Wiki iliyopita Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, katika mahojiano maalumu na JAMHURI alizugumzia maendeleo yaliyopatikana katika bandari za maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Katika sehemu hii ya tatu ya mahojiano hayo anazungumzia mikakati ya Bandari kuongeza wateja na ushirikiano na taasisi nyingine unavyotekelezwa. Endelea…

Swali: Mkurugenzi Mkuu umezungumza kuhusu mzigo katika Bandari ya Dar es Salaam tani milioni 17, hujatueleza bandari nyingine ulizozitaja za Maziwa Makuu zina mchango kiasi gani? Maana kuna Ziwa Victoria, kuna Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa… Lakini pia sijasikia kama una mpango wa kuweka reli tusije kuharibu barabara.

Mhandisi Kakoko: Mchango wa bandari nyingine. Niligusia gusia pale, sikutaka kutaja kila moja na asilimia zake. Kwa sababu nilitaka kule mbele nije nizungumzie shehena, kwa sababu tulikuwa tunataja bandari. Bandari inayofuata baada ya Bandari ya Dar es Salaam, ni Bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga uwezo wake kwa wastani ni tani milioni 1, kwenda mpaka, kwa kununua vifaa milioni moja na nusu inaweza ikafika, na ndiko tunakotaka iende, mpaka 2.

Sasa, wao mzigo wao kwa wastani wakati Bandari ya Dar es Salaam inafanya kwenye tani milioni 14, wao wanakuwa kwenye milioni 1, moja na nusu na Mtwara ambayo inafuata, ambayo ina uwezo wa tani 400,000 kwa sasa baada ya kujenga gati lile la pili na kuongeza mitambo, inakwenda kwenye tani milioni 1. Na mpaka sasa ilikuwa ikijitahidi inakwenda mpaka tani hizo 400,000. Mara ya mwisho imefanya karibu tani 390,000.

Ni kipindi kile ambacho tulisikia, mpaka mbuzi walikunywa soda, korosho ikawa ya kutosha. Ndiyo tulifanya kazi usiku na mchana, ilibidi tupeleke na mitambo, ilienda, kufikia uwezo wake kamili wa tani 400,000. Tangu ilipojengwa mwaka 1953, ilikuwa haijafikia uwezo huo. Lakini baadaye ilikwenda chini kidogo na sasa imerudi kwenye eneo lake.

Na tunadhani itakwenda kwenye tani milioni 1, pengine kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2019/2020, inaweza ikaenda mara mbili au baada ya miaka miwili ikafika milioni moja kwa sababu, baada ya gati hili la pili lakini tumepata shehena ya makaa ya mawe, ipo kampuni imeahidi inaweza ikaleta mpaka tani 600,000. 

Na tumeingia makubaliano na Dangote, kwamba kama watakuwa na mzigo kwa mwaka wanafikia tani 1,000,000, basi kunaweza kukawa na punguzo kidogo kwenye bei, tukagawana kwenye ule wingi, biashara ya jumla hii. Kwa hiyo Dangote nao wameahidi, wataanza kidogo na tuna matarajio kwamba mpaka Juni, si ajabu labda tukafikia kwenye tani 6, saba, nane pale Mtwara.

Eheee, Mwanza kwa maana ya Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na Ziwa Nyasa, Itungi kwa pamoja nazo zinakwenda kwenye wastani wa tani milioni 1. Kwa hiyo mkiangalia vizuri, haya maeneo matatu ndiyo yanayotengeneza tani milioni 3. 

Ukija kujumlisha zile 14 za Dar es Salaam, wanakwenda kwenye 17.1, ambayo ndiyo rekodi tuliyokuwa nayo, na tumepanga mpaka Juni mwakani, tuwe na uwezo wa kwenda mpaka tani milioni 18. Ndilo lengo letu ambalo tumejiwekea.

Hii inatoka kwenye wakati ule wa mdororo, mlipokuja mkaona bandari kama iko wazi wazi hivi, na wengine mlichukua mpaka picha pale, mkasema hii ndiyo bandari. Na Mheshimiwa Rais alisema, hata kama itakuja robo meli ilimradi ilipe kodi, wengine acha waende tu. 

Lakini ninadhani baada ya kuwa wamezoea sasa, tumetoka tani milioni 14, kwenda tani milioni 18 ndani ya miaka 4, kwa hiyo tunakwenda kwa wastani wa tani milioni 1.1 kwa mwaka, ambayo si mbaya sana, ingawa tunakusudia sasa baada ya pale tuweze kwenda zaidi. Kwa hiyo mchango wa bandari nyingine, unaweza kusema kwa haraka haraka ni 3/17 kwa sasa, kwa pamoja kwa uzito ambao nimeutaja.

Umezungumzia mpango sasa ukoje kuwa na, kwa kuwa tunafanya ushirikiano na watu wa reli na tunafanya kazi pamoja na ni ukweli. Na huko nyuma kwa wale, sijui kama kuna mzee sana zaidi yetu hapa alikuwepo mwaka 1977 kabla ya THA, tulivyoachana. 

Ni kweli kwamba tulikuwa shirika moja, reli na bandari tulikuwa shirika moja, na ndivyo kama ilivyo, ukizitenganisha reli isije mpaka bandarini, hujafanya kitu. Hiyo reli haina kazi kwa hapa Tanzania. Na kuweka reli ukainyima bandari kabisa kabisa, sawa malori yapo, lakini inapofikia uzito mkubwa, kwa malori ni gharama kwa jamii, ni gharama kwa nchi. Kwa sababu wenye malori na wenyewe ukiwauliza hawapendi hivyo. Kwa sababu wanasafirisha mzigo kwa bei kubwa kwa sababu ya umbali. Ipo mizigo na umbali unaofaa kwa malori, na ipo mizigo na umbali unaofaa kwa reli.

Kwa hiyo, upande wa Ziwa Nyasa, au Kusini Mtwara Corridor ule mradi wa reli unaendelea, ehee tunajua wote kwamba ule upembuzi yakinifu ulikuwa umekamilika, unajua gharama na kila kitu sasa hivi yanafanywa mapitio upya, ili ikiwezekana kuja kufanya uwekezaji kati ya serikali na sekta binafsi, kwa utaratibu ule wa Public Private Partnership (PPP).

Kwa hiyo iko timu sasa hivi inaendelea na TPA ni sehemu ya kamati hiyo kwa ngazi ya wataalamu, ngazi ya watendaji wakuu sisi, chini ya wizara, shirika la reli linafanya kazi hiyo, na sisi tunashirikiana nao, kwa sababu watatumia bandari za Mtwara, wanaweza wakatumia ya Mbamba Bay, kwa sababu wanaangalia kule Manda na Liuli, kama itakuwa lazima kwa sababu ya miinuko, hasa kwa ajili ya machimboya Liganga inawezekana wakatumia zaidi kule.

Kwa hiyo huu ushirikiano upo, na tunapofanya kazi kwa pamoja, labda nisema na Marine Services Limited, kwa upande wa soko la Uganda. Kama mnavyojua, tumefanya kazi kwa pamoja wote tumerekebisha bei zetu ili tuweze kushindana, kwa sababu Dar es Salaam na Kampala, kupitia bandari za Mwanza na Portbell, tunao uwezo wa kufikisha shehena iliyotoka Dar es Salaam, tunapoanza treni kutembea hapa tukaingia kwenye maji, pale Mwanza, tukatokea kwenye maji, kilomita 9 tukaingia Kampala kwa reli kwa muda wa siku 4, ambazo mshindani wetu yule mwingine hawezi hata angefanya nini.

Sasa hiyo ndiyo faida kubwa ambayo tunayo. Na tukaamua kupunguza bei kutoka tozo za bandari, mpaka bwana TICTS pale tukamwomba akapunguza, tukakubaliana tusiingize kwenye tozo za meli za demurrage kwenye mabehewa. Mkubwa kabisa, mkubwa wetu ni shirika la reli, kwa sababu yeye ndiye anatumia, ndiye kwenye kazi kubwa zaidi, kwa sababu yeye ndiye anasafirisha kilomita nyingi, akapunguza. Ehee, Marine Services Company Limited wakapunguza. Tukapata bei iliyokuwa sawa na wezetu Wakenya, kutoka Mombasa, inavyohudumia kontena ya Uganda.

Tukasema tuanze, muda sisi safi, wao siku saba, sisi siku nne. Bei, sawa sawa. Sasa tukapata wateja mpaka wakatuzidi, bahati mbaya kama nilivyosema, wezetu wa shirika la reli bado wanajenga uwezo. Serikali imewapa fedha Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 4 kupitia Hazina, wanafufua mabehewa. Tukiyapata yale sasa hivi nafikiri wamefika mbali, tutaweza kurudi kwenye biashara ile ya Uganda, kwa sababu baada ya pale kwa kweli wateja hatukuwahudumia vizuri, na wengine waliondoka tukabaki na wachache.

Tulikuwa tumeishatoka kwenye asilimia 2, tumekwenda kwenye asilimia 4. Wale waliokuwepo miaka ya 2008 mpaka 2013, Uganda kwenye Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na market share ya asilimia 10. Mzigo ulikuwa ni tani milioni 4, tulikuwa tunaweza kusafirisha tani 400,000. Sasa hivi tumerudi kusafirisha tani 300,000 hivi au tani 200,000 kwenda 260,000 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 2 au 3, baada ya wateja wengine kuwa wamejiondoa.

Tulichukua mizigo mingi kutoka kwa jirani zetu, ikahamia kwetu na tuna mpango wa kuirudisha kwa sababu tunajua changamoto za uwezo wa reli zitapungua, hata kaba ya Standard Gauge, zitarudi. Lakini ukiishakaa muda mrefu kwa sababu mizigo imekosa usafiri, basi tukawa na changamoto ya kisheria ya TRA. Baada ya siku 30 kuna tozo za VAT na Customes Warehousing Rent (CWR). CWR ile nayo kidogo haikuwapendeza wateja wetu, imewaondoa.

Kwa hiyo tumeomba, uongozi mpya wa TRA, tukae tuongee. Basi inapotokea sisi ndio tumemwita mteja, tumemwondoa kwenye bandari yake nyingine akaja hapa, basi tusimpe adhabu, maanake ndiyo biashara. Kwa hiyo wote tutoe mchango kwa sababu tutakachokipata ni kikubwa kuliko hiyo tozo ndogo. Kwa hiyo tutakapofikia maafikiano, ambayo yanaendelea katika ngazi za mawaziri, na tuna imani tutafikia, basi tutarudi tena Uganda, ambapo tunataka angalau turudi kwenye asilimia 5.

Na sasa hivi Uganda mzigo wake ni tani milioni 8. Tangu 2013 kuja leo, wame-double mzigo wao unaopitia kwenye bahari. Kwa hiyo sasa kwenye tani milioni 8 sisi tunafanya, sisi tunafanya tani laki 3, hata milioni 1 haifiki, kwa kweli ni aibu, na haifai, na haikubaliki, lazima wote tukae chini tufanye hiyo kazi. Reli, TRC, Marine Company Services Limited, TPA na washirika wake kama TICTS, lakini na mamlaka zote mbili zinazohusika na mapato na kodi kwa maana ya TRA na URA.

Na kwa kuwa marais wetu, viongozi wetu, viongozi wakuu, wamekutana wamezungumza, sisi wajibu wetu ni kutekeleza, hatupaswi kushindwa. Hii changamoto ninayo imani ikifika Januari, tutakuwa tumefikia maafikiano na taratibu zote ili tuweze kurudisha mzigo wa Uganda. 

Sasa mimi sitaki kusema mengi, mengine ni siri za biashara. Najua kuna swali limeulizwa hapa, lakini kwa ufupi, kwa ufupi, tukijaribu kufunga Uganda, Rwanda tumeishachukua, tulikuwa sisi tuna asilimia 60, washindani wetu 40, sasa tuna asilimia 84 katika soko la Rwanda, na ninakimbia kwenda 90, mpaka ifike Juni, biashara ya Rwanda asilimia 90 iwe kwetu.

Na nikimaliza kuchimbia Bandari ya Tanga mwakani, basi bidhaa ya Rwanda lazima niende kwenye 95. Burundi tumeishachukua asilimia 99. Robo ya mwisho ya mwaka 2018/2019, bidhaa ya Burundi asilimia 99.2 tulihudumia sisi, kutoka kwenye asimia 65 kwa 35. Jirani zetu walikuwa na asilimia 35, sisi 65, sasa tuna asilimia 99.2. Kwa hiyo tunaendelea na juhudi hizo. Vile ni vinchi vidogo vingine, na vina mizigo midogo, lakini Rwanda ndiyo nchi ya tatu kwa sehena tunayohudumia.

Baada ya asilimia 35 ambazo tunazipata sasa kutoka DRC, na Zambia asilimia 30, Rwanda tuna karibu asilimia 20. Kwa nini sasa, wao ni hub. Wao wanakusanya mizigo kutoka kwa jirani zao. Sasa wapo watu humu ndani wanasema, wengine viongozi wetu, kwamba tunaanza kutanguliza reli kwenda Rwanda badala ya Kigoma kuingia, hawaelewi.

Kwa sababu kama Rwanda akifanya udalali wa kukusanya shehena ya Congo, Burundi udalali, mimi nikahakikisha kwamba shehena zote za Rwanda na Burundi haziingii bandari nyingine zaidi ya bandari za Tanzania, nani amefaidi? Kwa hiyo yule anakuwa agent wa TPA. 

Kwa hiyo tunaweza tukawafanya majirani wakawa ma-agent wa TPA. Mbaya ni kwamba wakikusanya wakapeleka nchi za jirani. Na kwa sababu DRC ndo ina mzigo mojawapo mkubwa, sisi tunachotaka sasa ni kuhakikisha, ndiyo nilitaka nisingie ndani sana… kwa hiyo sisi peke yetu ndiyo tunaweza kuingia DRC.

Kuanzia Uganda, Rwanda na Burundi yule mwingine atakuwa hawezi. Wakikusanya zile shehena, zinapitia Dar es Salaam, zinapitia Tanga. Nadhani mmenielewa. Kwa sababu watafahamu… kwa hiyo anayesema kuwa sisi tunapita Rwanda, tunapita Burundi, inasaidia nini? Hawaelewi kwamba maana yake tunafanya biashara ya Congo.

Kwa hiyo sisi tutaendelea kwenda na Uganda, na hasa Masaka, kwenda Mbarabara, maeneo ya Magharibi, kwa sababu maalumu, huyu yeye abaki aende Kaskazini huko, ambako nako wana bandari… kwa hiyo lile swali lililokuwa linaulizia ushindani, eneo mojawapo ni hili, lakini lile swali lililokuwa linaulizia kwa nini tunashirikiana na reli?

Reli na bandari ni kampuni moja, pamoja na kwamba ni mashirika mawili. Kusaidia reli kuongeza ufanisi. Kama ninavyosema hapo juu, tayari shirika la reli linaboreka, lakini tunataka kuwe na vichwa zaidi. Shehena kwa ajli ya nchi za nje, kwa ajili ya mzigo unaopita, transit, ukiacha shehena ya ndani, sisi peke yetu tunahitaji vichwa visivyopungua 40. Vichwa vya treni kwa sasa. Kwa hiyo ni kama tunahitaji vichwa vyote ambavyo vipo. Sasa kwa sababu shehena kubwa ni ya ndani, kama mnakumbuka hesabu kubwa nilizofanya karibu theluthi mbili, bado ni biashara ya ndani ya nchi.

Theluthi moja, ndiyo inayokwenda nje, kwa hiyo wanahitaji vichwa vingi bado ndani, kwa hiyo ukiangalia ukweli wanahitaji vichwa vingi sana zaidi ya 100, na siwezi kuwasemea, nina hakika kwamba wana asilimia fulani, lakini bado. Kwa hiyo sisi tukaona ni vema tuchangie vichwa vya shanting, vichwa vya kupeleka mzigo.

Ukijua kwamba tuna Bandari Kavu ya Kwala – Ruvu itahitaji vichwa, tutatumia treni zaidi, na tuna Bandari Kavu ya Ubungo, ambayo tumeirudisha baada ya mazungumzo, tumeirudisha kutoka TICS, tunaihudumia wenyewe, iliachwa bila kazi miaka mingi, iliachwa tu ikatupwa, sasa karibu tunaijaza. Na tukiwa na vichwa vile, basi nitakuwa na nafasi ya kutosha bandarini. Na ndiyo biashara hiyo tunafanya.

Vile vichwa, vinanunuliwa na TRC ndio wataalamu specification, wataviendesha, lakini kimsingi vitakuwa ni vya TPA mpaka pale ambapo tutakuwa tumerudishiana hela hiyo, kwa sababu sisi ndiyo tutakaokuwa tunavikodi. Tukivikodi, tutafanya hesabu jinsi ya kurudishiana hela. Maana wanavyo wao kwa ajili ya kuviendesha kwa niaba yetu. Wateja wao ni sisi, sisi wenyewe.

Kwa hiyo unauona utaratibu ambao ni mwepesi kuliko tungewaacha, halafu hatuwezi. Kwa hiyo tutakuwa na uhakika wa kuhakikisha kwamba Bandari ya Dar es Salaam, kila mara shehena inavyofika, kwa zile za Dar es Salaam, siwezi kuzipeleka Ruvu halafu zirudi Mwenge, zirudi Tegeta, zirudi mjini katikati. Lazima zitakuwa maeneo ya Ubungo, na zile nyingine ambazo ni za mikoa ya Pwani, kwenda mbele na za nchi za jirani, zitakuwa Ruvu.

Kwa hiyo tunahitaji vichwa hivyo, na sasa hivi ninavyozungumza nadhani matengenezo yako zaidi ya asilimia 50 na kwa bahati nzuri, hii serikali msiichezee bwana. Bei ya vichwa vitano, tumepata saba. Iko serious, kwa hiyo story ya vichwa vitano ni ya wakati uleeee.

Kwa hela ile ile, kwa hiyo sasa tumepata vichwa saba. Kama ambavyo mlisikia vichwa vile vingine vya treni, wali-save karibu dola milioni moja moja, kwa kufanya mazungumzo. Kwa hiyo, hili la vichwa liko pale pale, na nina uhakika mwakani vitakuja na tutakuwa busy kiasi kwamba, ninadhani pale ambapo reli na magari yanakatiza kwa pamoja, itabidi tuongeze na foleni kwa sababu, tutakuwa busy kweli kweli. Tutakuwa na lazima treni nne, tatu, tano, zinatoka kwa siku kutoka bandarini, si jambo la kawaida.

Kwa nini tutakuwa meli zinatoka tunaendelea kuzilinda… kimsingi zinapokuwa zimetoka nje, na zinasubiri, zinakuwa chini ya ulinzi wao wenyewe, na wanakuwa nje zaidi. Kwa hiyo wanaweza wakafaidi ulinzi lakini sisi hatutafika kule walipo, hawawezi kuchanganyikana na hizi zinazosubiri kuingia ndani.

Meli zikiingia, mara nyingi zinakuja kukamilisha nyaraka zake, documentation, hizo ziko chini ya ulinzi wetu na zina mali zetu. Anapomaliza anawajibika kuondoka, sasa ukweli ni kwamba, eneo la Kaskazini si salama sana. Kwa majirani zetu, na wanapopata safari ya kwenda kule, kama hawaja-clear, clear, vizuri mara nyingi wanasubiri huku. Kwa hiyo hilo lipo, kwa sababu yeye ameishakunywa maji, amekunywa mafuta, amepakia chakula, sasa kwa sheria za kimataifa akiishatoka nje pale, huwezi kumfukuza.

Na hata akipata matatizo akivamiwa ana haki ya kukimbia na kurudi, hizo ndizo sheria za kimataifa, kuhakikisha usalama. Kwa hiyo kimsingi ni wao wanaokuwa wanajilinda, lakini kwa sababu ya biashara, na pengine hii nayo inatuongezea biashara, ile Bandari salama. Inasababisha hata kama amemaliza anataka kutoka lakini anajisikia yuko salama, basi atakuletea mzigo siku nyingine kwa sababu anapiga mahesabu akimaliza anajua ataondokaje, basi anajua atakaa pale.

Kwa hiyo sisi hatuna ugomvi nao, ingawa hawawezi kusema kwa kuwa wameishaondoka, basi watushitaki kwa kuwa wamevamiwa.

Kuna swali kuwa sasa kama tunasukumiwa lawama tunafanyaje? Niseme jambo moja tu, kile ambacho nimekitamka wakati ule nikirudie. Serikali si moja? Serikali ni moja. Na kama nilivyosema mwenyeji ni TPA. Kwa hiyo sisi inakuwa kama familia. Akija mgeni pale, huko mko na baba, mko na mama dakika 10 mlikuwa chumbani pale mnakwaruzana, mnaonyesha barabarani? Kwa hiyo inabidi tu, tuendelee kufa kidume tu hivyo hivyo.

Tutabeba hiyo lawama, tutaifafanua, huwezi kwenda kwenye vyombo vya habari ukasema hii si mimi ni TRA. Inawezekana? Kwa hiyo sisi tutakubali na tutarekebisha, lakini serikali kule ndani itajua, kwa sababu linakuwa jambo la ndani. Kwa hiyo tutakwenda hivyo, linakuwa jambo la ndani. Kwa hiyo kama nilivyosema awali, tumejaribu kidogo wadau, serikali ni wadau wetu, nyie ni wadau wetu, ataangalia na sisi tutakuwapo tutaeleza.

Wananchi ni wadau, kama hivi ninavyosema hapa, tumejaribu kutoa hii elimu, kusudi hata Mhe. Waziri wa Maliasili kama anakuja na kuna tatizo la utendaji, basi haidhulu, yeye atakutana na watu wake, ataeleza na sisi tutakuwepo, basi akimaliza anaweza akawaomba nyie mkaenda mkazungumza ofisini kwake. Na yale mazingira ni ya ofisini, na hoja inayozungumziwa.

Yupo mwandishi mmoja nimempenda, yule amefanya professional news making, sikumbuki ni gazeti gani, hii niliyokuwa naisema ya NEMC, alieleza vizuri, kwamba maofisa fulani, walileta kitu fulani, katika ofisi yao iliyo bandarini. Hiyo ndiyo kweli ni sawa. Lakini sasa wakati ule ilikuwa “TPA tena, waharibu mazingira”, sasa ukiangalia nadhani mnanielewa inakuwa tofauti.

Kwa hiyo ninachofanya sana sana ni ile tu kuelewa, waziri anakuja anafanya kikao mle, akitoka anaomba waandishi anawaeleza labda, basi taasisi yangu fulani haijafanya vizuri, lakini bado sisi tunahusika. Kwa sababu nilikuwa ninazungumzia faida ya bandari mojawapo, ni kuhakikisha wateja hawabughudhiwi. Kwa hiyo kuna wakati sisi tunaweza tukapingana na taasisi mwenzetu ndani ya Bandari, kuhakikisha mteja anahudumiwa.

Kwa sababu wateja wakikauka, inatamkwa bandari na TPA. Mteja akipata shida njiani hata huko katikati, kuna wakati wenzetu huko njiani mambo hayaendi vizuri, wanasimamisha malori hata wanafanya mazungumzo mengine yasiyo sawa sawa, wanasema huko barabarani bwana Tanzania ukitoka bandarani, bandari haina maana kweli kweli wanaomba rushwa njiani.

Sasa wewe rushwa iko Iringa, sasa Bandari ya Dar es Salaam inakujaje tena? Kwa hiyo ni suala la elimu. Na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, tunayo Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama vimekwenda wamefanya semina njiani kote. Ndiyo kazi tunafanya, mpaka kwenye mikoa yote, ambayo vifaa vinakwenda, Mtukula, Rusumo, Kabanga, maeneo yale ya Katosho, ambako tunapita kwenda Burundi, Tunduma pale ambapo mmeona Nakonde jana, kote wamekwenda wamekaa mipakani, ndiyo kazi tunafanya.

Hata kuzungumza na vyombo vingine barabarani tutafanya. Kwa hiyo nadhani ndiyo kitu tutafanya, lakini hatuwezi kwenda kusema: “ahaaa, siyo sisi bwana barabarani, huko ni polisi.” Hatuwezi kusema hivyo. Kwa sababu mteja wa Zambia, yeye anajua Tanzania na Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo tunashiriki namna hiyo.

Ushirikiano na Tazara tunafanyaje kwani ushindani ni mkubwa. Ni kweli kabisa, ushindani ni mkubwa sana. Ushindani ni mkubwa kupindukia, kwa sababu ziko zile nchi ambazo kwa sehemu kubwa tulizisaidia katika vita ya ukombozi, wamekuja baadaye, na bado hawakuwa na amani amani sana, sasa hayo mambo yote yamekwisha.

Ya akina Savimbi yamekwisha, ya akina Afonso Dhlakama yamekwisha. Sasa ni muda wa biashara. Na ndugu zetu, wa katikati, hawa mliokuwa mnaita, tunaitwa Landlocked, wamefungiwa katikati ya ardhi, baadaye wakasema hapana, land-linked, tunaunganishwa. Yaani sisi Zambia tumekuwa linked na Tanzania kwenda baharini. Sasa hivi wanatutumia kama wake wenza. Ni wazuri kweli kutushindanisha, kwa hiyo tunaangalia tunafanyaje, ndiyo swali lenyewe.

Je, unafahamu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imefanya nini katika kuimarisha usalama wa bandari zilizoko chini yake, hasa usalama wa magari? Usikose toleo la JAMHURI wiki ijayo uendelee kusoma mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita.

By Jamhuri