Nianze kwa maneno mepesi. Anachokifanya sasa hivi Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, ni kutapatapa. Amegeuka kuwa mtu wa kulalama na kulalamika kila uchao utadhani ndiyo kwanza “anazaliwa”, na wala hajawahi kuwa mmoja wa  vigogo wakubwa kabisa Tanzania.

Rushwa. Hii ndiyo kete kuu ambayo Sumaye anaamua kuitumia katika harakati na mbio zake za kuisaka Ikulu. Rushwa. Yaap. Rushwa.

Kama vile “amezaliwa” leo, na wala hajawahi kuwa mmoja wakuu kabisa nchini, Sumaye anafoka, analalama na kupiga kelele kwamba uongozi kwa sasa Tanzania umekuwa “rushwa-oriented”. Ili uupate uongozi, hasa ule wa kuchaguliwa, lazima uwe tayari kukohoa rushwa ili uununue.

Amegeuka kuwa ‘nabii” yule atarajiwaye katika mapambano ya vita dhidi ya rushwa. Kwamba anaichukia rushwa. Kwamba anapambana vita dhidi ya rushwa. Mashambulizi yake hasa ndani ya chama chake — Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika mikutano na mahojiano yake na vyombo vya habari, amekuwa akikishutumu chama chake kwamba kimekithiri kwa rushwa, hasa katika eneo la kutafuta uongozi ndani ya chama na au “kwa tiketi” ya chama.

Sumaye, kama vile amezaliwa leo na wala hajawahi kuwa mmoja wa vigogo wakuu kabisa Tanzania, au sasa amegeuka kuwa nabii yule atarajiwaye kupambana na vita dhidi ya rushwa Tanzania, amekuwa akionekana (kwa maneno) akiichukia rushwa inayoonekana kushamiri kwenye chama chake.

Rushwa ni ugonjwa tete unaoonekana kutafuna maeneo mengi nchini. Kwa Sumaye, kama vile amezaliwa leo na wala hajawahi kuwa mmoja wa vigogo wakuu kabisa nchini. Rushwa inayomtesa na kumuumiza ni ile iliyoko ndani ya chama chake wakati mtu anapotafuta uongozi. Ukichunguza kwa makini kauli zake utabaini kwamba rushwa ya kununua au kuuza uongozi ndiyo aliyoikomalia zaidi.

Binafsi sijamsikia Sumaye akikemea kwa nguvu zake zote rushwa zilizotamalaki maeneo mengine ambako kuna wanyonge anaodhani anawasemea. Polisi na Mahakama, kwa uchache, kunanuka rushwa. Wanyonge na maskini wanaonewa na kukosa haki zao.

Bahati mbaya, hata huku kwenye rushwa za kisiasa ambako amejiweka mstari wa mbele kuzipiga vita, nabii  huyu mpya wa vita dhidi ya rushwa hajajipanua sana. Amejifinya na kujibana kupigania maslahi yake binafsi ya kisiasa. Ni kwamba, anapigana vita kinafiki. Huwa anakuwa mbogo pale ambapo nafasi ya kisiasa anayoisaka inapoonekana kutishiwa na rushwa.

Sasa hivi anaonekana kwamba ni mpambanaji sana vita dhidi ya rushwa za kisiasa. Jibu lipo wazi. Anawania kuwa mmoja watakaoomba kuteuliwa na chama chake ili kuja kuwania urais 2015. Kwa hiyo, vita yake ni mahususi kwa ajili ya kujihami dhidi ya washindani wengine watakaojitokeza. Kwamba yeye peke yake ni msafi. Kwamba washindani wengine wanaotajwa kujitokeza kuwania nafasi hiyo kutoka kwenye chama chake, ni walanguzi wa uongozi, wananuka rushwa. Kwamba yeye peke yake ndiyo anayefaa. Kwamba wengine wote hawafai.

Sumaye anahangaika usiku na mchana akilia huruma ya Tanzania ili aonekane kwamba ni yeye peke yake aliyesalia msafi, asiyekuwa na chembe ya harufu ya rushwa, na hivyo wamwamini na kumkabidhi madaraka ya urais, huu kwangu ni udhaifu mkubwa unaomuengua moja kwa moja Sumaye kwenye marathoni ya kuwania urais kupitia tiketi ya chama chake, au kingine chochote kile, kama ataamua kukikacha chama chake endapo kitamtema. He is not a political material (frankly speaking).

Hivi karibuni amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba atarudi kijiji kwake kuchunga mbuzi kama ataenguliwa na chama chake kwa njia za rushwa katika mbio na harakati za kuwania kuteuliwa kugombea uraisi 2015.

Huu ni unafiki, na ndiyo sababu za kusema kwamba Sumaye anapigana vita dhidi ya rushwa kinafiki. Ikumbukwe na kuzingatiwa kwamba Sumaye hajaanza leo kulalama juu ya kushamiri kwa rushwa ndani ya chama chake. Kulalama kwake ni za tangu enzi.

Hangeonekana kuwa mnafiki anayepigana vita dhidi ya rushwa kwa maslahi binafsi kama angeamua kuacha siasa na kwenda kijiji kwake kuchunga mbuzi mwaka ule aliodondoshwa na Mary Nagu kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe wa NEC-CCM Taifa kutoka Wilaya ya Hanang.

Kama vile ndiyo kwanza alikuwa amezaliwa mwaka huo, Sumaye alilalama kila kona ya nchi kwamba alibwagwa kwa sababu ya mpinzani wake kumwaga pesa za rushwa. Kama kweli anaichukia rushwa na alibwagwa kwa rushwa, mwaka ule ndiyo mwaka wa Sumaye kubwaga manyanga na kwenye siasa na kwenda kijijini kwake kuchunga mbuzi. Hakubwaga manyanga, na wala hakwenda kijiji kwake kuchunga mbuzi.

Si mwaka huo tu, hata mwaka ule wakati akisaka nafasi ya kuwania urais kupitia chama chake, alisikika kulalama kufanyiwa rafu. Naukumbuka mkasa wake wa kusafiri kwenda Kigoma kujaza fomu za wadhamini wake kwa kiberenge baada ya kudai kufanyiwa zengwe na kushindwa kusafiri kwa njia ya ndege.

Hapa, angeanza kufanya maandalizi ya kujenga mabanda ya kufugia mbuzi kijijini kwake. Sina uhakika kama alifanya hivyo. Kulalama kwa Sumaye kumekuwa kama debe tupu lisiloacha kutika. Ameshakuwa waziri mkuu kwa miaka kumi mfululizo.

Angekuwa anaichukia rushwa, lazima angeacha alama ambayo ingekuwa inamsemea leo badala ya yeye kulalama kila uchao. Ameshawahi kuwa mzito ndani ya chama chake, iwe kwa kupitia kura za itifaki au vinginevyo, angekuwa anaichukia rushwa kwa vitendo angekuwa ameacha alama kwenye chama, na leo hii asingekuwa na kibarua cha kulalama kila uchao.

Baada ya miaka kumi ya uwaziri mkuu, aliondoka akiwa mwepesi. Hakuacha alama za kumsemea. Alichofanya ni kujaza tu jina lake kwenye orodha ya mawaziri wakuu wastaafu tena yeye akivunja rekodi ya kushika nafasi hiyo kwa mihula miwili mfululizo.

Hana rekodi kubwa ya kujivunia, ni kama vile anahangaika kuwakumbusha watu kwamba amewahi kuwa waziri mkuu wa nchi hii. Haishangazi kumuona akihangaika kujitangaza kupitia eneo moja tu. Rushwa. Tena rushwa ndani ya chama chake. Huyo ndiye mchawi wake mkubwa anayemuhofia kuwa ni kikwazo katika mbio zake za kuwania tena urais 2015.

Kulalamika kwake kunaweza kukufanya uamini kwamba yeye ni msafi. Anaichukia rushwa. Hajawahi kutoa wala kupokea rushwa. Si kweli. Na wala Sumaye si nabii yule ajaye katika mapambano dhidi ya rushwa. Haichukii rushwa, ila tu pale inapoonekana kumkwaza kuyafikia malengo yake binafsi ya kisiasa.

Kuonesha kwamba Sumaye mwenyewe ananuka rushwa, nitacheza naye kwenye eneo moja dogo tu. Alipokuwa madarakani kwenye wadhifa wake wa uwaziri mkuu, kuna wakati aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akiwaambia wafanyabiashara ili mambo yao yawaendee vizuri watundike bendera za CCM kwenye maeneo yao ya biashara.

Hii ilikuwa ni rushwa kwa wafanyabiashara, tena rushwa inayosigana na sheria za nchi. Na kweli, wafanyabiashara wakwepa kodi na wale wenye biashara zenye utata, walitundika bendera za CCM kwenye maeneo yao ya  biashara, na bendera hizo zikageuka kuwa kinga kwa wafanyabiashara wakwepa kodi na wale wenye biashara haramu, kama kwenye vibanda gongo, vibanda vya kuuzia bangi na dawa za kulevya.

Kama hii kwa Sumaye haikuwa rushwa, basi atusaidie kutueleza kiufasaha kwake hasa rushwa ni nini? Ni kujilimbikizia ujasiri wa kifisadi kwa Sumaye kukemea rushwa ndani ya chama chake ambayo pia kwa namna zote ameshiriki kuilea na kuikuza na sasa inamtafuna mwenyewe.

Wakati Sumaye akiwa waziri mkuu katika mihula yake miwili, alishiriki kikamilifu na Serikali yake kuuza kwa bei iliyo sawa na kugawana bure mashirika na kampuni za umma, kama vile Benki ya Biashara (NBC), pamoja na ule ufisadi mbaya kabisa wa kuuza nyumba za Serikali kwa bei iliyo sawa na kujigawia wenyewe bure nyumba za Serikali. Sumaye and the gang ndiyo hasa waliofanya siasa sasa hivi ionekane kuwa ni dili, na bei ya kununua na kuuza uongozi ndiyo hanikizo hasa la dili hilo.

Vinginevyo, apunguze kulalamika, maana fimbo anazojichapa (siyo kuchapwa), alishiriki kikamilifu kuzichuma na kuzichonga. Aidha, walioacha alama wakati wakizitumikia nyadhifa zao, wala hawasikiki kulalama. Alama walizoacha  zinaendelea kuwasemea.

 

NB: Mwandishi wa makala hii ni mwanasheria anayefanya shughuli zake mkoani Njombe. Anapatikana kwa namba 0765 892476.

1394 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!