa vyombo vya dola ukamilike.

 

Tukio la Kibiti

Tukio la wiki iliyopita, limechukua uhai wa polisi wanane. Nao ni Inspekta Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis, F.6990 PC Haruna, G.3247 PC Jackson, H.5503 PC Siwale, H.1872 PC Zacharia, H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.

Mauaji hayo ni mwendelezo wa matukio mengine saba ya aina hiyo yaliyotokea katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja mkoani Pwani.

 

Tukio la kuuawa kwa askari wanane limetokea ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia baibui.

Wanaume hao ambao walikuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vizuizi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika Daraja la Mkapa.

Februari mwaka huu, watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji Mapato ya Ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi/mgambo ambao walipigwa risasi na walikufa papo hapo eneo la tukio.

Mei, mwaka jana Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa kwa risasi.

Oktoba, mwaka jana Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho, Ally Milandu, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne. Novemba, mwaka huo huo wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, mwaka huu watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu walimuua mfanyabiashara Oswald Mrope kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, mwaka huu watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kutoroka.

Matukio ya aina hii yanayotia shaka ustawi wa amani ya Tanzania, kwa mwaka 2013 yalitokea wilayani Kilindi mkoani Tanga ambako msikiti wa Madina ulibainika katikati ya pori kati ya Tanga na Bagamoyo.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2014 vijana waliokuwa wakipewa mafunzo ya kigaidi walikamatwa mkoani Mtwara wakiwa wanapewa mafunzo tayari kujiunga na al-Shabab.

Kenya kwa muda mrefu sasa imekuwa katika mapambano yasiyokwisha na kundi la al-Shabaab wanaoaminika kuwa wanatetea imani na Waislam nchini Somalia.

Ni kwa mantiki hiyo, matukio ya mauaji kwa mikoa ya Pwani, Mtwara na Lindi wachambuzi wa masuala ya kiusalama wameishauri Serikali kutumia zaidi diplomasia kuliko nguvu.

8080 Total Views 1 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!