Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imeanza rasmi kazi ya kuwahoji viongozi juu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Wanaotuhumiwa na kuchunguza na TAKUKURU ni Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Amir Said, Mkurugenzi wa Fedha, Mrisho Shabaan na maafisa wengine waandamizi.

Kati ya tuhuma zinazowakabili ni matumizi mabaya ya madaraka, ufujaji fedha na mkakati wa makusudi wa chini kwa chini wenye lengo la kuiangamiza TTCL kwa faida ya kampuni binafsi.


Hatua ya kuwafikisha mbele ya TAKUKURU imekuja baada ya JAMHURI kuripoti ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka uliofanywa na viongozi hao.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliitisha mkutano na wafanyakazi wa shirika hilo wiki iliyopita na kuamua malalamiko ya wafanyakazi yashughulikiwe na TAKUKURU.


Pia Makamba imeitaka Bodi ya TTCL kukaa na kumwandikia barua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya kukagua hesabu za shirika hilo la umma.


Chanzo cha kuaminika ndani ya TTCL, kimeliambia JAMHURI kuwa Meneja wa Kanda ya Kaskazini, Karim Bablia tayari amehojiwa na TAKUKURU kwa nia ya kufafanua shutuma nzito alizomwaga hadharani katika kikoa kati ya wafanyakazi na Makamba.


Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi wa menejimenti ya TTCL wameandaa taarifa zitakazotumika kuwahadaa watumishi wa TAKUKURU kama njia ya kukwepa mkono wa sheria.


“Tumepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi tayari amepigiwa simu na TAKUKURU kwa ajili ya kuhojiwa na chombo hicho.


“Sasa tumeamini kuwa Serikali inafanya kazi kwani tuliambiwa kuwa baada ya kumaliza mkutano Naibu Waziri aliwaita TAKUKURU na kuwakabidhi makabrasha yenye malalamiko yetu nao wameanza kuwaita wahusika,” kimesema chanzo kingine.

 

Katika mkutano huo, Makamba alitaka manejimenti ya Shirika hilo kuitisha kikao cha Bodi ya Wakurugenzi kilichotarajiwa Alhamisi iliyopitakupitisha mapendekezo ya wafanyakazi.


Wafanyakazi katika mapendekezo hayo walitaka kufanyika kwa ukaguzi wa hesabu kupitia Ofisi ya CAG jambo ambalo Bodi haijalifanya kutokana na kikao hicho kuahirishwa baada ya idadi ya wajumbe inayotakiwa kutotimia siku ya Alhamisi.


Wajumbe wa Bodi hiyo waliokosekana ni Mwakilishi, Detecom na MSI, Jaji Joseph Warioba na Mkurugenzi wa Benki ya Mkombozi, Edwina Lupembe.


Makamba katika mkutano huo amesema wote watakaobainika kutumia madaraka vibaya wakati wa uongozi wao watashitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.


Amesema wizara yake tayari imeanza mchakato wa kutafuta menejimenti mpya itakayoongoza shirika hilo ndani ya wiki mbili baada ya kubaini iliyopo haifai.


“Huwezi kuwa na menejimenti yenye uhusiano mbaya na wafanykazi wake hata tukiamua kuingiza bilioni 180 hapa zitakwisha kwani wafanyakazi na menejimenti hawaheshimiani. Zitakwisha zote hivyo ninawahakikishieni kuwa tutakapoonana wiki mbili au tatu zijazo tutakuwa na uongozi mpya,” amesema Makamba.


Hata hivyo, Makamba amesema Serikali iko katika mazungumzo na wawekezaji walipo TTCL inunue hisa zote na kumiliki shirika hilo kwa asilimia 100.

Madai ya Wafanyakazi

Akichangia katika mkutano huo, Meneja wa Mkoa wa Kaskazini, Karim Bablia amesema kuwa katika kanda yake kwa miaka miwili sasa ametakiwa kukusanya Sh bilioni 4.7 ila akavuka lengo na kufikia Sh bilioni 7.9 lakini kila mwaka katika makusanyo kumekuwa na upotevu wa Sh bilioni tatu.


Bablia amesema ametumia mbinu mbalimbali kufuatilia upotevu huo lakini uongozi wa juu umekuwa ukimkatisha tamaa kwa kutoa majibu ya jeuri.


“Nasema hapa hakuna kitu kibaya kama unapewa bajeti unakusanya na kuvuka lengo waliokuwekea, lakini ripoti inayoletwa katika kikao cha mameneja unaambiwa kuwa Sh bilioni 3.5 [kati ya hizo] hazionekani, unauliza unajibiwa kijeuri, hii Mheshimiwa Waziri inakera sana.


“Nimefuatia katika kila idara kupata ukweli wa upotevu huu kwa miaka miwili sasa, lakini napigwa danadana ukifuatilia sana unapewa majibu ya kejeli unambiwa wewe ndo unapenda shirika sana,” amesema Babilia.

 

Amesema shirika hilo lina nafasi nzuri ya kufanya vizuri katika soko, lakini linakwamishwa na menejimenti iliyopo.


“Msheshimiwa Waziri hadi sasa nimepeleka maombi ya modem 600 zinazohitaji kwa wateja nimeambiwa hadi wiki sita hivi.


“Haya niliomba dola 2000 kwa ajili ya kuwafungia simu wateja wetu wakubwa…. ni ni… ni… nani hawa ok….. Benki ya CRDB, lakini naambiwa kuwa dola hizo hazipo. Jamani shirika hili linakwenda wapi? Hadi sasa hawajafungiwa simu hizo wako katika foleni.


“Katika kanda yangu nina wateja 3,600, lakini mtambo uliopo una uwezo wa kuchukua wateja 1,800 sasa nimepiga kelele kwa menejimenti, lakini wameweka pamba masikioni kwa mtaji huu tutaliokoa shirika hili kweli? Wateja wapo tunashindwa kuwahudumia kwa kushindwa vitu vidogo vidogo tu.


“Lakini haya yote nayafanya menejimenti inaniona kuwa sifai baadala yake naambiwa kuwa mie natoa siri ya shirika katika magazeti ninasema mimi ninaijua kazi yangu.


“Kila ninachokifanya nataarifu viongozi wangu mameneja. Machifu jamani, mameneja wenzangu ni uongo? Kama ni uongo mtu asimame hapa na kukataa kama ni uongo. Kila mtu humpa taarifa ya kile ninachodai. Sina haja ya kupeleka katika magazeti mambo ya ofisi.


“Lakini Mheshimiwa Waziri yaliyoandikwa kwenye gazeti sitaki kulitaja ni gazeti lipi hapa [akimananisha JAMHURI] ni kweli tupu. Hakuna hata chembe ya uongo. Kuna kampuni imepewa kazi ya kulinda katika kanda yangu na nyingine hawana askari.


“Hata akiwepo, hana silaha yeyote. Kila siku mie ni mtu wa kwenda kutoa ripoti polisi inayohusu wizi. Sasa nina RB zaidi ya 20. Menejimenti imekaa kimya, tumelalamika tumeshindwa kupata majibu,” amesema.


Akiwasilisha madai kwa niaba ya wafanyakazi, Lucas Ishengoma amesema uongozi wa menejimenti umeshindwa kufanya kazi sasa umebaki kula fedha.


Makamba baada ya kupokea tuhuma hizo nzito aliamua kuzikabidhi TAKUKURU bila kuwapa fursa ya kusikilizwa viongozi wakuu wa TTCL akisema ikiwa wanalo la kujitetea watalitoa mbele ya TAKUKURU.


JAMHURI kwa muda wa mwezi mzima sasa limekuwa likiripoto wizi, uozo na uzandiki unaondelea ndani ya TTCL hali inayolibemenda shirika hilo kongwe la simu nchini.

1011 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!