Siku zote napenda kufuatilia siasa za Tanzania. Ni siasa hizi za kuchafuana. Siasa za kuchafuana si ngeni katika jamii yetu. Mtu akimwona mwenzake kazidi kwa jambo jema katika jambo fulani, basi atamchafua ili jina lake lionekane kuwa si kitu.

Mume atamwona mwanamme mwingine ni maarufu zaidi kuliko yeye. Atahisi atapendwa na mkewe. Kwa hiyo, atamwambia mkewe, “Huyu fulani ambaye inaonekana anakuvutia hafai. Kwanza nimesikia kuwa ni mwizi” hata kama hajasikia!

Kwa muda mrefu sasa tumemsikia Samwel Sitta (pichani kulia), Mbunge wa Urambo Mashariki na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akiendelea kumsema vibaya Edward Lowassa (pichani kushoto), Waziri Mkuu aliyejiuzulu mwaka 2008, kutokana na sakata la Richmond.

Binafsi sina uhusiano wa aina yeyote na Lowassa zaidi ya kuwa yeye na mimi ni Watanzania. Lakini nimechoshwa na tabia hii ya Sitta kumsema vibaya kila uchao. Anaonekana ana uhasama naye usio wa kawaida.

Sitta anamwona Lowassa kuwa ni fisadi wa kutisha. Ushahidi wa Sitta ni Lowassa anavyochangia fedha nyingi makanisani na misikitini. Sitta anataka Lowassa aeleze fedha hizi anapata wapi. Na kama ni kweli ni marafiki zake wanaochangia basi awataje wote kuthibitisha kwamba yeye si fisadi. Sitta hajathibitisha kuwa Lowassa hana marafiki.

Nadhani sikosei nikisema kwamba utajiri wa Lowassa ulipata kumshangaza hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mwaka 1995 Lowassa alikodi ndege kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma wakati wa mchakato wa kumtafuta rais wa Tanzania. Mwalimu Nyerere alishangaa kuona kijana wa wakati ule akikodi ndege.

Hiyo ni karibu miaka 20 iliyopita. Lakini kuanzia wakati huo hatujasikia kuwa Lowassa amekamatwa kwa kuiba fedha benki au kwa kuuza dawa za kulevya.

Lakini Sitta haachi kushikilia kuwa fedha za Lowassa ni chafu. Anayataka makanisa yakatae fedha za Lowassa. Anaona kuwa ni fedha za mtu anayenunua watu katika maandalizi yake ya uchaguzi wa rais mwaka 2015.

Cha kushangaza hata Sitta mwenyewe inasemekana kuwa anataka kuwania urais mwaka 2015. Na anakaribishwa na makanisa kuyachangia na anachangia.

Kinachoonekana hapa ni kwamba Sitta anaona kuwa Lowassa ana uwezo mkubwa wa kuchangia makanisa na misikiti kuzidi uwezo wake yeye. Kwa hiyo anamwonea wivu. Kama kweli Sitta hana lengo la kununua watu makanisani basi aache kabisa kuchangia makanisani. Kinachogomba hapa si kiasi cha fedha mtu anachochangia makanisani, bali kitendo chenyewe cha kuchangia makanisa.

Kama kitendo cha kuchangia makanisa ni ufisadi basi Sitta  aachane na kuchangia makanisa ama sivyo na yeye atawekwa kundi la mafisadi.

Ukweli ni kwamba Lowassa anaonekana kuwa ni mtu wa watu kuliko alivyo Sitta. Kwa hiyo, Sitta ana kila sababu ya kumwonea wivu Lowassa. Na ukizingatia Sitta hajaacha kumsema vibaya Lowassa popote anapopata nafasi, tunaweza kukubaliana kwamba Lowassa anamnyima Sitta usingizi.

Hakuna anayeweza kudai kuwa Lowassa ni mtu safi kabisa. Lakini kama ni mchafu sana basi Sitta atoe ushahidi wa kuthibitisha kwamba fedha za Lowassa ni chafu.

Turudi nyuma. Mwishoni mwa miaka ya 1970 Tanzania iliendesha vita dhidi ya  walanguzi na wahujumu uchumi. Kule Mwanza alikamatwa mtu mmoja kwa kukutwa anamiliki nyumba nyingi na magari. Akawekwa katika kundi la wahujumu uchumi. Akaletwa mahakamani. Akahukumiwa kwa kuhujumu uchumi. Lakini alikata rufani.

Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki iliposikiliza rufani hiyo ilitaka Serikali ya Tanzania ithibitishe mtu huyo alivyohujumu uchumi kwa kuwa iliona mtu kuwa na nyumba nyingi na magari si kuhujumu uchumi. Ni matokeo ya juhudi zake za kutafuta maendeleo.

Inasemekana kwamba kitendo cha mtu huyo kuibwaga Serikali ya Tanzania kilichangia sana Tanzania kuanzisha mahakama yake ya rufani mwaka 1979.

Katika mazingira hayo hayo, wakati umefika kwa Sitta kututhibitishia kwamba fedha za Lowassa ni chafu. Vinginevyo, aachane na Lowassa. Mbona wote mnasafiri katika mtumbwi mmoja wa Chama Cha Mapinduzi? Ya nini kugombana? Vita ya siafu si furaha ya kunguru?


1162 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!