MAFANIKIO YA OSHA KATIKA MIAKA MINNE YA JPM

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.

Imetimia miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, ilipoingia rasmi madarakani. 

Sote tutakumbuka kwamba awamu hii ya uongozi iliingia kwa kishindo kikubwa huku ikijipambanua kuwa na nia ya dhati ya kuwainua Watanzania wengi maskini kutoka kipato cha chini hadi cha kati kwa kuimarisha uchumi wa nchi kupitia maendeleo ya viwanda.                                   

Si jambo la kushangaza kama ukisikia kwamba watu wengi hawakuamini kama maono haya ya serikali ya awamu hii yangeweza kutimia siku moja hadi hapo walipoanza kushuhudia kwa vitendo mikakati na hatua mbalimbali zilizoanza kuchukuliwa na rais wetu ambazo zilionekana wazi kwamba zinalenga kuleta mageuzi makubwa katika uchumi wa nchi na maisha ya Mtanzania.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kubana matumizi ya serikali na kupanua wigo wa ukusanyaji mapato ili kupata fedha za kuendesha shughuli za serikali, ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kasi hadi sasa. 

Miradi hiyo ni kama ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway), upanuzi wa viwanja vya ndege, sambamba na ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL), uboreshaji wa sekta ya afya na ujenzi wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara, utoaji wa elimu bure na mengineyo. 

Hayo ni baadhi tu ya mambo makubwa yaliyotekelezwa na ambayo yanaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayosimamiwa na Rais wetu mpendwa Magufuli. Baada ya kuona japo kwa muhtasari mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika miaka minne iliyomalizika, tuangazie mchango wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika mafanikio hayo katika kuilinda nguvu kazi ya taifa ambayo ndiyo kiini cha mafanikio ya nchi yoyote. 

Kwa wasomaji ambao hawajawahi kupata fursa ya kuifahamu OSHA kabla ya hapa, niwafahamishe kwamba, OSHA ni Wakala wa Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). 

Taasisi hii ina wajibu wa kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vilivyopo katika sehemu za kazi ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa na ajali. Wajibu huu unatekelezwa kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Historia ya OSHA inarudi nyuma hadi mwaka 2001 ambapo ndipo ilipoanzishwa chini ya Sheria Na. 30 ya Wakala wa Serikali ya mwaka 1997 kama sehemu ya Mpango wa Maboresho katika utoaji wa Huduma za Serikali kwa wananchi. Makusudi ya kuanzishwa kwa OSHA ni kupata chombo cha serikali kwa ajili ya kusimamia Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Ili kutimiza lengo la kuanzishwa kwake, OSHA ina jukumu la kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira ambayo ni salama na yenye kulinda afya zao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa katika kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi. 

Kwa sasa OSHA ina ofisi katika kanda sita zinazohudumia nchi nzima. Kanda hizo pamoja na mikoa yake kwenye mabano ni pamoja na Kanda ya Pwani (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro), Kanda ya Kati (Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma), Kanda ya Ziwa ( Mwanza, Shinyinga, Simiyu, Mara, Geita na Kagera), Kanda ya Kaskazini (Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa, Njombe na Iringa) na Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma). Taasisi hii ina majukumu makuu manne:

· Kusimamia Utekelezaji wa Sheria Namba 5 ya mwaka 2003 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

· Kushauri serikali kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, kuhusiana na sera, kanuni na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa Usalama na Afya nchini, ikiwemo kushauri namna ya kuridhia mikataba ya kimataifa kuhusu masuala ya Usalama na Afya.

· Kuongeza uelewa miongoni mwa wadau kuhusiana na masuala ya Usalama na Afya kwa kutoa mafunzo mbalimbali, ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau.

· Kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usalama na afya katika sehemu za kazi ili kuweza kushauri serikali namna bora ya kutekeleza sheria tajwa. 

Ili kufikia malengo katika utekelezaji wa majukumu tajwa, Wakala hufanya shughuli mbalimbali zikiwemo kusajili sehemu za kazi, kufanya ukaguzi wa jumla (General Inspections), kufanya ukaguzi maalumu (specific inspections), mfano ukaguzi wa usalama wa umeme, vyombo vya kanieneo (Pressure vessels) na ukaguzi wa vifaa vya kunyanyulia vitu vizito (Lifting appliances). 

Kazi nyingine ni pamoja na kutathmini hatari zilizopo mahali pa kazi (Risk assessment), kufanya mapitio ya michoro na majenzi ya sehemu za kazi, kufanya uchunguzi wa afya na magonjwa kulingana na kazi husika mahali pa kazi, kufanya uchunguzi wa ajali (accident investigation), kufanya tathmini ya athari za kimazingira (Industrial hygiene surveys and measurements), kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi.

Gazeti hili lilipiga hodi katika ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ili kufahamu ni mafanikio gani ambayo OSHA imeyapata katika jitihada zake za kuboresha hali ya Usalama na Afya katika maeneo ya kazi kwa kipindi hiki cha miaka minne ya serikali ya awamu hii ambapo lilifanya mahojiano na Kaimu Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda, ambaye alitoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na suala husika. 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mkuu wa taasisi, OSHA ina mambo mengi ya kujivunia ndani ya kipindi hiki cha miaka minne ya Rais Magufuli. Bi. Mwenda ameeleza kuwa OSHA imefanikiwa kwa kiwango kutekeleza malengo yaliyoanishwa katika mpango mkakati wake wa miaka mitano hususan lengo kuu ambalo ni kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi. 

“Kupitia uongozi makini wa Mh. Rais pamoja na wasaidizi wake na sisi kama taasisi ya umma tumeweza kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi na maono ya uongozi wa juu ambapo kwa kipindi hicho tu tumeweza kuyafikia maeneo mengi zaidi kwa kuyasajili, kuyafanyia kaguzi, kupima afya za wafanyakazi pamoja na kutoa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi,” amesema Kaimu Mtendaji Mkuu na kuongeza:

“Kwa mfano: kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sehemu za kazi zipatazo 16,457 zilisajiliwa ukilinganisha na 3,354 zilizosajiliwa kwa mwaka 2016/17, sawa na ongezeko la asilimia 390. Aidha, kaguzi 137,938 zilifanyika ukilinganisha na kaguzi 85,491 zilizofanyika mwaka 2016/2017, sawa na ongezeko la asilimia 61.3 kama zinavyoonekana katika chati hapa chini. Hivyo, ongezeko hili katika usimamizi wa sheria linamaanisha kwamba sehemu nyingi za kazi zimefikiwa, kaguzi zimefanyika, tathmini ya afya imefanyika kwa wafanyakazi walio wengi, hivyo kuendelea kuimarisha hali ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Aidha, Bi. Mwenda amesema mafanikio mengine ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kiutendaji na usimamizi ndani ya taasisi ambayo imesaidia kuondoa urasimu katika utoaji wa huduma, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji. 

“Katika kulifanikisha hili tulifanya mapitio ya mlolongo wa biashara (Business Process Review) ili kubaini maeneo yanayoleta urasimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na kupitia mapitio hayo OSHA imefanikiwa kupunguza muda wa kutoa cheti cha usajili wa sehemu ya kazi kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na muda ya kushughulikia leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kutoka siku 28 hadi siku tatu baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu”, amefafanua mkuu huyo wa taasisi.

 Akifafanua zaidi kuhusu uboreshaji wa mifumo, mtendaji mkuu amesema ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kiteknolojia na mabadiliko ya kimahitaji, OSHA imeshaanza kusimika mfumo wa Tehama ujulikanao kama “Workplace Inspection Management System (WIMS) ambapo kupitia mfumo huo, usajili wa maeneo ya kazi utaanza kufanyika kwa njia ya kielektroniki. 

Aidha, kupitia mfumo huu waajiri ama wamiliki wa sehemu za kazi wataweza kuingiza taarifa zao zinazohitajika bila kufika katika ofisi za OSHA pamoja na kujifanyia tathmini ya namna walivyokidhi viwango vya usalama na afya (Self Assessment), hivyo kurahisisha upatikanaji wa vyeti na leseni. 

Mafanikio mengine yaliyoelezwa na Bi. Mwenda ni pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ambapo amesema OSHA ina mkakati endelevu wa kuwajengea uwezo watumishi wake akitolea mfano wa mafunzo yaliyotolewa kwa wakaguzi wa OSHA wa nchi nzima hivi karibuni.

 “Wiki mbili zilizopita tulikuwa na mafunzo kwa wakaguzi wetu wote ambayo tulishirikiana na taasisi ya kimataifa ya WHWB (Workplace Health Without Borders) yenye makao yake makuu nchini Canada. Mafunzo haya yalifanyika hapa nchini na kupitia utaratibu huu, tumeweza kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kugharamia mafunzo ya wakaguzi hawa nje ya nchi. Aidha, mafunzo haya yatawawezesha wakaguzi wetu kutambulika kimataifa, hivyo kuongeza hadhi ya OSHA katika masuala ya Usalama na Afya kimataifa,” ameeleza Kaimu Mtendaji Mkuu.

Aidha, ameeleza kuwa OSHA imefanikiwa kuanzisha dawati la kupokea kero, maoni na mrejesho kutoka kwa wadau kwa lengo la kuzishughulikia kwa wakati katika kuboresha huduma zao.

Orodha ya mafanikio ya OSHA haikuiacha sekta isiyo rasmi kama ilivyoelezwa na Mtendaji Mkuu huyo katika mahojiano. 

“Tumekuwa na mkakati endelevu wa kuifikia pia sekta isiyo rasmi, hasa kwa kuzingatia kuwa sekta hiyo ndiyo inayoajiri watu wengi na ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi. Ni jambo la kawaida katika nchi nyingi zinazoendeleo kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya sekta hiyo kukua, hasa ukizingatia kuwa msingi wa kukua kwa uchumi wa ndani unategemea kukua kwa sekta hii,” ameeleza. 

Pamoja na umuhimu wa mkubwa wa sekta hii katika maendeleo ya nchi, lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo mazingira hatarishi na yasiyo rasmi katika kuendesha shughuli zao.

“Baada ya kufanya tathmini ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ndipo OSHA ikaona kuna umuhimu wa kuanzisha programu maalumu ya kutoa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi katika sekta isiyo rasmi. Mafunzo haya hugharamiwa na serikali ikiwemo kupatiwa vifaa kinga kutegemeana na aina ya vihatarishi vinavyoendana na shughuli wanazozifanya,” ameeleza.

Taarifa iliyotolewa na OSHA kwa umma hivi karibuni inaonyesha kuwa jumla ya wajasiriamali wadogo 28,275 walinufaika na programu hii ya mafunzo katika mikoa ya Tabora, Mtwara, Ruvuma, Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, Iringa, Shinyanga, Pwani, Songwe, Singida, Kilimanjaro, Rukwa na Dar es Salaam. 

Kimsingi jukumu la OSHA ni kupunguza ajali na magonjwa katika sehemu za kazi, lengo hili la msingi linatakiwa kwenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini. 

Katika kutekeleza hilo, OSHA kama taasisi wezeshi kwa wawekezaji na wafanyabiashara ilifanya utafiti na kubaini uwepo wa baadhi ya tozo zaidi ya sita zilizokuwa zikilalamikiwa na wawekezaji. Tozo hizo zilionekana kuongeza gharama za uendeshaji, hivyo kufanya ushindani wa kibiashara kuwa mgumu, hivyo kusababisha waajiri wengi kutojisali na OSHA. 

Hivyo OSHA ilipendekeza kufutwa kwa tozo hizo ambapo serikali sikivu inayoongozwa na Mh. Magufuli iliridhia kwa kufanya marekebisho kupitia GN. 719 ya tarehe 16 Novemba 2018 ambayo ilifuta tozo mbalimbali zikiwemo ada ya usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 1,800,000; Ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh. 2,000; Faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto ya Sh. 500,000 ambayo ilikuwa inaingiliana na taratibu zinazosimamiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Tozo nyingine ni ada ya leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama iliyokuwa inatozwa Sh. 200,000 kwa mwaka; na Tozo ya ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya ya Sh. 450,000 kwa saa kwa mtaalamu mmoja. Mabadiliko haya katika tozo ndiyo ambayo yameleta ongezeko la sehemu za kazi zilizosajiliwa katika mwaka huu wa fedha kwa zaidi ya asilimia 390.

Aidha, Bi. Mwenda amesema kwa sasa taasisi yake imeimarisha ushirikiano kati yake na taasisi nyingine za serikali ambazo zinawahudumia wafanyabiashara na wawekezaji hususan katika kutambua maeneo ya kazi na kufanya kaguzi za pamoja pale inapobidi.

Tukiwa tunahitimisha mahojiano yetu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema: “OSHA tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wetu mpendwa, Dk. Magufuli, ambazo zinalenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kumkomboa Mtanzania wa kipato cha chini kwenda kipato cha kati. Sisi kama taasisi ya serikali tunatembea katika nyayo zake kwa kuendeleza mchango wetu katika maendeleo ya nchi, hususan katika kipindi hiki ambapo nchi inajenga uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha kwamba ongezeko la viwanda na sehemu nyingine za kazi nchini halileti athari za kiusalama na afya miongoni mwa Watanzania wote.”