Ana kwa ana na Rais Nyerere (4)

Swali:  Unasema kuwa umma hauna nguvu hasa, hii ni kweli, lakini pia ni hatari kubwa kutoa madaraka kwa umma wakati uongozi hauna imani  na jambo hilo. Mifano ya Obote na Nkrumah na viongozi wengine wa Kiafrika inaonyesha haya wazi. Hii inaonyesha hatari ambayo inaweza ikawakabili viongozi kwa sababu ya jambo hilo. Vipi mtu anaweza akajikinga na hatari ya aina hiyo ambayo ipo itokanayo na viongozi au pengine jeshi ambalo linaweza kuzotorotesha aina ya usawa unaojaribu kuuleta?

Jibu: Naelewa. Hili ni tatizo kubwa. Itakuwa ni mmoja wapo wa miujiza ikiwa Tanzania itafanikiwa. Hii inamaanisha kujihini, kwa vile viongozi wakuu, wanasiasa wakuu katika nchi ya Kiafrika, wafanyakazi wa juu wa serikali, maofisa wakuu wa jeshi, maofisa wa Polisi wanaweza wakaanzisha chama chao na kuukandamiza umma na umma usiweze kufanya chochote kabisa.

Wakuu hawa wanasema: “Haya basi tutazame; tupo hapa na nguvu tunazo.” Hii si haki. Huwezi kusema hii ni jamii huru wakati utawala umo mikononi mwa wachache ambao wanaweza wakaukalia kama wakipenda.

Kwa hiyo basi, kama unataka uhuru unasema kuwa demokrasia maana yake ni maendeleo, kwa hiyo natuendeleze jamii yetu wakati huo huo tukitoa utawala kwa umma. Mimi ninasema huku ni kujihini kwa upande wa viongozi. 

Hii inawezekana. Hapa kuna mfano kidogo: Tazama Ulaya ya Magharibi, majeshi hayajawahi kuchukua utawala, yangeweza, yanazo nguvu, nguvu za kivita ambazo zinayawezesha kuchukua utawala, lakini hayafanyi hivyo kwa kuwa jambo hilo haliafikiani na imani yao.

Mimi ninasema inawezekana kujenga demokrasia Tanzania. Nafikiri tunaweza kujenga demokrasia ingawaje sitaki kujidai kuwa ipo demokrasi hivi sasa, kwa vile demokrasi ni aina ya serikali ya watu huru na walio sawa. Pale pasipo na usawa hakuna uhuru. Kwa hiyo tunacho kiasi kidogo tu cha demokrasia. 

Nchini Tanzania imani yetu kwa demokrasia ni kubwa sana kuliko utekelezaji wetu wa demokrasia. Tunao uchaguzi na taratibu nyinginezo, lakini hatari ipo pale pale. Nchi inaweza ikaingiliwa bila taabu ikiwa umma hauna madaraka kamili. Hii ndiyo hatari yenyewe kila wakati.

Swali: Je, kwa wakati huu, ni katika mambo gani muhimu Tanzania ingeweza kujilaumu yenyewe?

Jibu: Nafikiri Tanzania ingekuwa ikisema tazama, sisi tumekuwa hodari sana katika kufikiria aina ya jamii ambayo tunataka kuijenga, lakini hatujawa hodari hasa katika ujenzi wenyewe wa jamii hii, na kila mahali, iwe serikalini au kwenye kisomo, kwenye kilimo au viwandani ni lazima  tulenge kwenye ujenzi bora.

Hatujakuwa tukifanya vizuri kama ambavyo tungeweza kufanya. Tumejitahidi, tunaweza kujilisha. Wakati mwingine tunakuwa na upungufu wa vitu, na katika jamii huru ambayo ina upungufu wa vitu malalamiko mengi hutokea.

Hili ni jambo zuri. Lakini wakati mwingine upungufu huu umekuwa ukitokana na uzembe na ninafikiri wakati umewadia sasa wa Tanzania kusema kuwa tunaweza kufanya kazi vema zaidi. Tusifanye kosa la kushirikisha ujamaa na uzembe.

Swali: Je, huwa unatiwa moyo na lawama zinazotolewa mambo ya kiharibika? Kwa mfano, matatizo ya ugawaji wa vitu. Watu hivi sasa wanaongea juu ya ukosefu wa nidhamu ya kazi. Unafikiri mtindo huu ni wa maendeleo katika jamii?

Jibu: Kusema kweli ni mtindo mzuri kwa kuwa sisi huwa tunachukua hatua wakati kuna malalamiko kuhusu mistari mirefu au mambo mengine. Vyombo vinavyohusika kuchukua hatua nafikiri vingezorota kama kungekuwa hakuna malalamiko. Nafikiri hii inatia moyo.

Swali: Je, si vizuri kwa viongozi kujitetea? Wakati unaposikia malalamiko haya utaona kuwa wanaohusika mara kwa mara hawako tayari kukubali. Upungufu mara nyingi hukaliwa wakati wananchi wanafahamu vilivyo kwamba upungufu upo. Upo mtindo kama huo wa kujikinga kwa upande wa viongozi?

Jibu: Ndiyo, ni makosa-makosa makubwa. Viongozi wasifiche makosa. Haya ni makosa kwa kuwa, njia iliyopo pekee ya kusonga mbele ni ya kukabili matatizo kama yapo na kuyakubali kuwa ni matatizo. Baada ya hapo ni kutafuta njia za kuyatatua na si kujidai kwamba hayapo.

Swali: Wakati wa kunyakua uhuru wengi wa viongozi sawa na wale waliokuwa wakiwaongoza, walikuwa maskini. Kwa nini basi hapajakuwa na mwelekeo mkubwa kwenye mali ya umma kuliko kwenye mali za kibinafsi katika uchumi? Hapa ninawazia Afrika kwa ujumla. Katika Tanzania hii haijatokea lakini imetokea sehemu nyingine.

Jibu: Nafikiri ni kama nilivyosema awali, ubepari una nguvu ya kuleta mabadiliko. Siwalaumu wale katika Afrika ambao labda kwa sababu ya tamaa au pengine si tamaa wanaitazama Ulaya ya Magharibi na kuona kuwa imeendelea sana, au wanatazama Amerika ya Kaskazini na kuona kuwa imeendelea na wanafahamu kuwa hizi ni nchi za kibepari, kwa hiyo wanasema: “Amerika ya Kaskazini, Ulaya ya Magharibi, hiyo ndiyo njia ya maendeleo.”

Siwalaumu kwa kufanya hivyo na wengi wamefanya hivyo. Sishangai kuwa wamefanya hivyo, lakini ninasema ni chaguo baya. Pengine kuchagua ubepari si jambo la kushangaza kama vile kuchagua ujamaa kwa kuwa vyama vya ukombozi vya Afrika ukiacha vile vilivyoko kusini mwa Afrika hivi sasa vilikuwa na siasa moja tu: kupata uhuru. 

Zaidi ya hapo hatukusema hasa nini tutaendelea kufanya: tulitaka kujitawala wenyewe, basi! Hatukutaja siasa maalumu kwa nchi zetu zaidi ya kujikomboa kutoka kwenye ukoloni. Kwa hiyo kujikomboa kutoka kwenye ukoloni halafu kukubali mtindo wa mkoloni si jambo la kushangaza sana au hata kutoeleweka, ni baada ya hapo unapoanza kujiuliza, lakini kweli huu ni uhuru?

Je, hii inaweza ikaleta uhuru kwa watu wetu?  Uhuru huu ni wa nani? Hili swali nafikiri huwa rahisi kuliuliza baada ya kujitawala kuliko kabla. Baada ya kujitawala watu wangesema: “Je, haya ndiyo tuliyopigania?” 

Lakini wakati wangali wakipigana walikuwa wakipigania kujitawala tu na hawakusema nini kitakuja baadaye. Kwa hiyo mtu hashangai kuwa nchi zetu za Kiafrika zimekwenda kibepari. Lakini mimi nitashangaa nikiona zimefanikiwa, nitashangaa sana, kwa kuwa umma utaukataa ubepari.

Lakini mimi nitashangaa nikiona zimefanikiwa, nitashangaa sana, kwa kuwa umma utaukataa ubepari. Umma utauliza: “ Hivi kweli hii ndiyo maana ya kujitawala?”  Ninasema kuwa ubepari Afrika utapingana na uhuru  na kujitawala, utapingana na hisia ya uananchi kwa vile ubepari wa  madola ya dunia hautaruhusu uzalendo; zaidi ya hapo utapingana na uhuru wa kibinafsi kwa vile ubepari hautakubali usawa hata katika nchi inayojitawala yenyewe. Ingawaje sishangai kuwa nchi za Kiafrika zimechagua ubepari, nitashangazwa sana ikiwa ubepari huu utakubaliwa na umma.