Spika, CAG ngoma nzito

Kama ungekuwa mchezo wa soka, basi ungesema zimechezwa dakika 90 zimekwisha, zikaongezwa dakika 30 zikaisha timu zikiwa sare, sasa wanaelekea kwenye kupiga penalti. Huo ndiyo mchuano uliopo kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad.

Mvutano wa viongozi hawa umeleta hisia kali juu ya nani ataibuka mshindi katika mabishano kati ya Spika Ndugai na CAG Assad, huku viongozi walio wengi wakitoa maoni bila kuwa tayari kunukuliwa.

“Nakuhakikishia Prof. Assad ndiye atakayepoteza. Nimezungumza na viongozi kadhaa wa Bunge, wamemwekea mtego. Ukiangalia wamemwita kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge na si kamati inayohusiana na hesabu kama PAC. Hapa CAG asipokwenda analo.

“Najua wengi tunasubiri kuona nani ataibuka mshindi, lakini Bunge lina mamlaka ya kuagiza mtu yeyote afungwe. Tumekwisha kushuhudia Mbunge Ester Bulaya akisafirishwa kwa helikopta kutoka Bunda hadi Dar es Salaam. Sasa kama CAG anadhani Ndugai anatania atakiona cha moto,” amesema mwanasheria aliyeomba asitajwe.

Habari kutoka ndani ya Bunge zinasema Bunge limejiandaa kulinda heshima yake, hasa baada ya Spika Ndugai kuagiza Prof. Assad aitwe kwenye Kamati ya Maadili. “Tunafahamu tabia za Prof. Assad hata wakati akiwa chuoni. Tumeyasikia maneno aliyotamka, kwamba hatakuja. Spika wetu amesema tujiandae.

“Kimsingi hatuoni atashindwaje kuja. Sisi hatukumuita kwenye Kamati inayohusiana na Hesabu za Serikali au aina yoyote ya hesabu aliko na kinga anayoitaja, ila ameitwa kwa suala la maadili. Hii ni sawa la wale polisi wa Mwanza wa dhahabu, ambao walikamata watuhumiwa wakawa wanazunguka nao kila kona wakidai rushwa.

“Ni kweli kuwa hata polisi anayo kinga kisheria. Ukimzuia polisi kufanya kazi yake unashtakiwa. Tumeona wale polisi wa Mwanza walipokiuka maadili ya kazi yao wamekamatwa na wamo ndani. Bunge halijasema linataka kupitia taratibu zake za kihesabu. Tunataka afike mbele ya kamati aeleze hayo maneno aliyosema akiwa Marekani kuwa Bunge ni dhaifu, atueleze kama hiyo ilikuwa sehemu ya kazi yake ya kukagua hesabu?

“Hii taarifa ya CAG inayoletwa bungeni ni maswali tu (query). Hata hiyo ripoti iliyodaiwa kuwa Sh trilioni 1.5 zimepotea tayari majibu yaliishapatikana. Mengi unakuta ni makosa ya kutofuata taratibu, ila sasa anataka kuonyesha yeye ndiye yeye. Subiri ifike hiyo Januari 21, 2019, mbichi na mbivu zitajulikana,” amesema ofisa mmoja wa Bunge.

JAMHURI limemtafuta Spika Ndugai, aliyesema: “Nimekwishatoa kauli, na sasa sina la ziada. Naisubiri hiyo tarehe, hivyo siongezi neno.”

Awali, Spika Ndugai alimtaka CAG, Profesa Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge Januari 21, 2019 kwa hiari kwa ajili ya kuhojiwa, vinginevyo atapelekwa kwa pingu.

Mbali na CAG, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, naye ameitwa mbele ya kamati hiyo siku inayofuata, yaani Januari 22, 2019.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo Januari 7, 2019 alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma akasema Profesa Assad amelidhalilisha Bunge.

Ndugai amesema CAG akiwa nje ya Tanzania  wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili Radio ya Umoja wa Mataifa alisema kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu.

“Kama ni upotoshaji, basi CAG na ofisi yake ndio wapotoshaji. Huwezi kuisema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi,  na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” amesema Ndugai.

Ndugai amesema kitendo hicho kimemkasirisha, kwani hakutegemea msomi kama huyo angetoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.

Ujumbe wa Prof. Assad

Katika ujumbe aliotoa kama ishara ya kumjibu Spika, Prof. Assad alisema: “Mmeuliza kama nitaitikia wito, sijajibu hili. Ila niweke rekodi sawa, ule si wito bali ni amri. Sasa kwa kuheshimu Katiba yetu na kwa kuwa sitaki kuwa miongoni mwao waivunjao niseme hivi: Ibara ya 18a inampa kila mtu uhuru wa kutoa maoni, hivyo kwangu mimi, nachukulia haya yote kama mtu kaamua kutoa maoni na kuelezea fikra zake.

“Jambo la pili, Ibara ya 26(1) inaeleza wajibu wa kila mtu kufuata na kutii Katiba ya nchi. Sasa mimi nilidhani mtu kama Spika alipaswa kuwa mfano bora katika kuhakikisha kuwa Ibara ya 143 inayonitambua mimi na taasisi ninayoiongoza inaheshimiwa kama inavyostahiki. Niseme tu, nitasimamia ninachokiaamini kitaaluma na kizalendo kwa masilahi mapana ya taifa letu.”

JAMHURI limemtafuta Prof. Assad afafanue ujumbe huu alioutuma kwenye mitandao ya kijamii bila mafanikio.

Alichosema CAG

Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu, lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

CAG Prof. Assad alijibu: “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

Mwaka 2018 liliibuka suala la upotevu wa Sh 1.5 trilioni kwenye hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2016 – 2017, na Prof. Assad alipoulizwa nini kifanyike kudhibiti hali kama hiyo, akasema Bunge liulizwe kwani ndilo lenye kutakiwa kuibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha hizo.

Bunge linakwenda kuaibika

Mwanasheria nguli aliyeomba asitajwe gazetini amesema: “Ninachoona Bunge linakwenda kupata aibu liliyotaka kuikwepa. Ni vema Katibu wa Bunge amshauri Spika aondoe agizo lake. Katiba ukiisoma vema Ibara ya 143(6) iko wazi. Bunge halina mamlaka ya kumchunguza au kumhoji CAG kwa jambo lolote. Chombo pekee kinachoweza kumchunguza au kumhoji CAG iwapo ametumia vema madaraka yake au la ni Mahakama.

“Ibara hiyo inasema katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.”

Spika mstaafu Msekwa

Hivi karibuni Spika (mstaafu), Pius Msekwa, kwa upande wake ameunga mkono hatua ya Spika Ndugai: “Spika anayo mamlaka ya kumuita mtu yeyote aje mbele ya Bunge, ni kwa mujibu wa sheria ya Bunge na inampa sifa Spika na uwezo alioutumia. Hata ningekuwa mimi ningemuita CAG. Haiwezekani Mtanzania kaenda nje ya nchi akaanza kulaumu Bunge la Tanzania.

“Ni kosa kubwa sana, anastahili kukemewa na mamlaka ya Bunge. Hakuna tatizo ila CAG ndiye aliyeleta tatizo, hata kama alitoa maoni yake binafsi angeweza kutoa maoni yake hata akiwa ndani ya nchi,” amesema Msekwa.

Ludovick Utouh

Taasisi ya Wajibu inayoongozwa na CAG (mstaafu), Ludovick Utouh, imesema busara inahitajika kutumika kumaliza sintofahamu iliyopo kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Katika taarifa kwa umma iliyoitoa wiki iliyopita, taasisi hiyo imesema: “WAJIBU – Institute of Public Accountability (WAJIBU), ni Taasisi inayojihusisha na masuala ya uwajibikaji hapa nchini. lmeendelea kufuatilia kupitia vyombo vya habari Tamko la Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyoitoa kwenye mahojiano ya ldhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa (UN Redio).

“Kwa kuwa suala hili limeleta sintofahamu kwa jamii, WAJIBU ikiwa ni miongoni mwa taasisi za fikra za uwajibikaji nchini imeona ni vizuri itoe maoni huru kwa kuzingatia masilahi mapana katika uwajibikaji na utawala bora nchini. Ifahamike kuwa Bunge na CAG ni vyombo vinavyotambulika na kulindwa kikatiba.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), pamoja na Sheria ya Kinga, Haki na Mamlaka (Madaraka) ya Bunge ya mwaka 1988, Bunge ni mhimili unaoishauri na kuisimamia Serikali katika matumizi bora ya rasilimali za umma. Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Kinga, Mamlaka (Madaraka) na Haki za Bunge ya mwaka 1988 kinasema (tafsiri isiyo rasmi):

“‘Bunge, Kamati za Kudumu au Kamati za Muda za Bunge kulingana na matakwa ya kifungu cha 18 na kifungu cha 20 cha Sheria hii, zinaweza kuagiza mtu yeyote kuhudhuria mbele ya Bunge au Kamati husika kutoa ushahidi au kuwasilisha nyaraka alizonazo au zilizo chini ya usimamizi wake.’

“Katiba hiyo hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 143 (1-5) pamoja na Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 zimeainisha majukumu ya CAG. Aidha, Ibara ya 143(6) inampa CAG kinga na uhuru wa kutoingiliwa na mtu au taasisi yoyote ya Serikali kama inavyonukuliwa hapa chini:

“‘Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.’

“Kwa kuzingatia umuhimu wa taasisi hizi mbili katika kusimamia rasilimali za umma na kukuza uwajibikaji na utawala bora, ni vema busara ya hali ya juu itumike baina ya pande hizi mbili katika kutatua mgogoro huu kwa sababu dhana ya uwajibikaji na utawala bora nchini itaimarika iwapo tu kutakuwepo na uhusiano mzuri kati ya taasisi zote za uwajibikaji na usimamizi nchini.

“Kutokana na umuhimu wa taasisi hizi mbili ambazo zinatakiwa kushirikiana kwa karibu sana katika kuimarisha uwajibikaji na utawala bora hapa nchini, wananchi wanashauriwa kutoa maoni yatakayoboresha na kuimarisha uhusiano wa taasisi hizi.

“Kwa muktadha huo, WAJIBU inaamini kwamba sintofahamu iliyojitokeza kati ya CAG na Bunge ni vema ikashughulikiwa kwa busara kati ya pande zote mbili bila kuathiri uhuru wa kikatiba uliotolewa kwa Mhimili wa Bunge na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.”

Jumatatu ijayo ndiyo siku ambayo mtifuano huu utahitimishwa au kuanza upya kutokana na kwamba Bunge limesisitiza kuwa asipofika Januari 21, 2019 basi atakokotwa hata kwa pingu.