Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) inatarajiwa kushuka dimbani Juni 8 mwaka huu, kucheza na Morocco katika mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki Mashindano ya Kombe la Dunia 2014 yatakayopigwa nchini Brazil.

Rais Jakaya Kikwete amewataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanafuzu kucheza fainali zijazo za Kombe hilo.

 

Kauli ya kuitaka Stars kucheza Kombe hilo, aliitoa hivi karibuni Ikulu, Dar es Salaam, alipokutana nao wakati alipowaandalia chakula cha mchana.

 

Rais Kikwete amesema amefurahishwa na matokeo mazuri ya Stars, inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi C, na kusema kwamba sasa Watanzania wanaipenda baada ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizotangulia.

 

Katika hafla hiyo, Rais Kikwete amesema kuna wakati hamasa ilipotea na kuwafanya baadhi ya mashabiki kuingia uwanjani wakiwa wamebeba mabango ya ‘Best Losers’, huku yakiwa na maneno ya kejeli.

 

Amesema wengine waliacha kwenda na baadhi kuzishangilia hata timu pinzani. “Kuna kipindi nilikuwa nafikiria hata kuacha kumlipa kocha wa timu ya Taifa na kuliacha jukumu hilo kwa TFF, hata hivyo, niliona kocha atakufa njaa na kuendelea na uamuzi wa awali.

 

“Nafurahi kuona sasa kuna mafanikio makubwa, lakini tunatakiwa kuhakikisha tunafuzu kwa ‘kuzinyoa’ timu zote katika mzunguko huu wa pili,” amesema.

 

“Kufungwa kunatunyong’onesha hata sisi ambao tunafuatilia michezo, hakikisheni mnatupa raha na mimi niko tayari kusaidia kila kitu,” amesema Kikwete.

 

Nahodha wa timu ya Taifa, Juma Kaseja, amemshukuru Kikwete kwa mchango wake na kuahidi kufanya vyema katika mechi zote na kufuzu.

 

Stars ikiongozwa na Kocha wa timu hiyo, Kim Poulsen, imeondoka Jumapili kwenda kupiga kambi nchini Ethiopia, ambako itacheza mchezo wa kujipima nguvu na Sudan kabla ya kuwavaa Morocco.

 

Kikosi kilichoondoka ni Makipa ni nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam),

Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam).

 

Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).

 

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na Salum Abubakar (Azam).

 

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).

 

Mchezo huo utakaokuwa wa kujipima nguvu, utakuwa ni mwisho kwa Stars, lakini ni wa muhimu kwa timu hiyo kutokana na ubora wa timu ya Morocco.

 

Stars iliyo katika Kundi C ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, wakati Ivory Coast inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi saba.

 

Morocco inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili na ya mwisho ni Gambia nayo ikiwa na pointi mbili sawa na Morocco, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

 

Katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Machi 25 mwaka huu, Stars, wakiongozwa na wachezaji wawili wa TP Mazembe – Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu – waliwapiga kumbo Morocco na kutupia 3-1.

 

Kati ya mabao hayo, mawili yalifungwa na Samatta, na Ulimwengu aliyetokea benchi dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto, kutupia bao moja.

 

Kwa ushindi huo iliyoupata kutoka kwa timu ngumu na yenye uzoefu mkubwa katika michuano ya kimataifa, Stars ina kila sababu ya kutobwetekea ushindi huo bali inatakiwa kuweka mikakati itakayoongeza nguvu na kusonga mbele hadi kituo cha mwisho Rio de Janeiro, Brazil.

 

Watanzania tuna kila sababu ya kuelekeza sala, fikra na kila msaada wa hali na mali kuisaidia Stars kushinda katika michezo yao iliyobaki.

 

Hakuna linaloshindikana chini ya jua. Kama wengine  wameweza kwanini  Taifa Stars tushindwe? Yote yanawezekana.

 

Tayari Rais Kikwete ameonesha nia kwa kutamka kuwa atawazawadia Taifa Stars zawadi itakayowafanya wamkumbuke katika maisha yao yote.

 

Wachambuzi wa  mambo ya michezo wanasema kuwa  pamoja na kuwa wachezaji hao wanakuwa na uzito wa kuelewa mafundisho ya kocha Poulsen lakini ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo.

 

Wanasema kufanya vizuri kwa kikosi hicho kunatokana wachezaji wa wengi kuwa na  vipaji kuliko mpira wa kufundishwa ikichangiwa na umahili wa wachezaji wanaocheza mpira wa kulipwa nchi ya Kidemkrasia ya Congo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

By Jamhuri