Madaktari bingwa wa MOI wakifanya upasuaji wa kuondoa uvimbe wa mishipa ya damu kwenye ubongo kwa kutumia darubini ya kisasa iliyonunuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa zaidi ya Sh bilioni 1.

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ni Taasisi pekee bobezi katika matibabu ya Mifupa, ajali, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kati. Ikiwa na umri wa miaka 23 Taasisi hii imekua tegemeo kubwa  hapa Tanzania na nchi nyingine barani Afrika.

Katika kuboresha kwa wananchi, Serikali ya awamu ya 5 imefanya mageuzi makubwa katika Taasisi ya MOI katika kipindi cha miaka 4. 

Mwaka 2015 Mh. Rais Dkt John Pombe Magufuli alipotembelea wodi za MOI (Mwaisela na Sewahaji) alikumbana na changamoto lukuki ikiwemo janga la wagonjwa kulazwa chini kwenye sakafu kutokana na uhaba wa vitanda, uhaba wa vifaa tiba na madawa, uhaba wa vifaa vya uchunguzi vya maabara na radilolojia), mlundikano wa wagonjwa wengi wanaosubiri huduma muda mrefu.

Kwakuwa Rais Magufuli alikua na dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi, Serikali ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni 16.5 kwaajili ya kukamilisha mradi wa jengo jipya la MOI (MOI Phase III) na kununua vifaa. Fedha hizo ziliiwezesha MOI kuwa na zaidi ya vitanda 380 kutoka vitanda 159 ambavyo vilikua havikidhi mahitaji na hivyo changamoto ya kulaza wagonjwa chini imekua historia.

Pamoja na ongezeko la vitanda na maboresho ya mazingira ya kufanyia kazi, Mh. Rais Dkt Magufuli aliirahishia kazi Taasisi ya MOI kwenye upatikanaji wa vifaa tiba, vitendanishi na madawa baada ya kufanya mageuzi makubwa kwenye Bohari kuu ya madawa (MSD) ambapo katika kipindi cha miaka 4 upatikanaji wa vifaa tiba na dawa umekua kwa zaidi ya asilimia 99%

Upatikanaji wa fedha hizi kumeiwezesha Taasisi ya MOI kununua vifaa vya kisasa vya MRI, CT Scan, X-Ray ya kidijitali, X-Ray zinazohamishika, Ultrasound, Fluoroscopy na vya vifaa vya kisasa vya maabara, ICU na chumba cha upasuaji. Vifaa hivi ni vya kisasa na ni sawa na vile vinavyotumika kwenye hospitali za mataifa yaliyoendelea hakika hii ni fahari kwa nchi yetu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface anaeleza mafanikio mengine makubwa ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka 4 ya Serikali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Mh Dkt John Pombe Magufuli.

Ongezeko la vyumba vya upasuaji: Katika kipindi cha miaka 4, vyumba vya upasuaji vya Taasisi ya MOI vimeongezeka kutoka 6 hadi 9. Ongezeko hili la vyumba vya upasuaji limepelekea idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kuongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi hadi kufikia wagonjwa zaidi ya 900-1000 kwa mwezi.

Dkt. Boniface anaeleza kwamba ongezeko la vyumba vya upasuaji unakwenda sambamba na uanzishwaji wa huduma mpya za kibingwa ambazo zilikua hazipatikani hapa nchini. Huduma mpya za kibingwa za hali ya juu zilizoanzishwa  ni upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu (Athroscopy) ambapo zaidi ya watanzania 800 wameshafanyiwa upasuaji , huduma nyingine ni upasuaji mkubwa wa mfupa wa kiuno (Acetabula reconstruction) ambapo wagonjwa 500 wamenufaika.

Anasema huduma nyingine mpya ni upasuaji wa Mgongo kwa kufungua eneo dogo (Minimal invasive spine surgery) upasuaji wa kunyoosha vibiongo kwa watoto (Scoliosis), upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo (Celebral aneurism sugery), upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kwa kupitia kwenye tundu la pua (Transphenoidal trans nasal Pituitary surgery)

Kadhalika, upatikanaji wa vifaa tiba kumeiwezesha Taasisi ya MOI kuendelea kufanya upasuaji mkubwa wa kupandikiza nyonga na goti bandia (Total hip and Total Knee replacement) ambapo watanzania wengi wamenufaika.

“Wakati MOI inaanzishwa nilikuwepo, na nimekuwepo katika vipindi vyote mpaka leo, mabadiliko ambayo yametokea ndani ya kipindi hiki cha miaka 4 hayajawahi kutokea, maboresho aliyoyafanya Mh. Rais Dkt John Pombe Magufuli yametupa heshima kubwa hapa barani Afrika na duniani” Alisema Dkt Boniface.

Aidha, uanzishwaji wa huduma hizi mpya za kibingwa kumepelekea matokeo chanya yafuatayo, Dkt Boniface anaeleza.

Kupunguza rufaa za nje ya nchi: upatikanaji wa vyumba vya kutosha vya upasauji vyenye vifaa vya kisasa na uanzishwaji wa huduma mpya za kibingwa kumepelekea MOI kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi kwa asilimia 98. Rufaa hizi zimekuwa zikiigharimu serikali mabilioni ya fedha kwa ajili ya wagonjwa kwenda mataifa mbalimbali kufuata huduma.

Pia, Taasisi ya MOI imechaguliwa kuwa kituo cha mafunzo cha madaktari bingwa cha Afrika Mashariki na kati (COSECSA) ambapo madaktari kutoka mataifa mbalimbali wanakuja MOI kujifunza kadhalika MOI ipo kwenye hatua za mwisho za kuwa kituo cha mafunzo cha madaktari bingwa wa nusu kaputi (CANECSA).

 “Juhudi nyingine za Mh.Rais katika kuboresha huduma za MOI ni kuiwezesha MOI kuingia mkataba wa ushirikiano na Hospitali ya Chuo kikuu cha kimataifa cha Peking cha nchini China ili kuboresha huduma za tiba za Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu” Dkt Boniface.

Katika kuboresha huduma za upasuaji wa Ubongo hapa nchini, Serikali ya awamu ya 5 imetoa Tsh Bilioni 7.9 kwaajili ya ujezi wa Maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Endovascula Neuro-suite). Maabara hii ya kisasa inaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma za upasuaji wa ubongo kwa njia za kisasa ambapo tayari Serikali imeshawapeleka wataalamu nchini China kwaajili ya kupata mafunzo maalum ya kutumia mitambo ya maabara hiyo.

Kukamilisha Makala haya, Dkt Boniface anaangazia kwa kifupi matarajio ya Taasisi ya MOI katika kipindi cha miaka 5 ijayo kwamba ni uanzishwaji wa huduma nyingi zaidi za kibingwa, kuimarisha ushirikiano na hospitali na taasisi mbalimbali duniani na kushirikiana nazo kutoa huduma hapa nchini, kuendelea kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa katika fani za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu na kuendesha kambi za upasuaji mikoani ili kuwafikishia huduma wananchi na kusambaza ujuzi kwa hospitali za mikoa.

237 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!