NA MOSHY KIYUNGI

Tabora

Kundi la wanamuziki wa Soukous Stars limekuwa likifanya vyema pindi wanapopata mchongo popote pale Duniani.

Hawa ni wanamuzikia raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huishi katika nchi tofauti duniani, kila mmoja huko aliko anayo shughuli ya kuendesha maisha yake.

Mfano wa karibu ni wanamuziki Lokassa ya Mbongo ambaye ni maarufu kwa kulicharaza gitaa la rhythm, pia ni mwenye uwezo wa kutunga na kuimba ambaye makazi yake yapo nchini Marekani.

Aidha muungurumishaji wa gitaa zito la besi, Ngouma Lokito, naye amefanya makazi Marekani.

Tofauti na bendi, wao ni kundi linalojitegemea, hupiga muziki popote wanapo alikwa. Soukuos Stas wamekwisha toa album nyingi ikiwemo ya Studio album ya Soukous Stars Morenita, iliyotoka mwaka wa 1993.

Uandaji wa album hiyo ulifanyika nchini Ufaransa katika studio za Galaxy Sound Studios na Studio Harry Son.

Nyimbo nyingine za Soukous Stars ni pamoja na Robin uliotungwa na Lucien Bokilo, Sophia uliotungwa na Lokassa Yambongo, Morenita, utunzi wake Ballou Canta na Rhoda uliotungwa na Ngouma Lokito.

Nyingine ni Rosy, uliotungwa na Shimita, ambaye ni mwimbaji na pia mnenguaji mkuu wa kundi hilo.

Wimbo wa Aba Guimo, ulitungwa na Philippe ‘Saladin’ Ferreira, ambaye pia ndiye mcharazaji mahsusi wa gitaa la solo. Wimbo wa Cayina, ulitungwa na mwana mama Yondo Sister Kusalaa, ambaye licha ya utunzi, pia ni mwimbaji na mnenguaji mahiri katika kundi hilo.

Kundi la Soukous Stars lina mafundi na wanamuziki ambao hupiga ala za muziki wakimwemo mtayarishaji mkuu, Emma Helou akisaidiana na Mustapha Sesay.

Kinanda  Filimbi, Saxofonie hupigwa na Abdul Mbacki na Andy Suzuki. Kwa upande wa  sauti waimbaji ni Ballou Canta, Luciana Bokilo, Shimita Balou Kanta, Shimita el Diego na Yondo Sister.

Katika harakati za kufanya vizuri kimuziki, Soukous Stars miaka kadhaa ya nyuma, wanamuziki akina Lokassa ya Mbongo, Ngouma Lokito, Balu Kanta na wengine walinakiri nyimbo za wanamuziki kutoka Tanzania na kuzitoa katika wimbo mmoja waliouita ‘Nairobi Night.’

Nyimbo hizo zilikuwa Dada Asha wa Tabora Jazz, wana Segere matata na Vigelegele ndiyo furaha na Roza za Western Jazz, Wana Saboso.

Soukous Stas walinakiri maneno yake na melodi yake pia walinakiri mapigo ya vyombo vyake.

Wanamuziki hao wakapata sifa kubwa kwa wapenzi wa muziki, baada ya kubaini uelewa wao mkubwa wa masuala ya muziki.

Walijua thamani halisi ya nyimbo hizo kama zingeuzwa katika hali zilivyotengenezwa na Watanzania.

Kundi hilo hilo lilishawahi kujumuisha katika albam yake nyingine kipande cha wimbo wa ‘tufurahi wikiendi’ wa bendi ya Afro70, Wana Afrosa iliyokuwa ikiongozwa na marehemu Patrick Balisidya. Kipande hicho walikiimba kama kilivyoimbwa na Afro 70 wenyewe.

Tshala Muana, pamoja na umaarufu wake mkubwa kimuziki, aliunakiri kama ulivyo wimbo ‘Dezo dezo’, wimbo ulitungwa na kupigwa na bendi ya Zaita Musica, ‘Wana Zuke Muselebende’ chini ya uongozi wake marehemu Maestro Supreme Ndala Kasheba.

Wimbo huo ni mzuri sana kuliko alioupiga Tshala Muana.

Zaita kirefu chake kilikuwa ni Zaire – Tanzania, kwa kuwa ilikuwa na wanamuziki waliokuwa wanatoka nchi hizo mbili.

Wimbo wa ‘Dada Asha’ pia uliwahi kutumiwa kibiashara na mwanamuziki mkubwa wa Jamhuri ya Kidempkrasia ya Kongo, Afrika na Dunia, marehemu Tabu Ley (Roucherou).

Tabu Ley yaelezwa kwamba alinunua Kanda katika mitaa ya jiji la Nairobi.

Alipokuja hapa nchini mwaka 1987 kwenye sherehe za miaka 10 ya CCM, mwenyewe aliomba akutane na mtunzi wa wimbo  wa ‘Dada Asha’ ili waelewane kutokana na yeye kuutumia wimbo huo kibiashara.

Vile vile, bila wengi kugundua, Werrason Ngiama wa Wenge Maison Mere, aliwahi kulitumia rhythm la wimbo huo kama lilivyopigwa na Tabora Jazz katika moja ya nyimbo zake kwenye albamu yake ya Solola Bien.

Hakuna wimbo uliopigwa baadaye miongoni mwake uliovutia zaidi ya ule wa asili. ‘Dada Asha’ wa Tabora Jazz ulikuwa mzuri na wenye mapigo yaliyotulia kuliko huo wa kwenye ‘Nairobi Night.’

Hali ikawa hiyo hiyo kwa nyimbo za Vigelegele na Roza bendi ya Western Jazz wana Saboso.

Utaratibu huo wa kuimba au kionjo cha wimbo kimefanyika tangu miaka ya 1970.

Ikumbukwe kwamba zilikuwepo bendi kubwa za Dar Jazz na Kilwa Jazz ambazo nazo zilinakili nyimbo toka kwa bendi za DRC. Nyimbo hizo ni kama Lau Nafasi, Nacheka cheka na Roze waua za bendi ya Kilwa Jazz.

Miaka michache iliyopita, mchawi wa kupuliza saksafoni Afrika, Kiamangwana Waze la Mbongo Mateta ‘Verckys’ alifika nchini mwetu kufuatilia uhalali wa biashara ya kazi za muziki wa Kongo yeye kama kiongozi wa wanamuziki wa nchi hiyo.

Ujio wa Verkies alikuwa wa kiofisi kwani alikuja hapa kwa maslahi ya wanamuziki wote wa DRC.

Hilo ndilo hasa vyombo vinavyohusika mfano Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Sanaa Tanzana (BASATA) vinapaswa kufanya juhudi ya kuanzisha upya mapambano ya kufuatilia haki ya nyimbo za Tabora Jazz, Western Jazz, Afro Band 70 na Zaita Musica.

Viongozi wa kundi hilo la  Soukouss Stars waliposhtuliwa kidogo kuhusu nyimbo walizoiba, walitoa jibu jepesi kwamba nyimbo hizo walizinunua Nairobi nchini Kenya, kwa kufuata taratibu zote na hawakujua chochote kuhusu Tanzania kuhusiana na nyimbo hizo.

Hapo ukawa ndiyo mwisho wa mchezo, hakukuwa na hoja tena kutoka kwa Watanzania wenye haki yao.

Imefikia wakati ambapo Wasanii wa Tanzania kubadilika katika mikakati ya kudai haki zao kama wenzao wanavyofanya.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba; 0784331200, 0713331200 na 0767331200.

By Jamhuri