Wiki iliyopita, Spika wa Bunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alifanya mabadiliko ya nafasi mbalimbali za viongozi wa Kamati za kudumu za Bunge.

 

Habari tuliyochapisha leo inaonesha kuwa Spika Ndugai amechukua hatua hizo kutokana na kuwapo tuhuma zilizoonekana kuwa na ukweli wa baadhi ya wabunge kuomba na kupokea rushwa.

 

Spika Ndugai amefanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa kifungu cha 116 (3) cha Kanuni za Kudumu za Bunge kinachompa mamlaka ya kuteua wabunge na kuunda kamati mbalimbali.

 

Pamoja na kanuni hizo, sisi wa JAMHURI tunaungana na Watanzania wengine kutaka uchunguzi unaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa wa kina na wenye kujibu maswali yanayoulizwa na wengi juu ya wabunge hawa.

 

Kamati zilizoathirika Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

 

Wenyeviti wanaotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Sumbawanga, Hilary Aeshi, na wabunge wa Viti Maalum, Martha Mlata, na Dk. Mary Mwajelwa.

 

Wito wa JAMHURI ni kuona haki inatendeka. Hatutaki wabunge wetu wachafuke. Hatutaki chombo muhimu cha kutunga sheria kipate doa. Hatutaki taasisi zinazoripotiwa kutoa rushwa zivurugwe.

 

Kwa msingi huo, tunatoa wito kwa Takukuru kama chombo huru cha uchunguzi kufanya kazi yake kwa weledi kutoa taarifa itakayoondoa maswali tata yakiwamo yaliyowafanya baadhi ya wabunge, kama Zitto Kabwe na Hussein Bashe kuandika barua kwa Spika Ndugai kujiuzulu katika kamati hizo.

 

Ni matarajio yetu kuwa matokeo ya uchunguzi yatatangazwa hadharani na wabunge watakaobainika kuwa na hatia watachukuliwa hatua kali za kisheria iwe fundisho si kwa wabunge tu, bali kwa jamii nzima ya Tanzania. 

 

Tunamuunga mkono Spika Ndugai kwa hatua hii aliyoichukua. Mungu ibariki Tanzania.

1305 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!