Mafanikio yoyote yana sababu (20)

Padre Dk Faustin Kamugisha

Kutenda au kuchukua hatua ni siri ya mafanikio.  Ahadi ni wingu, kutenda ni mvua. Ni methali ya Kiarabu. “Kutenda ni ufunguo wa msingi wa mafanikio yote,” alisema Pablo Picasso (1881-1973), mwandishi wa maigizo, mpaka rangi na mchongaji wa sanamu wa Hispania.

Matendo yana kauli kuliko maneno. Watu wanaofaulu wanafika juu ya mlima kwa kuupanda na waotaji ndoto tu za mafanikio wanakaa chini ya mlima na kuwaza juu ya kupanda mlima.

“Si kila mara kutenda kutaleta furaha, lakini hakuna furaha bila kutenda,” alisema Benjami Disraeli (1804-1881) ambaye alihudumu awamu mbili kama Waziri Mkuu wa Uingereza. Tunaweza kusema hakuna mafanikio bila kutenda au kuchukua hatua.

Unataka kujua wewe ni nani? Usijiulize. Kutenda kutakutambulisha na kukuainisha. Matendo yanakuthibitisha wewe ni nani. Maneno yanathibitisha unataka kuwa nani.

“Chukua hatua. Inchi ya mwendo itakufikisha karibu na malengo yako kuliko maili ya kunuia,” alisema Steve Maraboli, mhamasishaji na mwandishi wa vitabu wa Marekani aliyezaliwa mwaka 1975. Kuwa na nia ni siri ya mafanikio lakini nia tu haitoshi. Ukinuia kufanya biashara, fanya. Ukinuia kulima, lima.

Ukinuia kusoma soma. Ukinuia kuwa mwanamichezo, cheza. Umbali kati ya nia na uhalisia ni kutenda. Kuna mlevi ambaye aliamua kuacha kunywa pombe kabisa kutokana na matokeo mabaya ya ulevi katika maisha yake.

Alianza kuvunja chupa kwenye kreti ya bia. Kila alipovunja chupa alisema maneno fulani. Alipochukua chupa ya kwanza alisema: “Wewe umenifanya nikose karo ya watoto.” Alivunja chupa hiyo.

Alipochukua ya pili alisema: “Wewe umenifanya nifukuzwe kazini.” Alivunja chupa hiyo. Alipochukua chupa ya tatu alisema: “Wewe umenifanya nigombane na wanafamilia.”

Alivunja chupa hiyo. Alipochukua chupa ya nne alikuta haijafunguliwa, alisema: “Wewe kaa pembeni huusiki katika ugomvi huu, nitakunywa baada ya shughuli hii.” Huyu alikuwa anasitasita katika uamuzi wake.

“Kutotenda kunazaa mashaka na hofu. Kutenda kunazaa kujiamini na ujasiri. Ukitaka kuishinda hofu, usikae nyumbani na kufikiria juu yake. Toka nje shughulika,” alisema Dale Carnegie.

Tukumbuke hofu ni adui wa kwanza wa mafanikio. Kuna mambo mengi duniani yanakwama kwa sababu ya hofu. Unaweza kukwamisha mafanikio yako kwa sababu ya hofu. Jambo jingine ambalo linafanya watu wasifanyie kazi ndoto zao ni kuwa katika eneo la faraja.

Lakini wakumbuke kuwa katika eneo la faraja hakuna kitu kinachipuka. “Hakikisha kuwa matendo yako na tabia yako vinaendana na kuakisi maneno na mawazo yako, ahadi na kujitoa vinavyotoka mdomoni mwako,” alisema Steve Farber.

“Kufikiri muda mrefu kufanya jambo fulani mara nyingine matokeo yake ni kutolifanya,” alisema Eva Young. Kama ni tendo la kukuletea mafanikio fursa hiyo imetoweka. Katika msingi huo Victor Kiam alisema “Kusitasita ni muuaji wa fursa.”

“Matokeo ya kusitasita ni majuto ya kuhuzunisha. Kazi za leo ambazo zinaahirishwa zinatupa mizigo miwili ya kubeba, njia nzuri sana ni kuzifanya muda wake mwafaka,” alisema Ida Scott Taylor.

Unaweza kujikuta umebeba mizigo ya jana ambayo hukufanya na mizigo ya leo ambayo utu na ukarimu mtoto wake vinakudai uvifanye.

Kama unataka ukarimu au tendo la huruma lionekane ni jambo gumu sana kulifanya jaribu kuliahirisha! Kuna aliyesema, “Namna nzuri ya kufanya jambo lifanyike ni kuanza.”

Ukingoja mpaka uwe tayari utangoja maisha yako yote. Kuna aliyesema: “Hakuna lifti ya kukupandisha hadi kwenye mafanikio, lazima upande ngazi.”

Please follow and like us:
Pin Share