Bandari ya Tanga fursa muhimu kwa uchumi wa Tanzania

Katika toleo la wiki iliyopita tuliwaletea makala iliyohusu bandari ya Mtwara kwa jinsi
ilivyobeba fursa ya viwanda kwa ukanda wa kusini mwa Tanzania na taifa kwa jumla. Pia
bandari ya Mtwara inatarajiwa kuwa tegemeo kwa nchi jirani hasa baada ya uboreshaji na
upanuzi wa bandari ya Mtwara kukamilika kwa jinsi utakavyokuwa chachu ya kufungua
milango katika kuhudumia shehena kutoka nchi za Malawi, Zambia na Msumbiji.
Katika makala ya leo tunakuletea taarifa za bandari ya Tanga ambayo ni miongoni mwa
bandari kubwa nchini zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Bandari hii inayopatikana kaskazini mwa Tanzania katika pwani ya bahari ya Hindi ni fursa
kubwa katika kuleta chachu katika uchumi wa viwanda kwa mikoa ya kaskazini na kwa nchi
jirani za Uganda na Sudani ya Kusini. Pia bandari hii inaweza pia kuhudumia soko la nchi za
DRC, Burundi na Rwanda kupitia bandari kavu ya Isaka na bandari ya Kigoma kwa kutumia
miundombinu ya Reli na barabara.
Bandari ya Tanga ilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1888. Bandari hii ina uwezo
wa kuhudumia meli zenye uzito wa zaidi ya tani 1,200. Shughuli za upakuaji na upakiaji meli
hufanyika kwenye maji yenye kina kirefu (Nangani). Meli zenye uzito chini ya huo uhudumiwa
bandarini (Gatini). Bandari hii ina gati yenye urefu wa mita 462 na kina cha maji kuanzia mita
2 hadi 3.5 wakati wa bamvua dogo na asili gati lilijengwa na kina cha maji cha mita 5.
Kwa upande wa maji marefu ambako bandari inahudumia meli kubwa nangani (Deep sea
vessels) kuna kina kati ya mita 8 hadi 18. Vifaa mbalimbali hutumika katika kuhakikisha meli
inahudumiwa nangani na gatini ikiwemo Matishari ya kati ya tani 80 hadi 600 ambayo
huvutwa na ‘Tugs’. Bandari ya Tanga kama ilivyo bandari nyingine Tanzania inafanya kazi saa
24 siku 7 za wiki na siku 365 za mwaka.
Katika kipindi cha mwaka 2015/ 2016 hadi mwaka 2017/ Februari 2018 bandari ya Tanga
imehudumia jumla ya shehena ya tani 1,861,037 huku shehena ya mafuta iliyohudumiwa
ikiongezeka kwa kipindi cha miezi nane ya Julai 2017 hadi Februari 2018 kufikia tani 212,818.
Mwaka 2015/2016 tani zilizohudumiwa zilikuwa tani 169,893 wakati mwaka 2016/2017 tani
231,597 za mafuta zilihudumiwa.
Katika kuhakikisha bandari ya Tanga inaleta chachu katika sera ya taifa ya uchumi wa
viwanda, serikali kupitia TPA inatekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuifanya bandari
ya Tanga inaleta mchango mkubwa kwa taifa katika uchumi wa viwanda. Kwa kuwa bandari
ni lango la uchumi na biashara, TPA imeona ni vyema kuijengea uwezo bandari ya Tanga ili
iweze kuhudumia meli na shehena kubwa kwa ufanisi.
Ili kufanikisha azma hiyo miradi mbalimbali imekuwa inatekelezwa ikiwemo ya muda mfupi
kama vile manunuzi ya vifaa, miradi ya muda mrefu kama ujenzi wa sehemu ya kuhifadhia

makasha na uboreshaji wa gati namba 2 kwa ajili ya kuhudumia meli na mizigo kwa ufanisi
wenye tija kubwa.
TPA inatekeleza mradi wa kuboresha gati namba 2 ambapo maboresho yanayofanywa ni
pamoja na kuongeza kuchimba kina kwa zaidi ya mita 2, kuimarisha gati na kuweka mfumo
wa kuzuia kutu katika nguzo. Mradi huu utakapokamilika utasaidia kuongeza uwezo wa
kuhudumia meli na shehena zaidi. Pia mradi huu utawezesha wafanyakazi kufanya kazi katika
mazingira bora na usalama wa vyombo vitakavyohudumiwa.
Katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa bandari na mizigo ya wateja na kudhibiti uingiaji na
utokaji bandarini, TPA inatekeleza mradi wa kisasa wa ulinzi kwa kuweka kamera za CCTV na
vifaa maalum vya ukaguzi (metal detectors) na kuweka mashine ya kukagulia mizigo
(scanners) inayoingia na kutoka bandarini. Mradi huu utakapokamilika utasaidia kuimarisha
ulinzi na usalama wa bandari na utasaidia kujiridhisha usalama na uhalisia wa mizigo
inayopita bandarini.
Aidha katika bandari ya Tanga kuna mradi mkubwa wa kimataifa wa bomba la mafuta
unatekelezwa ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2019 na kuanza kazi rasmi mwaka
2020. Bomba hili lenye urefu wa kilomita 1,444 na upana wa inchi 54 litaanzia Hoima,
Kabaale nchini Uganda na litaishia bandari ya Tanga kwa kupitia mikoa ya Kagera, Geita,
Shinyanga, Simiyu, Singida, Manyara, hadi Tanga kupitia wilaya ya Handeni na Muheza.
Mradi wa bomba hili utakapokamilika inakadiriwa litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa
200,000 kwa siku. Inatarajiwa kwamba meli uwezo wa mpaka tani 250,000 (Suezmax)
zitakuwa zinaingia katika bandari ya Tanga. TPA tayari imeshaainisha eneo lenye mita za
mraba 2,400 ambalo litatumika kuhifadhia kwa muda vifaa vya ujenzi kabla ya Pongwe katika
eneo mahsusi lililotengwa na Jiji la Tanga kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta.
Bandari ya Tanga ilichaguliwa kuwa lango la kupitishia mafuta ghafi kutoka Uganda kwa
sababu eneo la kufunga meli lina kina kirefu hadi kufikia mita 23. Pia eneo hilo lina kingo za
asili ambalo limezibwa na kisiwa cha Pemba na mafungu kama Niuli na Fungu Nyama. Tayari
eneo la Chongoleani lenye hekta 200 lililoko kilomita 6 kutoka barabara kuu ya Tanga –
Mombasa limeainishwa na fidia iliyofikia kiasi cha Shilingi 2,979,130,838/= zimeshalipwa kwa
wakazi wa eneo hilo.
Mradi huu wa bomba la mafuta utakapokamilika utakuwa na faida mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kuchangia pato la taifa kwa kuwa tozo
zitakazokuwa zinakusanywa kwa upande wa meli zitakazokuwa zinaingia pamoja na utumikaji
wa eneo bomba litakakopita (wayleave). Wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi idadi ya
Watanzania kati ya 15,000 hadi 20,000 watapata ajira katika bomba hili. Bomba hili
litachangia uchumi wa mkoa pamoja na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Ujio wa bomba hili unatarajia kuchochea miradi mingine kama ujenzi wa reli kutoka Tanga
kuelekea nchi za Maziwa Makuu. Mradi huu utachochea kasi ya utafutaji wa mafuta katika
nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha TPA imeshawasilisha serikalini mradi wa ujenzi wa bandari ya Mwanmbani ili kumpata
mwekezaji. Eneo la Mwambani liliainishwa na kuwekwa jiwe la utambuzi na serikali tangu
mwaka 1975. Eneo hilo lina ukubwa hekta 174.2 na fidia ya shilingi bilioni 2.59 zimeshalipwa
kwa wakazi wote wa eneo la mradi baada ya tathimini kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Mradi wa bandari ya Mwambani baada kukamilika utaondoa changamoto za bandari
kuhudumia meli nangani na kuiwezesha bandari kuhudumia shehena inayokadiriwa kuwa tani
2.5 kwa mwaka.