Sisi Waafrika weusi tukoje? (4)

Nchini mwetu, licha ya kilio cha Baba wa Taifa kuacha ufahari na matumizi ya magari makubwa, lakini ukienda Mbezi Beach, au Jangwani Beach, au hata hapo Oysterbay, mtu unashangazwa na mijumba mikubwa ya watumishi wa umma yanavyoumuka kama uyoga vile.

Juu ya usafiri, sasa barabara za Dar es Salaam hazipitiki kwa wingi wa magari ya mikopo. Kinachosikitisha sana ni magari ya Serikali yenye ukubwa na ufahari wa kutisha. Mashangingi ya “air condition” si kwa mawaziri tu, bali hadi kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi na hata wafanyabiashara. Nchi za Kiafrika zina ugonjwa mkubwa wa matumizi mabaya.

 

Matumizi ya kifahari namna hii kwa Kiingereza tunasema “conspicuous consumption” yaani MATANUZI! Swali hapa, hivi kweli Ilala, Kinondoni au Temeke panahitajika gari Land Cruiser 4×4 shangingi kwa barabara hizi za lami?

 

Mji kama Liwale, Namtumbo, Nanyumbu, Kibondo, Nkasi kweli nyakati za mvua magari hayo yanahitajika. Tukoje Waafrika weusi sisi na ugonjwa wa ufahari?

 

Hii inadhihirisha viongozi Waafrika walidai Uhuru si kuwasaidia watu wao waendelee, bali viongozi hao wenyewe walidai ili kunyakua madaraka na kujinufaisha na rafiki, jamaa na koo zao. Kuukana Uafrika, kuachana na ushamba wa bara jeusi hili na kujigeuza kuwa Wazungu weusi ndiyo yalikuwa malengo yao.

 

Hata wageni walioleta dini za Ukristo na Uislamu wakaona ni mahali pa kuendeleza mila zao za kigeni kwa kutupatia majina ya kigeni, mathalani ukiitwa Majaliwa au Kazibeni au Muhanje sasa ukiingia tu Ukristo utapewa jina la Kizungu kama vile John au Joseph au Damian. Ukisilimu tu utaitwa Issa au Mohamed au Juma na hivyo umeachana kabisa na “ushenzi” wa Kiafrika. Sasa umekuwa au Mzungu au Mwasia (mweusi).

 

Hadi hapo nimejaribu kuelezea Waafrika weusi tunavyosujudu Uzungu na Uarabu kimila – majina, ufahari, anasa na kimavazi, lakini hakuna aliyeiga ile tabia nzuri ya UCHAPAKAZI na mila ya uzalishaji kwa kuinua uchumi kwa kila mtu au kwa Taifa zima. Sisi ni mafundi wa usambazaji mali za kutoka nje kama wafanyavyo hawa wamachinga katika miji yetu humu nchini. (We are good distributors but not producers). Kamwe hatujishulishi na uzalishaji wa bidhaa nchini mwetu.

 

Umaskini unatuganda licha ya kuvaa vizuri na kuishi katika majumba ya kifahari. Neno hili UMASKINI wengi tunalitafsiri kuwa ni ukosefu wa fedha tu. Mtu hana fedha za kununulia mahitaji yake muhimu kama chakula, mavazi na mahali pa kujihifadhi (malazi bora), basi huyo ni maskini! Moja ya sababu za umaskini wetu Waafrika inasemekana ni viongozi wa Kiafrika kushindwa kusimamia utendaji kazi wetu na kutokujithamini wenyewe kwa wenyewe.

 

Hii tabia ya kuleana ukoo mzima inayoitwa “extended family” tumefuga ndugu wengi wasio na kazi katika nyumba zetu sisi viongozi. Basi, kila kiongozi anatumia fursa yake kiwadhifa kuwatafutia kazi katika ofisi mbalimbali ndugu, jamaa na rafiki zake au watu wa makabila yao. Kwa njia hii wanaoajiriwa huwa hawana sifa kwa kazi waliyopatiwa. Hapa kazi katika viwanda au ofisini itapungua kifaida maana haifanywi kitaalamu na wenye ujuzi.

 

Sababu nyingine iliyoelezwa na Mhandisi Bundara (katika kitabu chake Waafrika Ndivyo Walivyo uk. 27-29) ni ile ya viongozi kusaidia kuhamisha rasilimali kutoka kwenye nchi zetu kupeleka ng’ambo. Kutokana na mtindo namna hiyo, viongozi wa nchi mbalimbali wanajipatia kamisheni kutoka kwa wageni husika na ndipo wanaweza kuwa na vijisenti mabenki ya nje – ughaibuni.

 

Viongozi namna hii wameweza pia kuwa na majumba zaidi ya moja, kuwa na magari zaidi ya moja na kuishi maisha ya kifahari ilhali wananchi wakulima au makabwela wanazidi kuwa hoi kwa vile fedha za mikopo kwa maendeleo ya Taifa zina wanufaisha zaidi walioko madarakani.

 

Kila Taifa la Kiafrika huwa lina madeni makubwa na yasiyolipika katika nchi. Kunakuwa na matabaka katika nchi – wale walionacho wananeemeka zaidi na wale wasiokuwa nacho ndiyo wanazidi kudidimia. Hali namna hii ndiyo inayoleta chanzo cha uhasama miongoni mwa raia wa nchi moja. Ufukara unaongezeka na hali ya umaskini kwa Waafrika inakua.

 

Jambo au sababu nyingine ya kukosa maendeleo kwa Waafrika weusi ni utendaji kazi wetu. Waafrika wengi wana kisomo kizuri kweli na waliobahatika kupata kazi Ulaya au Marekani au hata nje ya nchi zao za kuzaliwa, wanachapa kazi nzuri sana na kusifiwa kwa utaalamu wao. Lakini vipi hatukuiga tabia ile nzuri ya Wazungu waliotutawala ya kuchapa kazi kwenye viwanda, kwenye mashamba makubwa kama ya mkonge, kwenye migodi uzalishaji umedorora sana? Uaminifu katika kazi umepunguka sana. Rushwa imeshamiri na uwajibikaji haupo kabisa. Kazi zile zile akiletwa afisa Mzungu kusimamia, uzalishaji unaongezeka, inakuwaje?

 

Wajapani wakati wanajenga barabara ile ya Mnazi Mmoja hadi Mtwara, ndugu zangu Wamakonde wengi walifukuzwa kazi kwa utoro kazini. Imezoeleka kutoa sababu kama “shangazi anaumwa”, “mjomba kafariki”, “binamu anaolewa”, “bibi anaumwa” na kadhalika. Kila walipoulizwa kwanini hukuja kazini walitoa majibu namna hiyo. Basi Wajapani waliwatimua. Haya ni mazoea yale yale ya kutega kazi ili kuvuna tusichopanda yanayozorotesha kazi za uzalishaji katika nchi zetu.

 

Makaburu kule Afrika Kusini hawana utamaduni wa wafanyakazi wao kukosa kazi eti shangazi, mjomba au kaka amefariki na kuwa mazikoni. Misiba yote kule kiutamaduni wao inashughulikiwa wikendi tu – Jumamosi au Jumapili. Kwa Mswahili hapo analalamika eti huo ni ubaguzi na kutokujali mila na desturi za wananchi! Réne Dumont ametoa hata mfano wa uchapaji kazi maofisini kati ya Mzungu na Mwafrika kwa maneno haya, namnukuu; “A typist for the Dakar Government types an average of six to seven pages double spaced, a day less than a quarter of what an average French typist accomplishes for a salary that is equal if not higher” (False Start in Africa uk. 82). Hapa anaonesha uwajibikaji wa mtumishi Mzungu ukilinganishwa na Mwafrika.

 

Hapa kwetu maofisini muda mrefu unatumika kupiga stori za mitaani, mipira ya Yanga na Simba au wanauza maandazi/chapati au nguo/viatu maofisini saa za kazi, na hivyo kuathiri sana uzalishaji maofisini kwa ucheleweshaji wa nyaraka.

 

Nchi zote za Dunia ya Kwanza za Ulaya, Marekani, Japan na kwingineko, watu wanahesabu uzalishaji kwa saa zinazotumika kufanya kazi “man hours”, hivyo, kazi inathaminiwa kimuda wa saa itakayochukua kukamilika na wala si suala la kufika ofisini kusaini kitabu cha mahudhurio kisha kukaa au kuondoka. Huo ni unyonyaji. Kazi inafanyika kwa muda uliopimiwa katika nchi za wenzetu ughaibuni.

 

Itaendelea